Kesho ndio kilele cha Tamasha la Simba Day kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambako wenyeji Simba SC wanatarajia kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya APR ya Rwanda.
Huu utakuwa ni msimu wa 16 wa Tamasha la Simba Day lililoasisiwa mwaka 2009 chini ya uongozi wa Mzee Hassan Dalali na Mwina Kaduguda.
Kuelekea msimu wa 2024-2025, Simba imetangaza kusajili wachezaji wapya 13. Kati ya hao raia wa kigeni ni saba ambao ni Valentin Nouma, Chamou Karaboue, Charles Ahoua, Debora Mavambo, Augustine Okejepha, Joshua Mutale na Steven Mukwala.
Wazawa ni Kelvin Kijiri, Abdulrazack Hamza, Yusuph Kagoma, Awesu Awesu, Omary Omary na Valentino Mashaka. Lameck Lawi alikuwa wa kwanza kutambulishwa lakini usajili wake umezua utata, na hivyo hayupo kambini.
Mashabiki wa Simba wana imani kubwa na timu yao kuelekea msimu ujao ambapo kupitia wachezaji wapya na wa zamani, wanaona makombe yanarudi Msimbazi baada ya kusuasua kwa kipindi cha misimu mitatu mfululizo.
Kuna rekodi mbalimbali zimewekwa ndani ya Simba tangu 2009 ambapo Mwanaspoti linakuletea matokeo ya mechi zote 15 za kirafiki zilizochezwa Simba Day.
Msimu wa kwanza wa Simba Day 2009, Simba ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya SC Villa ya Uganda kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar wakati huo ukiitwa Uwanja wa Taifa.
Bao pekee la kiungo Mkenya, Hilary Echessa katika dakika ya 8 lilitosha kuipa Simba ushindi wa 1-0. Kiungo huyo alikuwa ndiyo kwanza amesajiliwa kutoka SC Villa.
Kipindi hicho, Simba ilikuwa chini ya kocha Mzambia, Patrick Phiri na msimu huo ikaandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza katika historia ya soka la Tanzania kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara bila kupoteza mchezo, huku nyota wa Uganda, Emmanuel Okwi na Joseph Owino walikuwa wamesajiliwa kwa mara ya kwanza.
Msimu wa pili Simba Day 2010, Simba ikiwa chini ya kocha Phiri ikacheza dhidi ya Express ya Uganda, timu hazikufungana.
Hii ndio mechi pekee ya Simba Day iliyomalizika bila ya bao kufungwa baada ya timu hizo mbili kutoka suluhu kwenye Uwanja wa Uhuru wakati huo ukiitwa Uwanja wa Taifa.
Ilikuwa ni kama vile Simba imeganda nchini Uganda kwani katika msimu wa tatu wa Simba Day 2011, waliialika timu nyingine kutoka huko ambayo ni Victors.
Mechi hiyo iliweka rekodi mbili, kuchezwa kwa mara ya kwanza nje ya Dar es Salaam kwani ilipigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, kisha kushuhudiwa Simba ikipoteza kwa mara ya kwanza ikilala kwa bao 1-0.
Bao hilo liliwekwa kimiani katika dakika ya 70, kwa mkwaju wa penalti na Patrick Sembuya. Ulikuwa ni mwanzo mbaya wa kocha mpya wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic.
SIMBA 1-3 NAIROBI CITY STARS
Cirkovic hakuwa na upepo na Simba Day 2012 kwa msimu wake wa pili kushiriki tamasha hilo ambalo lilifanyika kwa mara ya nne, alipokea kichapo kutoka Nairobi City Stars ya Kenya.
Mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Taifa (sasa hivi Benjamin Mkapa) na mabao ya washindi yakiwekwa kimiani na Duncan Owiti (dk.57), Bruno Okullu (dk.69) na Boniphace Onyango (dk.79), huku bao la Simba likifungwa na Mzambia, Felix Sunzu mapema tu dakika ya 15.
Baada ya Simba Day tatu mfululizo kutopata matokeo mazuri, Simba ikaamua kurudia kwa ‘kibonde’ wake SC Villa ambaye walimchapa msimu wa kwanza 1-0.
Safari hii wakapata ushindi mnono wa mabao 4-1, mchezo ukipigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Simba ikiwa chini kocha Abdallah Kibadeni aliyechukua nafasi ya Cirkovic. Ilikuwa mwaka 2013.
Kiungo chipukizi wa kipindi hicho Jonas Mkude alifungua pazia kwa bao la dakika ya 43, kabla ya chipukizi mwingine William Lucian ‘Gallas’ kuweka chuma cha pili katika dakika ya 53 na mkongwe Betram Mombeki alifunga mabao mawili katika dakika ya 70 na 72.
Simba ikabadili upepo wa kucheza na timu za Afrika Mashariki, safari hii ikaialika Zesco kutoka Zambia, ikawa bahati mbaya kwao kwani walichapika mabao 3-0.
