Balaa la Simba Day 2024… Unyama sana!

KAMA hadi sasa bado hujanunua tiketi ya Tamasha la Simba Day, baki nyumbani tu. Kwani hiyo kesho, ambapo kutakuwa na pati ya Simba Day, hutaweza kupata uhondo.

Mashabiki wa Simba wamefanya unyama sana kwa kuwekwa rekodi mpya kabla ya tamasha hilo lenye historia kubwa nchini, baada ya kumaliza tiketi za kwenda Kwa Mkapa siku tatu kabla.

Hii ni mara ya kwanza kwa Simba kumaliza tiketi hizo siku tatu kabla ya tamasha baada ya msimu uliopita kumaliza siku mbili kabla ya tamasha hilo linalofanyikia kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, na kama itakuwa hivyo, basi litahudhuriwa na mashabiki 60,000 (full house).

Huu ni msimu wa 16 wa Simba Day tangu lilipoasisiwa mwaka 2009, likiwa ndilo kongwe zaidi kwa klabu kwa hapa nchini.

Msimu uliopita Simba ilishindwa kufanya vizuri katika michuano iliyoshiriki kwa kukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikimaliza ya tatu, Kombe la Shirikisho, huku ikitolewa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini hiyo haijajalisha kwa mashabiki wa klabu hiyo, kwani wenyewe wameamua kufanya yao.

Hata hivyo, kuna sababu sita zilizosababisha Simba ikaweka rekodi hii mpya iliyoshindwa kuiweka hata wakati ambapo ilitwaa makombe mfululizo.

Simba imefanya usajili wa wachezaji wengi zaidi msimu huu tofauti na misimu minne iliyopita na mashabiki wa timu hiyo wanataka kuwaona wakiwa na uzi wa timu hiyo.

Baadhi ya wachezaji wapya wa timu hiyo ambao mashabiki wanasubiri kuwaona kwa mara ya kwanza ni Karaboue Chamou, Joshua Mutale, Omary Omary, Charles Ahoua, Steven Mukwala, Abdulrazak Hamza, Debora Mavambo, Yusuf Kagoma, Kelvin Kijili, Awesu Awesu, Augustine Okajepha, Valentino Mashaka na Valentin Nouma.

Kila shabiki wa timu hiyo anatamani kuwaona wachezaji hao wakiwa na jezi ya Simba kwa mara ya kwanza ndio sababu mojawapo iliyowafanya wanunue tiketi kwa wingi.

Moja ya jambo ambalo Simba imelifanya na limewafanya mashabiki wengi zaidi kununua tiketi ni kutowaona mastaa wake wakicheza kuanzia msimu wa Ligi Kuu Bara ulipomalizika.

Simba ikiwa tofauti na timu nyingine zilizocheza michezo ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi haijaruhusu mchezo hata mmoja kuonyeshwa kwenye televisheni tangu imeanza maandalizi ya msimu ujao.

Pamoja na kuwa kambini Misri, mabosi wa timu hiyo walizuia kitu chochote kurekodiwa katika michezo yao, lakini ilikizuia kituo kimoja cha televisheni kuonyesha mechi zote tatu ilizocheza nchini humo tofauti na watani wao, Yanga ambao mechi zao tatu ilizocheza Afrika Kusini zilionyeshwa mubashara.

Hii inawafanya mashabiki wa timu hiyo kutamani kwenda Kwa Mkapa kuona kikosi hicho kilicho chini ya benchi jipya chini ya kocha Fadlu Davids kinachezaje.

Misimu miwili nyuma kulionekana kuwapo mpasuko kwa baadhi ya viongozi wa zamani na wa sasa wa timu hiyo, lakini msimu huu hali imeonekana kuwa tofauti.

Mabosi wa zamani wa timu hiyo akiwemo muasisi wa Simba Day, Hassan Dalali, ameonekana sehemu mbalimbali akipigia debe mashabiki kwenda uwanjani katika tamasha hili jambo ambalo limeonekana kuwaunganisha pia mashabiki wa timu hiyo na kununua tiketi kwa wingi tofauti na nyuma ambapo kazi hiyo alikuwa akifanya Ahmed Ally pekee.

Kauli mbiu ya tamasha hili msimu huu ya Ubaya Ubwela imeonekana kuwateka mashabiki wengi ikionekana kuwa gumzo tangu Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Simba, Ahmed Ally alipoitangaza.

Kauli mbiu hii imeonekana kuwa maarufu msimu huu kuliko zile ambazo zimekuwa zikitumika kwenye tamasha hilo kwa misimu kadhaa ya nyuma, lakini pia mashabiki wa timu hiyo wameonekana kuitumia zaidi kuwakejeli wapinzani wao.

