Akutwa amefariki kwenye kisima cha maji Mbozi

Songwe. Kijana aliyefahamika kwa jina la Daniel Siyame (23) mkazi wa Mtaa wa Ilolo wilayani Mbozi amekutwa amefariki dunia kwenye kisima cha maji.

Tukio hilo limebainishwa leo Agosti 2, 2024, majira ya asubuhi na mtoto wa mmiliki wa kisima hicho, Samweli Kisanga, wakati wa kuchota maji, aliposhtuliwa na harufu kali kwenye maji.

Kisanga amesema kisima hicho kinatumiwa na familia yao na majirani, na usiku wa kuamkia leo walichota maji bila kubaini dosari yoyote. Hata hivyo, leo asubuhi ndipo walipokutana na tukio hilo.

“Baada ya kutoa ndoo iliyokuwa kwenye kisima, nikaona ni tukio ambalo si la kuhangaikia pekee yangu. Nimetoa taarifa kwa majirani na kwa viongozi baada ya kuona kitu cheusi kwenye kisima,” amesema Kisanga.

Shuhuda wa tukio hilo, Grace Salamba, amelishukuru Jeshi la Zimamoto kwa kufika eneo la tukio na kuopoa mwili huo.

“Tunachoomba serikali za mtaa zihakikishe zinatoa miongozo ya kila mwenye kisima akifunike ili kuepusha matukio kama haya, na tunaliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa matukio kama haya ambayo yameanza kuwa tishio,” amesema Salamba.

Yutasi Mnkondya, mwenyekiti wa mtaa wa Ilolo Shuleni, amesema alipigiwa simu na mjumbe Kaselema Kibona kuhusu tukio hilo, naye akatoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Polisi ambao walifika na kuopoa mwili wa marehemu.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Songwe, Joseph Kapange, amesema wamepokea taarifa ya wito kutoka Jeshi la Polisi ambao walifika eneo la tukio na kufanikiwa kuuopoa mwili huo.

Paulo Siame, baba mzazi wa kijana huyo mkazi wa kitongoji cha Ilembo kitovu B, amesema mtoto wake alipotea tangu Julai 28 mwaka huu akiwa na tatizo la kuchanganyikiwa na alikuwa anamwambia mama yake kuna watu wanataka kumuua, hali iliyopelekea kupotea nyumbani.

“Nimepokea kwa masikitiko kifo cha mwanangu ambaye amekutwa ndani ya kisima cha maji na hatujui amekufaje. Hivyo tunaliachia Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi, ukweli utabainika chanzo cha kifo chake,” amesema Siame.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 2, 2024, Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Augustino Senga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba marehemu amekutwa amefariki ndani ya kisima ambacho kifuniko chake kimeondolewa.

Kamanda Senga amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini nini kimesababisha tukio hilo.

Related Posts