Ukaguzi wa CAG wabaini madudu ujenzi hospitali 11

Unguja. Ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), umebaini dosari katika ujenzi wa hospitali 10 za wilaya na moja ya mkoa, zikisababisha hasara ya mamilioni ya fedha na muundo wa majengo kuwa chini ya viwango.

Mbali na hayo, maeneo ya ujenzi hayakufanyiwa uchunguzi na mjiolojia kubainisha usalama wa ardhi, hivyo athari zimeanza kujitokeza katika baadhi ya hospitali kwa kuwa na nyufa kutokana na eneo kutokuwa rafiki kwa ujenzi.

Ripoti ya ukaguzi wa kiufundi ya mwaka 2022/23 iliwasilishwa kwa muhtasari na Dk Abbas Ali Othman, Mei 13, 2024 kwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Ikulu Zanzibar kisha vitabu vya ukaguzi huo kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi Juni 27, 2024 kwa ajili ya kujadiliwa. Itajadiliwa kwenye vikao vijavyo vya baraza hilo.

Machi 11, 2020 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko wa virusi vya Uviko-19  kuwa janga la kimataifa.

Ili kukabiliana kikamilifu na janga hilo, Serikali ya Tanzania ilipokea Sh1 trilioni kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) chini ya mpango wa mikopo ya haraka (RCF). Katika kiasi hicho cha fedha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ilipokea Sh230 bilioni.

Kutokana na ugonjwa huo, Serikali iliona umuhimu wa kuongeza hospitali ili kukabiliana na janga hilo. Awali SMZ ilitenga Sh72.8 bilioni kwa sekta ya afya kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hizo na usambazaji wa vifaatiba.

Licha ya kutenga kiasi hicho, baadaye ziliongezeka gharama za ziada Sh19.2 bilioni kutoka kwenye kiasi cha mkataba wa awali.

Ujenzi huo ulihusisha hospitali moja ya Mkoa ya Lumumba na hospitali 10 za wilaya katika wilaya zote 10 hivyo kufanya hospitali zote zilizojengwa kufikia 11.

Ripoti ya CAG inasema chimbuko la ukaguzi huo linatokana na mambo mawili: Gharama kubwa za ujenzi zilizotajwa na dosari za kiutendaji, na gharama za juu za ukarabati wa mradi huo.

Pamoja na nia nzuri ya kuimarisha afya,  ukaguzi umebaini hakuna uchunguzi wowote wa kijiolojia uliofanyika kabla ya kuanza kwa ujenzi huo.

Ripoti inasema hali hiyo imechangiwa na upangaji usioridhisha wa utekelezaji wa miradi na dosari kwa mhandisi kwa kushindwa kusimamia vyema kanuni za maadili za Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), kwa kushindwa kuishauri Wizara ya Afya kuhusu kufanyika uchunguzi wa kijiolojia.

Kwa mujibu wa kifungu namba tatu cha Sheria ya Maadili ya Wahandisi ya mwaka 2020, mhandisi atajitahidi kusimamia na kuendeleza uadilifu na heshima ya taaluma ya uhandisi.

“Kushindwa kufanyika ukaguzi wa kijiolojia kunaweza kusababisha kuandaa muundo wa msingi wa jengo bila kujumuisha vihatarishi vya eneo la ujenzi kama vile makazi ya udongo, maporomoko ya ardhi au hatari zingine za kijiolojia ambazo zinaweza kuhatarisha uimara wa jengo pamoja na usalama wa muda mrefu wa jengo,” amesema.

CAG amebainisha hali hiyo imejitokeza katika moja ya hospitali hizo ambayo ilikuwa na nyufa za miundo kwenye kuta na nguzo za jengo ambalo lilichangiwa na ujenzi uliofanyika katika sehemu isiyokuwa na udongo mzuri.

Amesema ukaguzi ulibaini nyufa za muundo katika hospitali ya Vitongoji kuanzia katika msingi wa jengo uliokusanywa kupitia kuta kuelekea katika ghorofa ya kwanza ya jengo. Pia nyufa za muunganiko ziliendelea na kuathiri zege ya ghorofa ya kwanza.

CAG ameshauri wizara kufanya tathmini ya uhimilivu wa udongo kwa kuwashirikisha wataalamu wa kijilojia kabla ya kuanza hatua za utekelezaji wa mradi, huku ikichukua hatua za haraka kukabiliana na dosari zilizobainika katika hosptali ya wilaya hiyo.

Amesema gharama za mradi ni zaidi ya gharama za awali za mikataba, hivyo kufanya kuwapo ongezeko la gharama ya ziada ya Sh18.5 bilioni. Hali hiyo ilitokana na kushindwa kuandaa vyema tathmini ya mahitaji.

