UWT WATAKIWA KUMFIKIA KILA MTU, KUONGEZA ‘JESHI LA MAMA’

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amewataka Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Jumuiya ya CCM, kuendelea kuwa sauti ya wanawake nchini na kuwahamasisha kushiriki siasa, akiwataka wahakikishe wanawafikia watu wote, kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.

Katika kutimiza jukumu hilo, Balozi Nchimbi amewahimiza UWT kuendelea kuwatembelea wananchi nchi nzima, kama wanavyofanya sasa, kupitia ziara zao, ambazo pia amewaambia waendelee kuzitumia kuyatangaza mafanikio makubwa yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na Serikali ya CCM, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Balozi Nchimbi amesema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya afya ya uzazi, mama na mtoto kwa Wajumbe wa Baraza Kuu la UWT, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Dodoma, leo Ijumaa, Agosti 2, 2024,

“Hongereni sana kwa kazi kubwa na nzuri mnayoendelea kuifanya ya kuimarisha Jumuiya. Tumeona amsha amsha yenu mnayofanya kila kona. Hongereni sana pia kwa kuendelea kusajili wanachama wengi. Tunataka muendelee hivyo hivyo kwa vitendo ili muongoze. Na sasa tunaelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, msiache ziara za kukutana na wananchi.

“Kwenye CCM wanawake ni jeshi la kutegemewa. UWT hakikisheni watu wote wanafikiwa. Mnao wajibu mkubwa kwa Jumuiya yenu, kwa Chama Cha Mapinduzi na Mwenyekiti wa CCM. Kazi ya kuhamasisha maendeleo na kutangaza mafanikio makubwa kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya CCM, chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mkaifanye bila kumuonea haya mtu yeyote,” amesema Balozi Nchimbi.

Naye Mwenyekiti wa UWT Taifa, Ndugu Mary Pius Chatanda, akimkaribisha kuzungumza, ameushukuru uongozi wa Chama kwa jinsi unavyoendelea kuwaamini UWT, na kumuomba Katibu Mkuu Balozi Nchimbi afikishe salaam kwa Mwenyekiti wa CCM kuwa jumuiya hiyo itaendelea kufanya kazi kubwa kwa ajili ya CCM na nchi kwa ujumla, ikiwemo kuendelea kuwahamasisha wanawake kushiriki shughuli za kisiasa nchini.






Related Posts