Kocha Mcroatia Zdravko Logarusic alikutana na kipigo hicho kutoka kwa Wazambia ambao walipata mabao yao kupitia kwa Jackson Mwanza (dk.14), Clatous Chama (penalti dk.64) na Mayban Mwamba (dk.90). Hii ni mwaka 2014.
Baadaye Chama alijiunga na Simba 2018 ambapo amedumu hapo hadi 2024 alipotimkia Yanga anakosubiriwa kwa hamu kuanza kazi rasmi msimu ujao wa 2024-2025.
Tamasha la saba katika Simba Day 2015 ilishuhudiwa SC Villa ikirudi tena nchini kwa mara ya tatu kuvaana na Simba na kama kawaida iliendelea kuwa vibonde kwa kufungwa bao 1-0.
Bao pekee la Simba liliwekwa kimiani na kiungo Awadh Juma katika dakika ya 89. Kocha alikuwa Mwingereza, Dylan Kerr.
Msimu wa nane wa Simba Day 2016 ulihitimishwa kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya AFC Leopards ya Kenya.
Ibrahim Ajibu ndiye aliyekuwa shujaa wa mchezo huo kwa kufunga mabao mawili, huku straika Mrundi aliyekuwa amejiunga na timu hiyo akitokea Vital’O, Laudit Mavugo akitupia moja kambani.
Winga, Shiza Kichuya aliyekuwa akiicheza Simba kwa mara ya kwanza akitokea Mtibwa Sugar alifunga bao jingine. Kocha alikuwa Joseph Omog raia wa Cameroon.
Simba ilishinda bao 1-0 dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda kupitia mfungaji Mohammed Ibrahim aliyemalizia pasi ya Emmanuel Okwi katika dakika ya 15. Simba Day ya 2017 Kkocha alikuwa Omog.
Katika mechi hii Simba ikiwa chini ya kocha Mbelgiji Patrick Aussems ilisawazisha bao katika dakika 75, kupitia kwa mshambuliaji wake Mganda Emmanuel Okwi. Ilikuwa mwaka 2018.
Kocha Patrick Aussems aliiongoza Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 yaliyofungwa na Meddie Kagere ambaye alipiga hat-trick katika dakika ya 3, 58 na 73. Ilikuwa mwaka 2019, akaweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao matatu katika mechi moja ya Tamasha la Simba Day.
Kocha Sven Vandenbroeck ilikuwa zamu yake kuinoa Simba katika Simba Day 2020, akapata ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Vita’O ya Burundi. Akaweka rekodi ya kupata ushindi mkubwa zaidi katika tamasha hilo.
Hata hivyo, Simba ilisubiri hadi dakika ya 43 kupata bao la kwanza kupitia Bernard Morrison. Dakika mbili mbele, Morrison alitengeneza pasi kwa nahodha wa Simba, John Bocco ambaye alipachika bao la pili katika dakika ya 45.
Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili, Simba ilifanya mabadiliko kwa wachezaji wake wote ambao walianza kikosi cha kwanza.
Kikosi cha pili kilipachika mabao manne ambapo bao la tatu lilifungwa na Clatous Chama katika dakika ya 56 akimalizia pasi ya Ibrahim Ajibu ambaye naye alifunga bao la nne katika dakika ya 75 kwa pasi ya Chama, kisha bao la tano likafungwa na Chris Mugalu (dk77) kwa pasi ya Miraj Athuman huku Charles Ilanfya akafunga la mwisho kwa pasi ya Mohamed Hussein.
Kocha Didier Gomes alikaribishwa na kichapo katika Simba Day kutoka kwa TP Mazembe ya DR Congo, muuaji akiwa ni Jean Baleke aliyefunga katika dakika ya 83, ilikuwa mwaka 2021. Kumbuka mshambuliaji huyo baadaye alijiunga na Simba kabla ya sasa kutua Yanga 2024.
Simba hawakutaka kuharibu sherehe yao mwaka 2022, walitoa dozi ya mabao 2-0 dhidi ya St. George SC ya Ethiopia.
Mabao ya Simba yalifungwa na Kibu Dennis (dk18) na Nelson Okwa (dk59). Kocha alikuwa Zoran Maki ambaye alikaa kwa takribani miezi miwili, akasepa.
Simba Day iliyopita mwaka 2023, ilikuwa siku nzuri kwa wachezaji wapya waliotambulishwa siku hiyo, Willy Onana aliyefunga bao dakika ya 4 na Fabrice Ngoma akipachika bao katika dakika ya 75.
Kocha Roberto Oliveira aliiongoza Simba kuifunga Power Dynamos ya Zambia katika mchezo huo. Simba Day ya mwaka huu, Robertinho hayupo, lakini Onana na Ngoma bado wapo.