Mbeya. Mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi mkoani Mbeya, Hawa Mathias ameibuka mshindi wa tuzo ya umahiri wa uandishi wa habari za ‘Tulia Trust Journalism Awards’ katika kipengele cha afya.
Kwenye tuzo hizo ambazo ni za pili kufanyika, mwaka huu jumla ya kazi 90 ziliwasilishwa katika makundi mbalimbali zilizochapishwa au kutangazwa kwenye magazeti, redio, televisheni au mitandao ya kijamii.
Waandishi wengine walioshinda ni Kakuru Msimu (Azam Media), aliyeibuka mshindi wa jumla, Nebart Msokwa aliyeshinda kipengele cha Picha Bora huku Rebecca Kinyunyu wa ITV akishinda tuzo ya Mazingira.
Wengine ni Keneth Ngelesi wa EATV, aliyeshinda kipengele cha Habari za Uchunguzi, Isack Kyando (Utalii na Maliasili), Rashid Mkwinda (Siasa), Ipyana Njiku (Kilimo, Mifugo na Uvuvi) na Enock Fumbo aliyeshinda kipengele cha Madini na Gesi.
Akizungumza baada ya kutwaa tuzo hiyo, Hawa amesema itakuwa chachu kwake katika kufanya kazi kwa uadilifu na kujituma kwa kuzingatia maadili ya kitaaluma.
“Najivunia tuzo na ushindi huu ambao kwangu ni chachu katika kuendelea kupambana kufanya kazi kwa misingi ya kitaaluma kuhakikisha nafikia ndoto zangu na kuitambua jitihada na ushauri wa wahariri wanaotusimamia” amesema Hawa.
Mapema akitoa salamu katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo jana usiku, Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Ayasi Njalambaha amewataka waandishi wa habari kuzingatia miiko ya uandishi wa habari, haswa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
Amesema pamoja na kazi nzuri za waandishi, lazima wajiridhishe kuhusu usahihi wa habari ili kukwepa migongano, migogoro na taharuki, na kuwa waaandike habari zenye tija kwa masilahi ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amesema pamoja na kazi nzuri wanayofanya, waandishi wa habari wasijisahau katika nyanja ya kiuchumi kuhakikisha wanatumia uandishi wao kuinua kipato binafsi.
“Mnapokuwa katika majukumu yenu, hakikisheni mnatumia vema nafasi yenu kujiinua kiuchumi, msijisahau kwa ajili ya maisha yenu ya baadaye, haswa kupitia tuzo hizi,” amesema Malisa.
Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera amesema kwa ubunifu aliofanya Dk Tulia ni wa kuigwa kutokana na kuthamini taaluma ya habari kuwa ajira na kuamua kuwasapoti waandishi wa habari.