Tabora United yavuta winga Mkongo

TIMU ya Tabora United inaendelea kujiimarisha kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano mbalimbali ambapo sasa iko hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa winga Mkongomani, Heritier Kasongo Munani anayekipiga katika kikosi cha FC Lupopo.

Kasongo yupo katika mazungumzo na Tabora United huku ikielezwa ni mbadala sahihi wa aliyekuwa winga wa timu hiyo Mganda, Ben Nakibinge ambaye tayari amekamilisha uhamisho wake wa kukichezea kikosi cha Pamba Jiji kwa ajili ya msimu ujao.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Habari wa Tabora United, Christina Mwagala alisema, hajui taarifa juu ya mchezaji huyo huku akiweka wazi pindi watakapokamilisha kila kitu, ndipo ambapo watatangaza kwa mashabiki zao kama ambavyo wanafanya.

“Sijui chochote kuhusu hilo kwa sababu bado halijanifikia mezani kwangu, mambo yote yatakapokamilika tutayaweka wazi ila kwa sasa mashabiki zetu watarajie vitu vizuri vinakuja, tunaendelea na maandalizi kwa ajili ya msimu ujao,” alisema.

Nyota huyo aliyezaliwa Aprili 24, 1999, alijiunga na Lupopo Septemba 8, 2020, akitokea Racing Club de Kinshasa ya kwao DR Congo huku akisifika kwa uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kucheza kwa ufasaha winga zote kwa maana ya kulia na kushoto.

Mbali na Munani ila Mwanaspoti linatambua Tabora imekamilisha uhamisho wa kipa, Victor Sochima, beki wa kulia, Enyinnaya Kazie Godswill na kiungo mshambuliaji, Shedrack Asiegbu ambao wote wanatokea katika kikosi cha Rivers United ya Nigeria.

Nyota mwingine aliyekuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa kujiunga na timu hiyo ni Mnigeria mwingine, kiungo mkabaji, Morice Chukwu ambaye muda wowote atajiunga na kikosi hicho kwa mkopo akitokea Singida Black Stars.

Related Posts