Makatekista waibuka kidedea kortini, shauri lao kusikilizwa upya

Songea. Kukiukwa kwa utaratibu wa kurekodi mwenendo wa shauri kwa kuandika maswali na majibu badala ya simulizi ya ushahidi, umewabeba makatekista wawili wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea baada ya kesi yao kuamriwa isikilizwe upya.

Kutokana na dosari hiyo ya kisheria iliyoibuliwa na mahakama yenyewe, Jaji James Karayemaha wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Kanda ya Songea, ameamuru shauri hilo lisikilizwe upya na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).

Hayo yamo katika hukumu iliyotolewa na Jaji Agosti 1, 2024, baada ya kusikiliza rufaa iliyokatwa na makatista hao wawili, Renister Mnenuka na Bernard Mbecha dhidi ya Mkurugenzi wa Miito Jimbo na Makatekista Jimbo Katoliki Songea.

Katika rufaa ya shauri hilo la kazi namba 8482 la mwaka 2024 ambalo lilitokana na uamuzi wa CMA uliotolewa Oktoba 24, 2023, Bodi ya Wadhamini Jimbo Kuu Katoliki Songea nayo iliunganishwa katika shauri hilo kama mdaiwa wa pili.

Kulingana na mwenendo wa shauri hilo lilivyoendeshwa CMA, makatekista hao walidai kuwa walifanya kazi ya Ukatekista tangu mwaka 1994 hadi Febriari 23, 2019 waliposimamishwa kutoa huduma na wadaiwa hao kwa tuhuma za wizi.

Ilidaiwa wawili hao waliiba Siborio (Ciborium) katika Parokia ya Bombambili katika kituo cha Msamala walikokuwa wakihudumu kama makatekista. Ciborio hutumika kuweka hostia zilizobarikiwa ambazo kwa Wakatoliki wanaamini ni mwili wa Kristo.

Baada ya kusimamishwa kazi, walifungua malalamiko mbele ya kamishina wa CMA Songea wakipinga kusimamishwa kazi na kuomba tume hiyo iwarudishe kazini bila masharti katika nafasi walizokuwepo na kuwalipa stahiki zao zote.

Hata hivyo, maombi yao hayo yalipingwa na wadaiwa kwa maelezo kuwa hawakuwahi kuwaajiri wawili hao kama makatekista kwa kuwa wao huwa hawaajiri mtu yeyote kama katekista na mwishoni CMA ikawapa ushindi wadaiwa.

Walivyokata rufaa Mahakama Kuu

Kutokana na kutoridhishwa na uamuzi huo na kupitia kwa mwakilishi Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), Daud Mbonde, walifungua maombi Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Kanda ya Songea wakiiomba ipitie upya uamuzi huo wa CMA.

Wadaiwa katika maombi hayo walitetewa na wakili Optatus Japhet ambapo mbali na jaji kuwapongeza waombaji na wajibu maombi kwa hoja zao nzuri katika mawasilisho yao ya maandishi, asingeshughulika kuamua hoja zao hizo.

Badala yake, Jaji akasema atajikita katika hoja zilizoibuliwa na mahakama yenyewe (suo mottu) kuhusiana na namna CMA ilivyorekodi mwenendo wa shauri hilo hususan mahojiano ya msingi na ya nyongeza ya mfumo wa maswali na majibu.

Katika kujibu hoja hiyo iliyoibuliwa na mahakama, Mbonde aliiomba mahakama ilirejeshe jalada la shauri hilo CMA ili lisikilizwe upya na hiyo Jaji alisema pengine ni baada ya kubaini mwenendo uliandikwa kwa mfumo wa maswali na majibu.

Jaji alisema ingawa Wakili Optatus alifahamu kufunguliwa kusikilizwa kwa hoja hiyo mahususi, hakutokea mahakamani kuwasilisha hoja ya upande wake.

Hukumu ya Jaji ilivyokuwa

Katika hukumu yake, Jaji Karayemaha alisema ni msimamo wa kisheria kuwa ushahidi wa mashahidi ni lazima uchukuliwe katika mfumo mahususi ingawa katika mashauri ya kazi haitoi mfumo mahususi wa namna ya kurekodi ushahidi.

Hata hivyo, pamoja na kutotoa utaratibu mahususi, lakini kwa mazoea ya kivitendo ya ufanyaji kazi (practice) kwamba ushahidi ni lazima uchukuliwe katika mfumo wa simulizi (narration) na mfumo wa maswali na majibu hauhamasishwi kutumika.

Jaji alisema kanuni ya 32(3) sheria za kazi kuhusiana na usuluhishi iliyotangazwa katika gazeti la Serikali (GN) namba 64 ya 2007 inamtaka msuluhishi kurekodi muhtasari wa ushahidi uliotolewa lakini hairuhusu mfumo wa maswali na majibu.

Kulingana na Jaji, alisema hakuna ubishi kuwa msuluhishi katika shauri hilo alirekodi ushahidi wa mashahidi katika mfumo wa maswali na majibu lakini hoja inayopaswa kujibiwa na mahakama ni nini athari za dosari hizo kisheria.

Jaji alinukuu misimamo mbalimbali ya kisheria kutokana na kesi zilizokumbana na mazingira kama ya kesi hiyo ambazo ilisisitizwa ushahidi kuchukuliwa kwa maandishi lakini sio kwa mfumo wa swali na jibu bali kwa mfumo wa simulizi.

Kutokana na msimamo huo, Jaji alisema anakubaliana na misimamo hiyo ya kisheria kuwa ushahidi uliochukuliwa kwa mfumo wa maswali na majibu unakiuka sheria hivyo maana yake katika kesi hiyo kulikuwa hakuna ushahidi katika hatua ya uulizwaji maswali na majibu ya ziada, ambayo CMA iliegemea kutoka uamuzi.

Dosari hiyo kwa mujibu wa jaji ni kubwa na suluhusho pekee ni kurudisha jalada la shauri hilo CMA kwa ajili ya shauri hilo kusikilizwa upya ili kutenda haki kwa pande zote kulingana na msimamo wa sheria.

Related Posts