Dar es Salaam. Ikiwa imebaki takribani miezi miwili kufanyika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE), wanafunzi wa darasa la saba mkoani Dar es Salaam wamefanya mtihani wa kujipima wa mkoa (Mock) kwa mara ya pili.
Awali ulikuwa ukifanyika mara moja, siku chache kuelekea mtihani wa Taifa wa kumaliza elimu ya msingi ukitanguliwa na mithini ya kujipima ya kata na wilaya.
Baadhi ya walimu wamekiri wanafunzi kufanya mtihani huo juzi Julai 31 na jana Agosti mosi, 2024.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina, baadhi ya walimu wanadai kurudiwa mtihani huo kunatokana na matokeo mabaya ya ufaulu.
Kwa mujibu wa walimu hao matokeo mabaya yanatokana na kuchelewa kuanza kutumika mfumo mpya wa utungaji mitihani unaoondoa maswali ya kuchagua.
Inaelezwa mfumo huo ulianza kutumia Aprili, 2024 hivyo si watoto wala walimu waliokuwa wameandaliwa vizuri kuutumia.
“Serikali inapoamua kubadili haya mambo kwenye elimu kuwe na maandalizi ya mapema, hakukuwa na haja ya kuanza na mfumo mwaka huu, wangesogeza hadi mwakani ili watoto waandaliwe vizuri na si kama walivyofanya, kwani haiwapi tabu tu watoto bali hata na sisi walimu,” amesema mmoja wa walimu katika shule binafsi.
Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Gift Kiyando amethibitisha kufanyika mtihani huo mara ya pili, akieleza sababu ni kuwezesha wanafunzi kuzoea mfumo mpya wa utungwaji mtihani ambao umeanza mwaka huu.
“Hakuna uhusiano wa wanafunzi kufanya vibaya katika mtihani uliopita katika hili kama ulivyoambiwa, ila elewa tunafanya kwa ajili ya kuwapa mazoezi mengi zaidi wanafunzi kuulewa mfumo wa sasa wa utungwaji maswali ambao kwao ni mgeni,” amesema.
Tofauti na mfumo wa zamani ambao maswali yalikuwa ya kuchagua jibu sahihi na majibu mafupi kwa masomo yote, muongozo wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) unaelekeza kutakuwa na maswali ya kuchagua jibu sahihi, kuoanisha majibu mafupi, kupanga maneno au sentensi ili kuleta mtiririko wenye mantinki.
Maswali mengine ni kutafsiri picha, maswali ya utungaji au kukokotoa kulingana na matakwa ya somo husika.
Kwa somo la hisabati watahiniwa watatakiwa kukokotoa na kuandika majibu sahihi badala ya kuchagua majibu kutoka kwenye machaguo A hadi E.
Lengo la kuboreshwa kwa fomati hiyo ni kuimarisha utahini na umahiri, kuhakikisha wahitimu wana umahiri, weledi na uwezo wa kufikiri kwa kina, kuchambua mambo, kufanya uamuzi na kushauri.
Pia ni kuwawezesha kutumia maarifa wanayoyapata kukabiliana na changamoto za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni ndani ya nchi na duniani.
Mabadiliko hayo yanatokana na kufanyiwa kazi maoni ya wadau kuhusu kupunguza idadi ya maswali ya kuchagua ambayo yalikuwa 40 kati ya maswali 45 ya mtihani.
Akizungumza na Mwananchi, Dk Ave-Maria Semakafu amesema kinachofanywa siyo sahihi kwani inaonyesha namna gani bado elimu ya Tanzania ni kuwaandaa watoto kwa ajili ya kufanya mitihani na si elimu iende ikawasaidie katika maisha yao ya kila siku.
“Zamani tulikuwa tukisoma kuelewa somo husika lakini sasa hivi inasikitisha watoto wetu wanafundishwa kuja kufanya mtihani,” amesema.
“Pia mtihani wa Mock uliwekwa kwa ajili ya kumpima mtoto uelewa wake kuelekea mtihani wa Taifa, kulikuwa na haja gani ya kurudia kumpa mtihani huohuo tena, kinachofanywa hapa ni kuwakaririsha na si kuwafanya waelewe walichofundishwa,” amesema.
Ameiomba Serikali kuliangalia hilo kwani ukiacha gharama za kuchapisha mitihani, shule zimekuwa zikilipishwa na pia kuongeza gharama kwa wazazi na walezi ambao wanapaswa kuwalipia masomo ya ziada watoto ili kufaulu mitihani.
Dk Semakafu aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, amesema alifurahi Serikali ilivyoondoa mambo ya shule bora, kwa kuwa ndiyo yalikuwa yakichangia wanafunzi kukaririshwa na kueleza mtihani wa majaribio kufanyika mara mbili ni kama kutaka kurudi huko kwa kuwa mkoa unataka kuonekana umefaulisha zaidi ya mikoa mingine.
Haule Valeries, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Iringa amesema kama mwanafunzi amejengewa uelewa ni wazi hata mtihani uje katika mazingira gani ataweza kujibu maswali vizuri.
“Ni jambo la hatari kuwatathimini watoto kwa kuwafanyisha mitihani mingi, nadhani hizo nguvu zingeelekezwa zaidi katika kuwaandaa walimu kwa kuwapa mafunzo ya namna ya kuwafanya wanafunzi waelewe kile wanachowafundisha,” amesema.
“Nadhani Mkoa wa Dar es Salaam umefanya jambo sahihi ingawa tunaweza kusema muda uliobaki ni mchache sana kuelekea tarehe za kufanya mtihani wa Taifa lakini mitihani kwa ajili ya kutathmini utayari na uwezo wa watoto kuelekea mtihani wa Taifa nadhani si jambo baya,” amesema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chris Thomas.
“Kama wakiona kuna changamoto za kutoweza kufanya vizuri wasiwafanye wanafunzi wakachanganyikiwa bali wawape nguvu zaidi na kuwajenga kisaikolojia, amesema.
Amesema wanafunzi wakishindwa sana wasilaumiwe walimu au wanafunzi bali Baraza la Mitihani lililochelewa kutangaza utaratibu mpya.
“Ilitakiwa walimu na wanafunzi wajulishwe kuhusu mabadiliko haya tangu mwanzo wa mwaka ili waweze kujiandaa,” amesema.
Vailet James, mkazi wa Tabata amesema hata wao inawasikitisha kila mara wanapoona watoto wakifanya mithani na kujiuliza wanafundishwa saa ngapi lakini pia imekuwa ikiwachosha.
“Mitihani kwa watoto imezidi, hasa kwa shule binafsi, kuna ya kila siku asubuhi, kuna ya wiki, au mwisho wa juma, unajiuliza huyu mtoto anapumzika saa ngapi kufanya mitihani lakini kwa kuwa inabidi tufuate maelekezo ya walimu, hatuna namna kukubaliana nayo kwa kuwa ukikataa watoto wa wenzako wanaendelea,” amesema.
Chimo Kivamwa, mkazi wa Kimara amesema watoto wakifika madarasa ya mitihani wanakamuliwa, fedha kila siku zinahitajika za mitihani na wamezipa jina la re-medial ili waone ni kitu kigeni kumbe ndiyo hizohizo twisheni na kueleza kwa asiye na uwezo anaweza kujikuta mtoto wake akifeli kwa kushindwa kuhudhuria masomo hayo.