TAKUKURU wakamata watumishi wa serikali kwa tuhuma za kuomba rushwa ‘tutaendelea kukamata”

Wakurugenzi wa halmashauri wametakiwa kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale wanaohusika kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Njombe.

Kauli hiyo imetolewa April 25,2024 na kamanda wa Takukuru mkoa wa Njombe Kassim Ephrem wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo.

Amesema mkurugenzi anapelekewa ripoti ya mradi uliotembelewa na Takukuru na kubaini mapungufu wanategemea kuona mkurugenzi anachukua hatua kwani upo uwezekano wa kupewa taarifa za uongo na mhandisi anayemuamini.

Amesema mkurugenzi mradi upo kwenye eneo lake na Takukuru wamechunguza na kubaini mapungufu lakini wanaandika barua na kusaini lakini hakuna mrejesho wanaoupata kutoka ofisi ya mkurugenzi juu ya kile walichokibaini.

“Mkurugenzi mradi upo kwenye eneo lako tumeenda Takukuru tumekuletea barua tekeleza basi haraka ili mradi uonekane muite mhandisi wako ili kama anakulisha matangopori uone Takukuru wamenisaidia kwa kunipa taarifa hii” amesema Ephrem.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuzuia miradi hiyo isiwe na mapungufu makubwa ambayo itapelekea hasara kubwa kwa serikali ambayo lengo lake ni kusogeza huduma kwa wananchi.

Amesema sehemu nyingine ambayo wamebaini ni wahandisi kutotembelea miradi mara kwa mara ambapo hiyo inachangia miradi kutojengwa kwa viwango vinavyotakiwa.

“Wahandisi jengeni tabia ya kutembelea miradi ya halmashauri na ile mingine ya serikali ili utoe maelekezo pale unapoona kuna mapungufu ili kama kuna malalamiko yoyote upeleke kwa mkurugenzi ili atatue changamoto iliyojitokeza” amesema Ephrem.

 

Amesema wahandisi kushindwa kufuatilia miradi wanayosimamia kunaweza kusababisha kupelekwa mahakamani kama umeshiriki kwenye mbinu ya kukwamisha utekelezaji wa miradi ya wananchi.

 

Amesema taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi 2024 jumla ya miradi 21 imefuatiliwa ambayo thamani yake ni Sh. 7.3 bilioni.

 

Amesema katika miradi hiyo sita ambayo thamani yake ni Sh. 4.4 bilioni imebainika kuwa na mapungufu mbalimbali ambayo wameagiza yafanyiwe kazi.

 

Amesema kuelekea kuupokea mwenge wa uhuru mkoani Njombe wakurugenzi wa halmashauri wanatakiwa kuhakikisha nyaraka za miradi itakayotembelewa na mwenge zipo vizuri.

 

Amesema miradi ambayo mwenge inatembelea halmashauri inachagua yenyewe kuwa itapitiwa lakini mwisho wa siku inakataliwa hilo halijakaa sawa na aibu.

 

Aidha amesema bila kutaja majina na maeneo,TAKUKURU imewakamata watendaji wawili wa kata wamekamatwa taasisi hiyo na kesi ipo mahakamani kutokana na tuhuma zinazowakabili za kudai na kuomba rushwa.

 

“Tumekamata watendaji,yani mtendaji unapata mshahara lakini unadai shilingi laki moja,kituo cha afya unamzungusha mtu baada ya kumhudumia unadai elfu ishirini ni aibu tunaombeni watumishi tujirekebishe tutawakamata”amesema Ephrem

 

Amewakumbusha wanachama wa vyama vya siasa kufuata miiko na maadili ya vyama vyao kwa kuepuka vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi.

 

Amesema wapo baadhi ya wanachama wanaanza kufanya vitendo ambavyo si vya kimaadili na miiko ya vyama vyao.

 

“Tunawaombeni sana viongozi wa vyama ni aibu mwanachama anafanya vitendo ambavyo chama inavikataza na viongozi mnakaa kimya”amesema Ephrem.

 

Katibu wa Siasa na Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe Josaya Luoga amesema chama hicho kinatoa tahadhari kwa wanachama wa chama hicho kujihusisha na vitendo vya rushwa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi.

 

“Nawaonya wanachama wa chama hiki wanaotumia viongozi kutoa misaada kinyume na taratibu zilizowekwa kwa viongozi mpaka sasa wapo na muda wa uchaguzi haujafika” amesema Josaya.

Related Posts