Serikali yaridhishwa na ziada ya chakula mikoa ya Nyanda za Juu

Mbeya/Dodoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema Serikali imeridhishwa na ziada ya chakula tani 10.5 milioni za uzalishaji wa mazao ya kimkakati katika mikoa ya nyanda za juu kusini.

Mbali na hayo, Dk Biteko ameziagiza wizara zote kushiriki kikamilifu katika maonesho ya wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea maeneo mbalimbali nchini.

Dk Biteko amesema hayo leo Ijumaa Agosti 2, 2024 wakati wa uzinduzi wa maonesho ya wakulima ‘Nane Nane’ katika viwanja vya John Mwakangale jijini Dar es Salaam.

Amesema kwa kanda ya nyanda za juu kusini mahitaji chakula ni tani 3.1 milioni huku kwa msimu huu kuna ongezeko la asilimia 15 na kufikia tani 13.6, huku akibainisha  sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi vimekuwa na mchango mkubwa kwa Taifa.

“Naomba niwaelekeze NFRA (Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula) kuhakikisha bei ya mahindi inakuwa Sh,700 kwa kilo, lakini maeneo ya taasisi za utafiti yalindwe kwa wivu mkubwa kwani baadhi yao yamevamiwa na wananchi” amesema Biteko.

Mwezi uliopita, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa ziarani mikoa ya Rukwa na Katavi, alitoa maelekezo ya mahindi kununuliwa kwa wakulima kwa kilo Sh700. Ni baada ya kupokea kero kutoka kwa wananchi wakiomba ipande.

Biteko amezitaka pia wizara zote kushiriki vyema maonesho hayo na kutumia wataalamu walionao na kuwataka kuzingatia matumizi salama na bora katika viuatilifu na kemikali.

“Serikali itaendelea kuwezesha mbolea ya ruzuku na mbegu bora, lakini wizara zote lazima ziwe na wawakilishi katika maonesho haya, kilimo, mifugo na uvuvi imekuwa na mchango mkubwa ikiwamo ajira kwa vijana,” amesema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema Serikali ya awamu ya sita imendelea kuwekeza katika miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya kilimo.

“Tunaona namna Serikali inavyofanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu, afya sambamba na ujio wa ujenzi wa soko la kisasa na kituo kikuu cha mabasi ya mikoani na miundombinu ya barabara.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewataka wakulima na wafugaji kutumia fursa za maonyesho ya wakulima nanenane kama njia pekee kuongeza tija uzalishaji.

“Wakulima changamkieni fursa ya maonyesho Serikali iko kwenye mchakato wa kuboresha na kujenga uwanja wa kisasa wa maonyesho ya nanenane mikoa ya Nyanda za juu kusini, ‘’ amesema.

Mkulima wa mboga mboga kutoka Kilolo mkoani Iringa, Josephina Sanga amesema uwepo wa maonyesho hayo ni fursa pekee kwao kujifunza fursa za uzalishaji mazao ya kimkakati.

Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amesema idadi ya mifugo nchini imeongezeka kutokana na usimamizi mzuri unaofanywa na sekta ya mifugo na uzalishaji wa mazao ya mifugo kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Mnyeti ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Agosti 2, 2024 kwenye maonyesho ya wakulima nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Amesema hadi kufikia mwaka 2023/2024 Tanzania ilikuwa na jumla ya ng’ombe milioni 37.9, mbuzi milioni 27.6, kondoo milioni 9.4, nguruwe milioni 3.9 na kuku milioni 103.1 ambapo kuku wa asili ni milioni 47.4 na kuku wa kisasa milioni 55.7.

Naibu waziri huyo amesema ongezeko hilo ni tofauti na ilivyokuwa mwaka 2022/23 ambapo kulikuwa na ng’ombe 36.6, mbuzi milioni 26.6, kondoo milioni 9.1, nguruwe milioni 2.9. na kuku milioni 97.9.

Pia mesema sekta ya uvuvi inaendelea kuwa muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa kwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 198,475 na wakuzaji viumbe maji 34,057 na takriban Watanzania milioni sita wanajihusisha na shughuli mbalimbali zinazohusiana na uvuvi katika mnyororo wa thamani.

