Aliyejinadi Profesa wa Muhimbili na wenzake watatu wasomewa mashtaka 50

Dar es Salaam. Mkazi wa Kitunda, Ibrahim Bigirwa na wenzake wawili wamefishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 50 yakiwamo ya kuongoza genge la uhalifu, kutakatisha fedha na kujipatia Sh7.3 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Mbali ya makosa hayo, Bigirwa (33) pia anakabiliwa na mashtaka ya kujitambulisha kwa watu kuwa yeye ni Profesa Kamugisha, daktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kujipatia fedha akidai atawasambazia vifaatiba, akijua kuwa ni uongo.

Washtakiwa wengine ni Marick Kalimbe (35), mfanyabiashara na mkazi wa Kagera, na Godfrey Fabian (46), mkazi wa Kasindi- Kashai mkoani Kagera.

Washtakiwa wamefikishwa mahakamani leo Agosti 2, 2024 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Rhoda Mwakanyamale mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi.

Kati ya mashtaka 50 yanayowakabili washtakiwa, 35 ni ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, 10 kutumia laini iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, matatu ni ya kujitambulisha isivyo halali, na moja la kuongoza genge la uhalifu na kutakatisha fedha.

Kabla ya washtakiwa kusomewa mashtaka, hakimu Mushi amewaeleza hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. Pia shtaka la kutakatisha fedha halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Wakili Mwakanyamale katika shtaka la kwanza alidai kwa pamoja washtakiwa wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu, kosa wanalodaiwa kulitenda kati ya Februari mosi, 2024 na Juni 30, 2024 katika maeneo yasiyojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wanadaiwa kuanzisha mtandao wa uhalifu wa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (sms) wenye kushawishi watu na kujipatia Sh7.3 milioni.

Shtaka la pili linamkabili Bigirwa akidaiwa kujitambulisha kwa Segorina Mdegela kuwa yeye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) akijua ni uongo. Anadaiwa kutenda kosa hilo Februari 20, 2024.

Shtaka la tatu pia linamkabili Bigirwa akidaiwa kujitambulisha kwa Bindiya Sweety Aubroo kuwa yeye ni msaidizi wa Profesa Kamugisha ambaye ni daktari kutoka MNH akijua ni uongo. Anadaiwa kutenda kosa hilo Machi 2, 2024.

Katika shtaka la nne, Bigirwa anadaiwa Aprili 3, 2024 alijitambulisha kwa Joseph Masanja kuwa yeye ni Profesa Kamugisha kutoka MNH akijua kuwa ni uongo.

Shtaka la tano hadi 13 ni kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine bila kuwa na ruhusa ya mtoa huduma yanayomkabili Bigirwa na Kalimbe. Wanadaiwa kuyatenda kati ya Juni 22, na Juni 24, 2024.

Wanadaiwa kutumia namba za simu zilizosajiliwa kwa majina ya Wales Kinkande, Tofulo Swai, Gaitan Mlongamile, Neema Majid na Hakimu Musa bila kuwa na ruhusa ya mtoa huduma.

Shtaka la 14 hadi 49 ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, linalomkabili Bigirwa pekee, akidaiwa kujipatia fedha kutoka kwa watu mbalimbali akiahidi kuwasambazia vifaatiba, kicho ambacho ni uongo.

Bigirwa anadaiwa Februari 20, 2024 aliipata Sh188,000 kutoka akaunti ya benki ya CRDB inayomilikiwa na Segorina Mdegela.

Pia anadaiwa kujipatia Sh380,000 kutoka akaunti ya benki ya NMB iliyomilikiwa na Joseph Masanja, Sh670,000 kutoka kwa  Masanja, Sh315,000 kutoka kwa Jackline Rugashila, Sh300,000 kutoka kwa Gasaya Mekeya, Sh98,000 kutoka kwa Bibian Komba, Sh142,000 kutoka kwa Flavia Muniga, Sh85,000 kutoka kwa Wdita Abel.

Anadaiwa kujipatia Sh1 milioni kutoka kwa Prima Maheshi, Sh24,000 kutoka kwa Sauli Mohamed, Sh300,000 kutoka Gasaya Mekeya, Sh275,000 kutoka kwa Njelika Mwigira.

Bigirwa anadaiwa kujipatia Sh273,000 kutoka kwa Hawa Kamwela, Sh88,000 kutoka kwa Amon Henry, Sh88,000 kutoka kwa Ester Ndingu, Sh122,000 kutoka kwa Kelvin Shirima akidai atawasambazia vifaatiba.

Shtaka la 50 ni la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa wote, wanaodaiwa kati ya Februari mosi, 2024 na Juni 30, 2024 walijipatia Sh7,345,000 ambazo ni mazalia ya mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika. Hakimu Mushi aliahirsha kesi hiyo hadi Agosti 12, 2024 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Related Posts