Mitihani migumu aliyopitia Waziri Stergomena Tax

Dar es Salaam. Pengine kila anayeonekana na mafanikio leo, zipo nyakati ngumu alizopitia jana ambazo kama si kuvaa kibwebwe asingeupata umaarufu alionao.

Katika hili, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax ni kielelezo sahihi; anayesimulia magumu aliyowahi kupitia katika safari yake ya kuisaka elimu.

Kwa mujibu wa waziri huyo ambaye ni mwanamke wa kwanza kuiongoza wizara hiyo, magumu hayo yalitokana na kigugumizi cha nini alipaswa kuchagua kati ya kulea mtoto au kwenda nje ya nchi kujiendeleza na elimu.

Ingawa wakati huo, mwanawe huyo alikuwa na umri wa miaka minne, anasema kwa mzazi isingekuwa rahisi kukubali kumwacha kisha asafiri kwenda nje ya nchi kwa zaidi ya mwaka.

Kudharauliwa kutokana na jinsi yake, maswali yenye chembechembe za ukandamizaji wa kijinsia ni magumu mengine anayosimulia kama sehemu ya vikwazo ambavyo bila mapambano, pengine asingekuwa waziri anayeonekana sasa.

Dk Tax ameyasema hayo leo Ijumaa, Agosti 2, 2024 alipozungumza katika uzinduzi wa Redio Malkia Choice FM inayoendeshwa na kurusha matangazo yenye maudhui ya wanawake pekee.

Anasimulia changamoto hiyo ilimkabili miaka minne baada ya kuolewa na kuwa na mtoto, wakati huo huo alipata nafasi ya masomo nje ya Tanzania.

“Nilijiuliza nitafanyaje kuhusu mtoto maana kusoma nataka, kumlea mwanangu nataka nilikuwa katikati. Lakini baadaye nilifanya uamuzi mgumu wa kumwacha na kwenda kusoma,” amesema.

Ingawa ulikuwa uamuzi mgumu, anasema ndani yake alikuwa anafikiria mbinu gani itakayomwezesha kutengeneza mazingira ya baadaye kumchukua mwanawe ili awe naye nje ya nchi.

“Miezi sita baadaye nilifanikiwa kutengeneza mazingira na nikamchukua mwanangu na kuwa naye nje ya nchi,” amesema.

Mtihani mwingine anasema ulikuwa namna ya kutenga muda wa kusoma lakini wakati huo huo azingatie huduma za mtoto na ukizingatia alikuwa katika taifa lisilo lake.

Juhudi pekee, anaeleza ndizo zilizomwezesha kufanikisha hilo na baadaye alifaulu vema na kutakiwa kuendelea na masomo ya shahada ya uzamivu katika mazingira hayo hayo.

Baada ya mafanikio hayo, anasema kwa kuwa alishazoea mazingira mumewe pia alikwenda nchini humo na akawa anamsaidia shughuli mbalimbali zikiwemo kazi za nyumbani.

“Wanaume ni watu wa ajabu sana tulivyokuwa kule (nje ya nchi) alikuwa anafanya kila kitu lakini alivyorudi akaacha kila kitu. Nilimuuliza siku moja mbona ulipokuwa kule ulikuwa unanisaidia kila kitu hadi kuosha vyombo lakini tumerudi nchini umeacha.

“Akaniambia wewe una akili kweli? dada yangu anikute naosha vyombo atanielewaje,” anasema.

Changamoto nyingine anayosema pengine ndiyo iliyosababisha hata ateuliwe katika wizara hiyo, anasema ni uamuzi wa kupendekeza nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kujitegemea kwa vikosi vya ulinzi na usalama panapokuwa na  machafuko.

“Nikiwa Katibu Mkuu wa SADC, nimekuta tunajisifu kwamba jumuiya iko vema,  lakini kwenye ulinzi na usalama  tulikuwa tegemezi wanapotaka kudeploy  mission (kupeleka vikosi) tulilazimika kuwa omba omba,” anasema.

Katika mazingira hayo, anasimulia alivyotaka kutengenezwa kwa  bajeti ya SADC itakayowezesha kuwa na vikosi vyao, jambo alilopata upinzani mkubwa kutoka kwa timu yake.

Anaeleza wengi walimpinga kabla hata hajalifikisha kwa wakuu wa nchi kuliwasilisha, lakini aling’ang’ana hadi alipopata nafasi ya kuliwasilisha.

“Siku nilipoliwasilisha lilipitishwa na mwaka huo ndipo tulipoanza kudeploy mission ya kwanza  Msumbiji kwa fedha za ndani,” anasema Dk Tax.

Mitihani mingine iliyowahi kumkabili, anasema ni kupewa majukumu huku akiwa haaminiki kutokana na jinsi yake, lakini amekuwa akiwashangaza wanaompa kwani alitekeleza kama ilivyotakiwa.

“Nimeivuka kwa urahisi mitihani hii kwa sababu kwanza najiamini, ninapopewa jukumu natumia juhudi na bidii kulitekeleza inavyotakiwa,” amesema.

Anaeleza changamoto iliyopo kwa baadhi ya wanawake, hupenda kujidharau na kutanguliza udhaifu kabla hata jamii haijawatazama kwa tafsiri hiyo.

“Wewe mwenyewe unasema mimi ni mwanamke hii siiwezi badala ya kuangalia wewe daktari na mimi daktari basi naweza kama mwingine,” amesema.

Mkurugenzi wa redio hiyo, Johayna Kusaga amesema wanacholenga ni kutengeneza jukwaa linalolenga masuala ya wanawake na litajadili maudhui yanayoihusu jinsi hiyo.

“Tunatarajiwa wanaume pia watasikiliza kwa sababu sisi ni mama zao, wake zao na tumehusika katika kuhakikisha wanafika walipofika,” anasema.

Anaeleza katika redio hiyo wafanyakazi wote watakuwa wanawake na wasichana, akisisitiza haitakuwa ya kusutana kama wengine wanavyotafsiri.

Dk Tax aliyezaliwa Julai 6, 1960, alianza utumishi wa umma mwaka 1991, katika Wizara ya Fedha, akihusika na masuala ya kutoa misaada na usimamizi hadi mwaka 2002.

Baadaye mwaka 2006, aliteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, alikohudumu hadi mwaka 2007.

Mwaka 2008, alihudumu kama Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje hadi 2013, kisha Mkutano wa 33 wa Wakuu wa Nchi za SADC uliofanyika katika jiji la Lilongwe nchini Malawi, ulimteua kuwa Katibu Mtendaji wa jumuiya hiyo.

Septemba mwaka 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alimteua kuwa Mbunge kisha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Baadaye alimbadilisha kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Oktoba mwaka 2022, Rais Samia alimteua tena Dk Tax kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wadhifa anaohudumu hadi sasa.

Related Posts