“Katika mwaka 2023/2024 Serikali ilitoa jumla ya Sh60 bilioni kutekeleza mradi wa kuwapatia wavuvi mkopo wa masharti nafuu kwa ajili ya ununuzi wa boti za kisasa za uvuvi na zana zake, ufugaji samaki kwenye vizimba na uzalishaji wa zao la mwani ambao unasimamiwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB),” amesema Mnyeti

Aidha amesema wizara hiyo kwa kushirikiana na sekta binafsi, inaendelea kutekeleza programu ya utoaji wa mafunzo atamizi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji kwa vijana nchini ambayo inatarajiwa kuwezesha vijana kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri.

“Katika mwaka 2022/2023 jumla ya vijana 200 wamepatiwa mafunzo hayo na mpango wa Serikali ni kuendelea kutoa mafunzo kwa vijana 750. Nitoe wito kwa vijana kuchangamkia fursa hiyo itakayowawezesha kiuchumi,” amesema.

Amesema katika maonyesho hayo kutakuwa na mashindano ya mifugo ambayo yana lengo la kuwahakikishia wafugaji kuwa matumizi ya teknolojia ya ufugaji yanawezekana katika mazingira ya kufuga kwenye maeneo anayoishi na kushawishi matumizi ya teknolojia ya ufugaji bora.

Mnyeti amesema maonesho hayo  huwezesha wafugaji kujenga imani kwa wataalamu wa ugani kwa kuwahakikishia kuwa ushauri wao ni wa thamani na wenye tija pia, husaidia kujenga imani kwa wafugaji kuhusiana na matumizi sahihi ya teknolojia za ufugaji bora zinazotolewa na watafiti hapa nchini na kuwafundisha kutumia mbinu hizo kuboresha ufugaji wao.

Kwa upande wake,  mkurugenzi TADB Japhet Justine amesema hadi kufikia Aprili mwaka 2024, benki  imetoa mkopo wa Sh 15.82 bilioni ambapo mikopo hiyo ilielekezwa kwenye maeneo ya ufugaji wa ngómbe, kuku na nguruwe; uzalishaji wa malisho na vyakula vya mifugo; unenepeshaji wa mifugo na uchakataji wa mazao ya mifugo.

Katika hatua nyingine, ili kuwaepusha wakulima na mikopo umiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekuja na kampeni ya kutoa elimu ya kujiepusha na mikopo hiyo, ambayo huwa inawarudisha nyuma wakulima badala ya kuwaletea maendeleo.

Hayo yamesemwa na ofisa wa Idara ya Usimamizi wa Huduma ndogo za fedha (BoT), Deogratius Mnyamani, akizungumza na Mwananchi kwenye maonyesho ya Nanenane jijini Dodoma.

Mnyamani amesema wakulima ni waathirika wa mikopo umiza inayotolewa na watu ambao hawana leseni za kutoa huduma za kifedha na hivyo kujikuta fedha zao zote zinachukuliwa na hao watu.

“Kuna watu wanatoa mikopo na kutoza riba hadi asilimia 50 kwa mwezi hii haiwezekani kwa sababu hakuna biashara itakayokuingizia kipato kikubwa namna hiyo kwa mwezi na bado biashara yako iendelee kusimama na ndiyo maana tupo hapa kutoa elimu ya mikopo salama kwa wakulima,” amesema Mnyamani.

“Tunajua ili kilimo, mifugo na uvuvi viende mbele inahitajika mikopo lakini tunawashauri wakakope kwenye taasisi zilizosajiliwa na Benki Kuu badala ya kukopa kwa watu ambao hawajasajiliwa na mwisho wake wanafilisika.”

Amesema hivi karibuni BoT itakuja na kampeni maalum ya kuwaelisha watu kujiepusha na mikopo umiza itakayojulikana kama ‘zinduka, usiumizwe kopa kwa maendeleo’ kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania kukopa kwa malengo.

Imeandikwa na Saddam Sadick, Hawa Mathias (Mbeya) na Rachel Chibwete (Dodoma)

Related Posts