Bodi ya zabuni amesema ilitakiwa kutoa dhamana kuhusu kazi inayokusudiwa kufanywa kwa kulinganisha na mahitaji ya mradi, lakini mpaka utekelezaji wa mradi unaanza, ilishindwa kutoa dhamana ya kazi iliyokusudiwa.

Ukaguzi umebaini mradi ulianzishwa na Wizara ya Afya bila kuhusisha idara ya watumiaji kwa ajli ya mapitio na wataalamu wa ujenzi, ili kuonyesha uhalisia wa ujenzi na uhalisia wa usanifu wa majengo yaliyopendekezwa.

Jambo hilo lilisababisha ongezeko la gharama kutokana na kazi za ziada na kazi za nje ambazo ni sawa na asilimia 26 ya bei ya mkataba wa awali.

Amesema hilo limesababisha kukosa uhakika wa fedha kutoka serikalini. Kwa mujibu wa maoni ya CAG, miradi ya baadaye wizara inaweza kukabiliwa na changamoto za kushindwa kukamilisha kazi, endapo Serikali itashindwa kuingiza fedha za ziada ambazo hazikuwapo katika mpango wa awali.

Kwa mujibu wa kanuni ya 142 (5) ya kanuni za ununuzi na uondoshaji wa mali za umma za mwaka 2020,  taasisi ya ununuzi na uondoshaji wa mali za umma haitaalika zabuni za kazi isipokuwa michoro na vipimo vikiwa vimekamilika na makadirio thabiti ya gharama yamendaliwa.

Hata hivyo, ukaguzi umebaini wizara ilifanya malipo ili kupata wataalamu kadhaa kwa ajili ya kuandaa, kusanifu michoro ya majengo na nyaraka za zabuni.

Wataalamu hao ni pamoja na wasanifu, mkadiriaji majengo, mhandisi wa muundo na huduma na mhandisi wa umeme kwa jumla ya Sh40 milioni.

Pamoja na hilo wizara ilipokea michoro na nyaraka za makadirio ya gharama (BoQ) ambazo hazikukamilika na kuwapo kwa upungufu ikiwemo kukosekana kwa baadhi ya michoro.

Hasara ya Sh527.7 milioni kutokana na kushindwa kuandaa vyema vipimo vya kiufundi kwa ajili ya uwekaji viluva katika maeneo ya ujenzi hospitali ni eneo lingine lililotajwa na CAG.

Ukaguzi umebaini vipimo havikuandaliwa kulingana na viwango vya uhandisi vinavyohitajika ambapo ni kinyume na kanuni ya 142 (5) ya kanuni za ununuzi na uondoshaji wa mali za umma mwaka 2020.

Kushindwa kuandaa vyema vipimo vya kiufundi kwa ajili ya uwekaji viluva katika maeneo ya ujenzi wa hospitali kumesababisha hasara ya Sh527.7 milioni.

Pia uchunguzi umebaini muundo wa majengo ya hospitali ulio chini ya viwango.

Viwango vya Wizara ya Afya (Vol 3, 2022) ya masuala ya ujenzi wa hospitali za wilaya, mikoa na vituo vya afya, vimeainisha ukubwa wa vyumba vinavyohitajika katika idara husika ya matibabu.

Hata hivyo, ukaguzi umebaini vyumba vilivyojengwa ni tofauti na vilivyokubalika kwa mujibu wa viwango vya wizara.

Ukaguzi umebaini ujenzi wa hospitali za wilaya za Vitongoji, Kinyasini, Dunga na Kitogani, haukutolewa kwa mzabuni aliyependekezwa na timu ya tathmini wala kuidhinishwa na bodi ya zabuni, hivyo kufanya ongezeko la Sh995.5 milioni.

Kwa mujibu wa kifungu cha 30.3 cha masharti maalumu ya mkataba kinamtaka mkandarasi kuwasilisha mpango kazi uliorekebishwa kwa kila mwezi na gharama za ucheleweshaji wa kuwasilisha kwa mapitio ya mpango kazi zitakuwa Sh1 milioni.

Hata hivyo, kifungu hicho cha mkataba hakikutekelezwa na makandarasi wote kulingana na masharti maalumu ya mkataba na mapitio ya mpango kazi.

Makandarasi wasiosajiliwa watumika

Ukaguzi huo umebaini kampuni mbili kati ya 11 zilihusika na wataalamu wa kigeni katika utekelezaji wa kazi zao, hata hivyo walibaini kuwapo watumishi 10 ambao hawakuwa na usajili na kibali cha ERB kulingana na mahitaji ya sheria.

Kati ya watu hao, watatu ni kutoka Hospitali ya Lumumba, sita hospitali ya wilaya ya Chumbuni na mmoja hospitali ya wilaya ya Kinyasini.

Alipotafutwa Waziri wa Afya, Ahmed Mazrui simu yake iliita bila kupokewa hata alipotumiwa ujumbe mfupi haukijibiwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh alieleza atafutwe wiki ijayo.

Related Posts