KLABU ya Namungo imemuongezea mkataba mpya wa mwaka mmoja mshambuliaji wa timu hiyo, Meddie Kagere ili kuichezea msimu ujao.
Nyota huyo aliyecheza timu mbalimbali zikiwemo Gor Mahia na Simba, alijiunga na Namungo FC kwa mkopo akitokea Fountain Gate ingawa kwa sasa kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, kimefanikiwa kuipata saini yake ili kuendelea kusalia tena.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman alisema, ni kweli wamefanikiwa kumuongezea mkataba mpya nyota huyo baada ya ule wa miezi sita kumalizika, huku akieleza sababu kubwa iliyowashawishi ni uwezo wake aliokuwa nao.
“Hakuna mtu asiyejua uwezo na umuhimu wake kikosini ndio maana baada ya mkataba wake kuisha tulikaa naye na kumsikiliza mahitaji yake, kiukweli tunashukuru kuendelea kubaki na aina ya mshambuliaji kama yeye kwa msimu ujao,” alisema Ally.
Kwa upande wa kocha mkuu wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera alisema, wachezaji wote waliosajiliwa na wengine waliobakia ni mapendekezo yake, kwani anachotaka kukifanya ni kutengeneza timu imara itakayoleta ushindani katika mashindano tofauti tofauti.
Timu hiyo iliyoweka kambi ya maandalizi ya msimu Karatu jijini Arusha, tayari imenasa saini ya nyota wapya tisa ambao ni Beno Kakolanya, Djuma Shabani, Raphael Daud, Lenny Kisu, Erick Molongi, Anthony Mligo, Geofrey Julius, Moubarack Amza na Ritchi Nkoli.