LEO Aprili 26, 2024 ni siku 125 tangu aliyekuwa straika wa Simba, Jean Baleke alipofunga bao lake la nane, Desemba 23, 2023 dhidi ya KMC na hakuna mshambuliaji wa timu hiyo aliyefikia mabao hayo.
Baleke ambaye kwa sasa anaichezea Al-Ittihad ya Saudi Arabia alijiunga na Simba msimu wa 2022/23 kupitia usajili wa dirisha dogo na alimaliza akiwa na mabao manane, na ndio idadi ambayo kayafunga kabla ya kuondoka kikosini.
Simba iliachana na Baleke ikamsajili Freddy Koubalan ambaye hadi sasa amefunga mabao manne Ligi Kuu Bara, huku wanaoongoza kwa idadi ya mabao mengi Msimbazi ni Clatous Chama na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ kila mmoja ana saba.
Aprili 30, timu hiyo itacheza dhidi ya Namungo na
huenda kwenye mchezo huo Chama na Saido wakafunga au akatokea mwingine kufunga hat -trick ili kufikia mabao ya Baleke.
MABAO YA BALEKE
Mabao manane ya Baleke, aliyoyafunga Baleke ilikuwa ni dhidi ya Mtibwa Sugar (Agosti 17), Dodoma Jiji (Agosti 20, 23); Coastal Union (Septemba 21, 2023); Ihefu (Oktoba 28, 2023); Namungo (Novemba 9, 2023) na KMC (Desemba 23,2023).
WAONAVYO WAKONGWE
Anachojiuliza winga wa zamani wa timu hiyo, Steven Mapunda ‘Garrincha’ ni kitu gani kiliwashawishi viongozi wa Simba kuachana na Baleke ambaye alikuwa kwenye fomu nzuri ya kufunga na kuleta wengine ambao hawakuwa na uhakika wa kuizoea ligi mapema.
“Kuachana na mchezaji anayefanya vizuri dirisha dogo na kumsajili ambaye huna uhakika atakupa kitu gani ni jambo la hatari, sina maana kwamba Fredy ni mbaya, ila alihitaji kupata muda wa kuizoea Ligi Kuu,” amesema.
“Baleke angeendelea kuwepo Simba, angekuwa amefunga mabao mengi na huenda tungekuwa tunamuongelea kwenye levo ya ufungaji bora, siwezi kuwalaumu Saido na Chama kwa nafasi zao, wamejitahidi kila linalowezekana na nina imani watafunga mabao mengi zaidi.”
Mchezaji mwingine wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Gabriel ana imani huenda Saido na Chama wakafunga mabao mengi wakaingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kiatu cha ufungaji bora msimu huu.
“Bado mechi zipo nyingi. Wanaoongoza kwa kumiliki mabao mengi ni viungo, hivyo bado nina imani na Chama, Saido watafanya kazi nzuri hata kama imewachukua muda mrefu kuyafikia mabao ya Baleke,”amesema.