Tanzania yajipanga kudhibiti homa ya nyani, dalili zake hizi hapa

Dar es Salaam. Wizara ya Afya imesema imejipanga kuudhibiti ugonjwa wa homa ya nyani (Mpox) endapo utaingia nchini.

Kauli ya wizara inatokana na taarifa zinazoeleza ugonjwa huo upo kusini mashariki mwa nchi jirani ya Kenya.

Akizungumza na Mwananchi, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya, Englibert Kayombo amesema wamepokea taarifa za ugonjwa huo kufika Kenya japo hakuna taarifa zozote mpaka sasa za ugonjwa kufika Tanzania.

“Tumepokea taarifa za ugonjwa huo kufika nchi jirani lakini mifumo yetu iko imara kupigana na ugonjwa huo,” amesema.

Kayombo amesema taarifa za kitaalamu kuhusu ugonjwa huo zitatolewa hivi karibuni na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu.

Machi 29, 2023 kuliripotiwa kuibuka ugonjwa wa Marburg katika kata za Maruku na Kanyangereko wilayani Bukoba mkoani Kagera ambao watu sita walipoteza maisha.

Kubainika kwa ugonjwa huo kutoka kwa wanyama kulitokana na uchunguzi wa kitabibu baada ya vifo vya watu hao vilivyotokea Machi 16, 2023 vikidaiwa kusababishwa na ugonjwa usiojulikana.

Kutokana na vifo hivyo, Serikali ilichukua hatua kadhaa ikiwemo kutenga eneo maalumu la wagonjwa na wote waliochangamana nao kwa lengo la kuepuka maambukizi. Zaidi ya watu 200 waliwekwa karatini.

Taarifa za uwepo wa homa ya nyani nchini Kenya zimeripotiwa baada ya vimelea vya ugonjwa huo kugunduliwa kwa mtu aliyekuwa akisafiri kutoka Uganda hadi Rwanda kupitia Kenya.

Wizara ya Afya nchini Kenya imesema msongamano mkubwa wa watu kati ya Taifa hilo na mengine ya Afrika Mashariki unaleta hatari kubwa ya kuenea kwa ugonjwa huo katika eneo hilo.

Maambukizi mengine ya ugonjwa huo pia yameripotiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mpox au monkeypox ni ugonjwa wa virusi unaosababishwa na virusi vya monkeypox, ambavyo ni jamii ya familia ya virusi vya orthopox vinavyojumuisha virusi vinavyosababisha ndui.

Ingawa ugonjwa huo unafanana na ndui, inaelezwa madhara yake ni madogo na maambukizi siyo makubwa sana.

Kwa mujibu wa wataalamu, dalili za ugonjwa huo zinaweza kuonekana kati ya siku tano hadi 21 baada ya kuambukizwa.

Dalili za awali zinaelezwa kuwa ni homa, kichwa kuuma, maumivu ya misuli, uchovu, na kuvimba kwa tezi za limfu.

Wataalamu wanasema baada ya dalili za awali, vipele vinavyojaa majimaji au usaha huanza kujitokeza, mara nyingi huanzia usoni na kisha kusambaa kwenye sehemu nyingine za mwili. Vipele hivyo hukauka na kuwa makovu.

Inaelezwa ugonjwa huo huambukizwa zaidi katika nchi za Afrika ya Kati na Magharibi karibu na misitu ya kitropiki.

Wataalamu wa afya wanaeleza ugonjwa huo huenezwa kwa kugusa ngozi iliyo na jeraha au michubuko, njia ya upumuaji, njia ya macho, pua au mdomo.

Pia kwa kugusana na wanyama kama vile nyani na panya na kushiriki matandiko au mavazi na mgonjwa.

Taarifa kutoka mitandao zinaeleza virusi hivyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini DR Congo mwaka 1970 kwa tumbili aliyekuwa akifungwa na binadamu na baada ya hapo uliripotiwa katika nchi 10 za Afrika.

Kwa mara ya kwanza nje ya Bara la Afrika ugonjwa huo uliripotiwa mwaka 2003 katika Majimbo sita ya Marekani ya Illinois, Indiana, Kansas, Missouri, Ohio, na Wisconsin.

Walioripotiwa kuugua ugonjwa huo ni wale walioishi jirani na wanyama.

Mwaka 2017, Nigeria iliripotiwa kukubwa na mlipuko mkubwa zaidi wa ugonjwa huo kuwahi kurekodiwa kwa takribani miaka 40 iliyopita.

Wataalamu wa afya wanasema ugonjwa huo haujapata tiba ila unaweza kudhibitiwa kwa kuzuia maambukizi kwa njia ya chanjo.

Dalili ni pamoja na upele wa ngozi, vidonda mdomoni na sehemu za siri.

Kawaida hutibika bila matatizo ndani ya wiki mbili hadi nne.

Hatahivo maambukizi sugu yanahitaji matibabu maalum.

Wakenya wametakiwa kufuata masharti ya kiafya katika maeneo ya umma ili kujilinda binafsi, familia zao na jamii kutokana na kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.

Waoshe mikono kwa sabuni na maji mara kwa mara

Walio na dalili wametakiwa kufuata ushuari wa kiafya na kuzuia kushikana na watu wengine ili kuzuia maambukizi kabla ya kwenda katika kituo cha afya kilicho karibu

Kuzuia kushikana kimwili na mtu anayeshukiwa kuwa na maradhi hayo

Related Posts