SIMBA Day inayofanyika kesho itakuwa ni la 16, tangu tamasha hilo lianzishwe 2009, chini ya uongozi wa Hassan Dalali ‘Field Marshal’ na Mwina Kaduguda.
Katika msimu mpya wa Simba Day yenye kauli mbiu ya Ubaya Ubwela, Mwanaspoti, limefanya mahojiano na wazee na viongozi wa zamani wa klabu hiyo akiwemo Dalali na kikubwa zaidi wameupongeza uongozi kulisimamia tamasha hilo na sasa linazaa matunda makubwa.
Muasisi huyo anasema anajisikia faraja kuona tamasha hilo linafanyika kila mwaka ambapo linawaleta wana Simba pamoja ili kurudisha shukrani katika jamii na kutambulisha wachezaji wa msimu mpya.
“Kwa asilimia kubwa malengo ya tamasha hilo yanafanyika, ingawa ninachotamani kukiona ni kuona uwanja wa Bunju unamalizika na mechi zinachezwa pale, hilo ndilo ninalotamani kulishuhudia nikiwa hai.
“Ninachotarajia kwenye tamasha hilo ni kufurahia kuona Wanasimba tunakusanyika kwa pamoja na kuwatakia kila lakheri wachezaji wetu, kupigania ubingwa wa msimu ujao.”
Anasema kupitia tamasha hilo, wachezaji wapya wa Simba watatambua majukumu makubwa yaliopo mbele yao, kutokana na umati wa watu utakaofurika uwanjani.
“Wapenzi wa Simba kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania na nje, hao watawapa taswira wachezaji ama kuwaachia deni la kuhakikisha msimu ujao wanachukua ubingwa, kutokana na ukarimu ambao wataonyeshwa Simba Day,” anasema.
Kuhusiana na mechi ambayo Simba inatarajia kucheza dhidi ya APR ya Rwanda, anasema anatarajia kuona vipaji vikubwa kutoka kwa wachezaji ambao walikuwepo na wapya, kwani anaamini viongozi wamefanya kazi nzuri ya usajili.
“Simba imebadilisha kwa kiasi kikubwa kikosi chake, nilichopenda ni kuwasajili vijana ambao wana hamu ya mafanikio, hivyo naamini msimu unaokuja utakuwa wa kicheko kwetu,” anasema.
Abdallah Kibadeni, ambaye ni mchezaji na kocha wa zamani wa timu hiyo, anasema anatamani katika tamasha hilo wazee waliotumia muda mwingi kwa ajili ya kuitumikia klabu wathaminiwe.
“Kuna wazee wengi ambao waliitumikia Simba kwa nyanja mbalimbali. Hao watambuliwe katika tamasha hilo. Wapo wengi mfano ni kama Dalali, Kaduguda, nipo mimi na wengine wengi, ili kuonyesha vizazi vilivyo kwamba wanahitaji kuwa wazalendo kwa klabu yao,” anasema.
Ally Pazi Samatta ambaye ni mchezaji wa zamani na Simba anasema anatarajia kuona vitu vingi katika tamasha hilo pia anashauri uongozi ufanye kitu kwa Dalali.
“Dalali na Kaduguda ndio waanzilishi wa tamasha hilo, linalowapa raha mashabiki wa Simba, kama haitoshi Yanga imeiga kutoka Simba nayo inafanya vizuri, hilo litoshe kwa viongozi wa Simba kuwaza kufanya kitu kwa watu hao, ikiwezekana serikali iwaone maana wameleta furaha kwa Watanzania,” anasema.