Dar/Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kulisimamia shirika hilo kwa ubunifu, uadilifu na waweke mikakati ya kuendesha treni kibiashara ili tija iliyokusudiwa ipatikane haraka.
“Haitapendeza Serikali ikaendelea kulipa deni la fedha zilizokopwa kwa ajili ya ujenzi wa reli na kununua vitendea kazi, wakati shirika haliendi kwa faida, ingependeza sana shirika lifanye kwa faida ili lichangie kulipa deni,” amesema.
Rais Samia amesema hayo Agosti mosi, 2024 jijini Dodoma baada ya kuwasili akiwa kwenye treni hiyo kutoka Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya sherehe za uzinduzi rasmi wa safari hizo.
Amemtaka Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu kukaa na bodi ya shirika hilo na kuweka vigezo na vipimo vya utendaji kazi. Pia ahakikishe vinafuatiliwa kwa karibu.
Rais ameitaka Wizara ya Uchukuzi na Msajili wa Hazina kuhakikisha wakati wa uendeshaji wa reli za SGR na MGR kunakuwa na akaunti mbili tofauti za fedha na mifumo miwili ya uwajibikaji.
“Tukichanganya hatujui kipi kinatupa faida, kipi kinanyonya mwenziwe. Lakini tukizitenganisha tutakuwa makini katika kuendesha wa kila mfumo, na kila mfumo utasimamiwa vema,” amesema.
Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amesema Sh25 trilioni zimeshatumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa SGR kwa maeneo yote hadi sasa.
Pia amesema tangu kuanza kwa safari za treni ya umeme kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kufikia Julai 28, mwaka huu abiria 100,060 wamesafiri na kuingiza jumla ya Sh2.4 bilioni.
Baada ya kuanza kwa safari za Dar es Salaam hadi Dodoma Julai 25, amesema abiria 28,600 wamesafiri na kuingiza Sh744 milioni hadi leo Agosti mosi, 2024.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameagiza mifumo ya reli hiyo isomane na ya maziwa makuu na usafiri wa anga, ikiwemo kuingiza reli Terminal III ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA).
Pia ameagiza mifumo hiyohiyo itumike kuhakikisha ulinzi wa reli, ukataji tiketi na ufuatiliaji wa idadi ya abiria unafanyika.
“Tusingependa kusikia tunarudi tena kwenye tiketi za mkono, kwa hiyo hakikisheni mifumo yenu inalindwa ili isiingiliwe na wale wasiotutakia mema,” ameagiza.
“Hatutarajii TRC kuomba ruzuku kutoka serikalini, bali nasubiri gawio kutoka TRC kwenda serikalini, hivyo nimtake Msajili wa Hazina kufuatilia suala hili,” amesisitiza.
Katika hotuba yake Kadogosa alimwomba Rais stesheni ya Dodoma iitwe kwa jina lake Samia.
Baada ya Rais kukubali ombi hilo, aliendelea kuwaenzi maraia waliomtangulia kwa kuzipa stesheni nyingine majina yao, akianza na Tanzanite ya Dar es Salaam ambayo sasa itaitwa Magufuli.
Amesema stesheni ya Tabora ameipa jina la Rais wa awamu ya pili, hayati Ali Hassan Mwinyi.
Stesheni ya Shinyanga, itaitwa kwa jina la Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, ya Mwanza Mwalimu Julius Nyerere na Kigoma jina la Benjamin Mkapa.
Rais Samia amesema kwa kadri stesheni zitakapokuwa zinakamilika, atafikiria majina ya viongozi yanayopaswa kupewa miradi hiyo.
Wakati huohuo, Kadogosa amesema anatambua changamoto ya mkandarasi kutolipwa na kwa maelekezo ya Rais Samia hivi karibuni malipo hayo yatafanyika.
“Tunatambua changamoto ya kutokuwalipa wakandarasi na kupitia maelekezo yako tunafanyia kazi na najua kuna wakandarasi hapa wapo na hivi karibuni tutaanza kuwalipa yale madai yao,” amesema.
Mbali na hayo, ili kuepuka athari za kibiashara kwa wasafirishaji abiria kwa njia ya mabasi baada ya kuanza safari za treni ya umeme, Rais Samia amesema ipo fursa ya wasafirishaji kuunda ubia na TRC.
Ubia huo amesema utawezesha kuwa na tiketi moja itakayomwezesha abiria anayepanda treni, akishuka aitumie kupanda basi litakalomfikisha anakotaka.
Rais Samia ametoa pendekezo hilo wakati ambao wasafirishaji wa abiria kwa mabasi wameanza manung’uniko ya kudorora biashara zao baada ya kuanza safari za treni hiyo.
Kinacholalamikiwa zaidi ni huduma za treni kuwa bora na haraka zaidi ya mabasi, lakini Serikali imepanga nauli zinazofanana kwa aina hizo mbili za usafiri.
Pamoja na ubia huo, Rais ameitaka TRC kuhakikisha inawashirikisha wadau wa usafirishaji kwa njia ya mabasi na nyinginezo ili kufungamanisha reli na shughuli zao.
Kilichoelezwa na Rais Samia ndilo lililokuwa ombi la Taboa, wakiitaka Serikali ikae nao kuona namna watakavyokwenda.
Rais Samia amesema mradi huo utasaidia kupunguza msongamano wa magari barabarani, ajali na kusaidia usafirishaji kwa njia ya vifurushi.
Pia amesema utawezesha utunzaji wa mazingira kwa kuwa unatumia nishati ya umeme ambayo kimsingi haichafui hali ya hewa kama ilivyo kwa mafuta.