KLABU ya Simba imemtambulisha kipa mpya, Moussa Camara ‘Spider’ kwa mkataba wa miaka miwili akitokea AC Horoya ya Guinea.
Camara ni maarufu kwa jina la Spiderman, kwa umahiri wake wa kudaka mipira, ni raia wa Guinea mwenye umri wa miaka 25 amejiunga na klabu hiyo ya Msimbazi ili kuongeza nguvu katika eneo hilo baada ya Ayoub Lakred kuumia akiwa kambini jijini Ismailia, Misri.
Baada ya kusaini mkataba, kipa huyo anayeichezea pia timu ya taifa ya Guinea amesema anaushukuru uongozi wa Simba kwa kumpa nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi cha Mnyama.
Amesema Simba, ni timu kubwa na wachezaji wengi Afrika wana ndoto ya kuichezea kama ilivyokuwa kwake.
“Namshukuru Mungu kuwa hapa, pia nawashukuru viongozi wa Simba kunipa nafasi na kuniamini kuwa naweza kuwa sehemu ya timu hii,” amesema Camara na kuongeza;
“Nipo hapa kwa ajili ya kuhakikisha ninaisadia timu kufanya vizuri kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu.”