Hii ni suala jingine ambalo Simba imeonekana kufanikiwa kwenye tamasha la msimu huu baada ya kutoa jezi mpya za msimu mapema, lakini zikiwa zinapatikana kwa wingi madukani na kusifiwa kutokana na ubora wake.

Kabla ya tamasha la msimu uliopita mashabiki wa Simba walikuwa wakilalamika kuhusu upatikanaji wa jezi za timu hiyo hali ambayo iliwavunja moyo na wengi waliingia uwanjani wakiwa wamevaa jezi za msimu wa nyuma yake.

Msimu wa nyuma zaidi mashabiki hadi wanakwenda kwenye tamasha hilo walikuwa bado hawajapata jezi mpya, hivyo kitendo cha mashabiki kuwa na jezi mapema zikiwa na ubora zaidi kinawavutia zaidi kwenda uwanjani.

Kwa kipindi cha muda mrefu ambacho Simba imekuwa ikifanya tamasha hilo, limekuwa likiteka mashabiki wao na kuonekana kuwa sehemu ya burudani zaidi kutokana na mpangilio na wasanii ambao wamekuwa wakialikwa kuburudisha.

Kwa msimu huu kitendo cha mabosi wa timu hiyo kuwaalika wasanii wakubwa kama Ally Kiba, Joh Makini na Chino Kidd ni sababu nyingine iliyowafanya mashabiki kujitokeza kwa wingi kununua timu za tamasha hilo.

Ikiwa ni muda mrefu kwa wasaniii wawili, Joh Makini na Ally Kiba tangu walipofanya tamasha jijini Dar es Salaam, hivyo mashabiki wanatamani zaidi kuwaona mastaa hao wa muziki.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula alisema; “Simba tumeonyesha ukubwa wetu na tumeweza kuvunja rekodi yetu ya mwaka jana ambapo tuliuza tiketi zote siku mbili kabla ya Simba Day, mwaka huu tumeuza tiketi zote siku tatu kabla ya Simba Day.

“Hongereni sana mashabiki wetu na tukutane Uwanja wa Mkapa katika Simba Day ya Ubaya Ubwela. Timu yoyote kubwa inapimwa na ukubwa wa sapoti ya mashabiki wake, hii inadhihirisha kwa nini mashabiki wa Simba mlichaguliwa kuwa mashabiki bora barani Afrika.”

Akizungumzia suala hilo, Profesa Abel Kinyondo, alisema kitendo cha Simba kuuza tiketi zote siku tatu kabla ya mchezo wa ‘Simba Day’, sio jambo la kiuchumi, isipokuwa limekaa zaidi kwa mlengo wa kiutamaduni wa kikosi hicho uliojijengea.

“Tiketi kuuzwa zote huwezi kusema ni la kiuchumi kwa sababu kuna aina mbili ambazo zipo, ya kwanza ni ya uanachama na ya pili ni ya ushabiki, Simba iko katika hatua ya uanachama ndio maana wana kiu na shauku ya kuipigania timu yao,” alisema.

Abel aliongeza, unapokuja kwa mlengo wa kiushabiki ndipo unakutana na mashabiki wa Yanga, kwani wao wapo tayari kupewa vitu vya bure, ndio maana ikitangazwa kunywa supu utawaona kwa wingi kwa sababu hawana nia ya kuipagania klabu yao.

“Leo hii Ahmed Ally anapewa sifa kutokana na hamasa kubwa anayoifanya ila watu wanapaswa kutambua, hata kama Simba haina msemaji, amini kwamba itajaza uwanjani, kwa sababu wao wapo kwa mlengo wa uanachama kwa maana ya kupambania timu yao.”

Kwa upande wa Mtaalumu wa Uchumi, Oscar Mkude anasema kitendo cha Simba kumaliza tiketi mapema ni jambo nzuri kwa sababu linazidi kuonyesha klabu hiyo jinsi inavyojitangaza ndani na nje ya mipaka ya nchi, hususani kwenye suala la kibiashara.

“Hii inaonyesha soka linapiga hatua na sio hilo tu, kwa sababu unapojitangaza zaidi ndipo ambapo wachezaji kwa maana ya mmoja mmoja anazidi pia kujiuza, duniani kote tunaona wasanii na wanamichezo ndio watu wanaoingizia sana uchumi nchi.”

Mkude aliongeza, kwa Tanzania bado hatujapiga hatua kubwa kama nchi za wenzetu isipokuwa kuna mwanga mzuri unaonekana mbele, ndio maana michezo ya kubashiri imekuwa kwa kasi na inaingizia pato kubwa taifa, japo ina faida na hasara zake.

“Tunapiga hatua kubwa sana kwa sababu ukiangalia kuanzia katika soka au hata Bongo Movie utaona ni mtu mmoja mmoja kwa jitihada zake anajipambania ila anatangaza vizuri taifa letu nje ya mipaka, jambo ambalo linatuletea sifa hapa nchini.”

Related Posts