Mwabukusi rais mpya TLS, yaliyombeba haya hapa

Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimemtangaza Boniface Mwabukusi kuwa rais wa chama hicho, huku misimamo na ujasiri wake vikitajwa kuwa miongoni mwa turufu zilizompa ushindi.

Mwabukusi ametangazwa mshindi wa kiti hicho kwa kupata kura 1,274 ambazo ni sawa na asilimia 57.4 dhidi ya washindani wake Sweetbert Nkuba, Revocutus Kuuli, Ibrahim Bendera, Paul Kaunda na Emmanuel Muga katika uchaguzi ambao kwa mara ya kwanza umefanyika nje ya Jiji la Arusha.

Kinyang’anyiro cha uchaguzi huo kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma, kililenga kumpata mrithi wa Harold Sungusia aliyemaliza muda wake.

Matokeo ya uchaguzi huo yalitarajiwa kutangazwa saa 11 jioni, lakini yametangazwa saa 5. 15 usiku.

Matokeo yamechelewa kutangazwa tofauti na ilivyotarajiwa, kutokana na msiba wa mmoja wa wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, Maria Pengo na kusogezwa muda kutokana na karatasi za kura kupungua.

Safari ya Mwabukusi katika kinyang’anyiro hicho ilikumbwa na misukosuko, siku moja kabla ya kuanza kwa kampeni za urais, kamati ya rufaa ya TLS ilimwengua kuwania nafasi hiyo, akiwa ameshapitishwa na Kamati ya Uchaguzi.

Kilichotajwa kama sababu ya kuenguliwa kwake kupitia rufaa ya mmoja wa ma wakili ni ‘doa la kimaadili’ lililodaiwa kwenda kinyume cha kanuni za uchaguzi huo.

Mwabukusi Julai 11, 2024 aliwasilisha Mahakama Kuu maombi ya kufungua shauri la marejeo ya uamuzi uliomwengua kwenye orodha ya wagombea urais wa TLS, akiungwa mkono na mawakili wenzake kadhaa ambao walihudhuria mahakamani, mbali na 29 waliomwakilisha mbele ya jaji. Julai 26, mahakama hiyo ilibatilisha uamuzi uliomwengua kuwa mgombea.

Mwabukusi amejipambanua kuwa wakili wenye msimamo na kupigania haki na masilahi ya wananchi kupitia majukwaa mbalimbali aliyowahi kushiriki, ikiwemo mikutano ya hadhara.

Amejizolea sifa katika sakata la kupinga mkataba wa uwekezaji na uendelezaji bandari kwa kampuni ya Dubai World (DP-World), akidai hauna masilahi kwa umma, lakini Serikali ilisema mchakato huo una faida kubwa kwa Taifa.

Mbali na hilo, katika utekelezaji wa majukumu yake, Mwabukusi amekuwa akikumbana na misukosuko na changamoto, ikiwemo kuitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya Mawakili kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Agosti mosi, 2024, Mwabukusi alisema ukimwondoa mgombea mwenzake Kuuli, washindani wengine waliobaki ni lazima wangekuwepo katika kinyanya’nyiro hicho, ndiyo maana walijikita katika kusifu ilani na ajenda za hao wawili.

“Ilani nyingi tumeziona zenye sura za kupendeza na kuvutia, lakini kwa miaka 70 hazijawahi kutupa majibu ya changamoto zinazotukabili, tunailaumu Serikali kwa sababu moja tu, tumeacha kazi ya msingi ambayo kifungu cha nne (cha sheria ya mawakili), badala yake -tuna-dili- na mambo yasiyo ya muhimu sana.

Kifungu cha nne kinachozungumzwa na Mwabukusi ni cha sheria ya kuanzishwa kwa TLS kinachokipa jukumu chama hicho la kuishauri Serikali.

“Kwa hiyo Serikali ikitutafuta hatuonekani, kwa sababu imetupa sheria inayowezesha kuonekana na ukiwa na masuala yapi, yenye uzito upi na kwa utaratibu gani. Lakini sisi tunapiga sarakasi tukiwa na taulo kiunoni,” alisema Mwabukusi akishangiliwa na mawakili.

Mwabukusi alisema TLS inahitaji kiongozi atakayerudisha wanachama wa taasisi hiyo katika misingi yao na si mwingine, bali ni yeye, akiwaomba wajumbe wa chama hicho kumpigia kura kwa wingi.

“Kukosekana uhalisia na uwajibikaji, ndiyo maana tunaona huku tuna vyama vingi vya uanasheria, tunahitaji chama kimoja chenye nguvu na jumuishi. Kutokana na hili ndiyo maana Serikali inaingilia taaluma yetu kwa sababu tumekuwa kama ng’ombe aliyekatwa kichwa, amechoka na kuingia sokoni,” alisema Mwabukusi.

Mwabukusi aliwaomba wajumbe wa TLS kumchagua awe na rais wa taasisi hiyo, ili atekeleze majukumu yake kwa misingi ya kifungu cha nne.

Kwa upande wake Nkuba, alisema yeye ni muumini wa umoja na mshikamano, akisema miongoni mwa mambo atakayoyasimamia ni kifungu cha nne, masilahi ya kiuchumi ya ma wakili, ikiwemo ulipaji wa ada kwa awamu, bima ya afya, pamoja na kuwasaidia mawakili vijana katika malezi kwa kuwatengenezea kituo cha malezi.

“Kuimarisha uhusiano na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, ambayo tutaishinikiza na kujadiliana ihakikishe katika mikataba yote ya uwekezaji inakuwa na kipengele cha lazima cha huduma za kisheria kwa ‘local content’ ili kulinda kazi za mawakili.

“Nitahakikisha mawakili wanaheshimiwa katika utekelezaji wa majukumu yao, katika uongozi wangu hakutakuwa na vitisho vya aina yoyote kwa mawakili dhidi Polisi au chombo chochote. Pia heshima yetu itatawala katika viunga vya mahakama zetu, tutajenga uhusiano bora,” alisema Nkuba.

Mwabukusi ataongoza TLS kwa miaka mitatu badala ya mmoja wa awali, kutokana na mabadiliko ya sheria yaliyofanyika.

Related Posts