Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limewaomba radhi abiria waliosafiri kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam na treni ya kisasa (SGR) jana Alhamisi, Agosti 1, 2024 kutokana na hitilafu iliyojitokeza.
Taarifa ya TRC iliyotolewa leo Ijumaa, Agosti 2, 2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa shirika hilo, Jamila Mbarouk imesema kutokana na hitilafu hiyo treni hiyo ilichelewa kufika jijini Dar es Salaam.
“TRC linaomba radhi kwa abiria waliosafiri kutoka Dodoma saa 2:15 usiku kuelekea Dar es Salaam Agosti 1, 2024 kwa treni ya mwendo kasi kuchelewa kuwasili kutokana na hitilafu ya kiufundi iliyotokea eneo la mtaa wa Mshikamano, Kata ya Kihonda mkoani Morogoro.
Hitilafu za kiufundi zilitokea majira ya saa 4:33 usiku na kushughulikiwa kwa muda wa takribani saa moja na kusababisha treni hiyo ya abiria kutoka Dodoma kuchelewa kuwasili Dar es Salaam kwa wakati uliopangwa,” imeeleza taarifa hiyo na kuongeza:
“TRC inazingatia usalama wa abiria kabla na wakati wa safari ili kuepusha madhara kwa watumiaji wa huduma za usafiri wa reli na linaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza.”
Aidha, TRC imeeleza kuwa viongozi na wananchi wengine waliotoka Dodoma saa 1 usiku baada ya kushiriki sherehe za uzinduzi wa SGR uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan waliwasili Dar es Salaam kwa muda uliopangwa bila hitilafu yeyote.
Jana usiku, mitandao ya kijamii Mwananchi iliripoti tukio la treni hiyo kupata hitilafu na kusababisha adha kwa wasafiri.