LONDON, ENGLAND: DIRISHA la usajili wa mastaa huko Ulaya bado halijafungwa na klabu mbalimbali bado zipo bize kwenye kuhakikisha zinanasa saini za wachezaji wapya ili kwenda kuboresha vikosi vyao.
Tayari kuna timu zimepata wachezaji zilizokuwa zikiwahitaji ili kwenda kufanya vikosi vyao kuwa imara zaidi, huku timu nyingine zikiwa bado sokoni kusaka mastaa ambao zinaamini zikiwapata zitakuwa zimemaliza matatizo, mfano Chelsea ilivyo kwenye mchakamchaka wa kufukuzia huduma ya straika wa Napoli, Victor Osimhen.
Hata hivyo, kila mchezaji ana bei yake sokoni kwa mujibu wa Transfermarkt, hivyo kama utalipa zaidi ya pesa hiyo iliyotajwa kuwa ndiyo thamani halisi ya mchezaji husika sokoni, basi wajanja wamekupiga.
Na mara nyingi timu zimekuwa zikiuziwa wachezaji kwa pesa nyingi tofauti na thamani zao sokoni kutokana na presha ya timu zinazowataka, zipo tayari kufanya chochote kunasa huduma zao. Lakini, Transfermarkt inaweka wazi bei halali za mastraika hawa sokoni, ukilipa zaidi ya hapo, basi umeamua upigwe tu mkwanja wako.
10. Gabriel Jesus – Euro 65 milioni
Fowadi huyo wa Kibrazili amekuwa akiibua maswali mengi juu ya ubora wake wa uwanjani, akiwa amefunga mabao 19 na kucheza mechi 69 tu tangu alipojiunga na Arsenal mwaka 2022. Kinachombeba Jesus ni kwamba hayupo kwenye ubora mkubwa katika kazi yake ya msingi ambayo ni kutikisa nyavu, lakini amekuwa kwenye kiwango bora sana katika maeneo mengine na kuhesabika kama mchezaji wa timu. Bei yake ni Euro 65 milioni.
9. Rasmus Hojlund – Euro 65 milioni
Manchester United ililipa Pauni 64 milioni kunasa saini ya straika Hojlund kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, akitokea Atalanta, huku thamani yake hiyo inaweza kupanda hadi Pauni 72 milioni. Kwa hali ya soko la Hujlund ilivyo kwa sasa, inaelezwa kwamba bei anayopaswa kuuzwa ni Euro 65 milioni, hivyo kama Man United itaendelea kulipa pesa nyingine zilizobaki ili kufikia Pauni 72 milioni, itakuwa imepigwa.
8. Darwin Nunez – Euro 70 milioni
Straika, Darwin Nunez bado hajajipata tangu alipotua kwenye kikosi cha Liverpool, ambapo kiwango chake cha uwanjani kimekuwa cha kupanda na kushuka kama homa za vipindi. Hata hivyo, fowadi huyo bado alifunga mabao 33 na kuasisti mara 17 kwenye kikosi cha Liverpool, hivyo kumpa matumaini makubwa kocha mpya wa timu hiyo, Arne Slot kufanya kweli msimu huu. Bei yake inayotajwa sokoni kwa sasa ni Euro 70 milioni.
7. Alexander Isak – Euro 75 milioni
Kiwango chake kimekuwa matata sana tangu alipojiunga na Newcastle United mwaka 2022. Straika, Alexander Isak, wakati anatua St James’ Park, miamba hiyo ya Ligi Kuu England ililipa Pauni 60 milioni kunasa huduma yake. Lakini, baada ya kuonyesha kiwango kikubwa sana ndani ya uwanja, straika huyo mwenye umri wa miaka 24, thamani yake sokoni imekwenda juu na kwamba kwa sasa hivi, ukimtaka lipa Euro 75 milioni.
6. Julian Alvarez – Euro 90 milioni
Julian Alvarez alionyesha kiwango bora sana kwenye kikosi cha Manchester City mwaka 2022, ambapo kabla ya hapo, saini yake ilikuwa ikiwashindanisha miamba hiyo ya Etihad na mahasimu wao wakuu kwenye Ligi Kuu England, Manchester United. Alinaswa kwa pesa ndogo sana, Pauni 14 milioni na baada ya kuonyesha kiwango bora huko Man City na timu ya Argentina, thamani yake imepanda, bei yake Euro 90 milioni.
5. Harry Kane – Euro 100 milioni
Ndani ya uwanja straika Harry Kane amekuwa akifanya mambo yake kwa ufanisi mkubwa, akifunga mabao ya kutosha katika kuisaidia timu yake. Lakini, umri wake wa miaka 31 na kitendo cha kupata majeraha ya mara kwa mara kwa siku za hivi karibuni vimefanya thamani ya straika huyo sokoni kushuka. Hata hivyo, bado yupo juu, bei yake halisi ni Euro 100 milioni kama kiasi ambacho Bayern Munich ililipa kunasa saini yake.
4. Victor Osimhen – Euro 100 milioni
Napoli ilishindwa kutetea taji la Serie A msimu uliopita, ambapo miamba hiyo ilimaliza nafasi ya 10, pointi 41 nyuma ya mabingwa wa msimu wa 2023-24, Inter Milan. Lakini, hilo halimfanyi Osimhen kushuka thamani yake sokoni, kwani straika huyo bado anatazamwa kama mmoja wa wachezaji hatari sana mbele ya goli, ambapo kwa msimu uliopita alifunga mabao 17 na asisti nne katika mechi 32. Bei yake ni Euro 100 milioni.
3. Lautaro Martinez – Euro 110 milioni
Imekuwa muda mrefu, lakini kwa sasa straika Lautaro Martinez ameanza kupata maua yake kutokana na kuwa matata kabisa mbele ya goli kwa kile anachofanya kwenye kikosi chake cha Inter Milan. Muargentina huyo anaingia msimu wa 2024-25 akiwa amefunga mabao 103 katika mechi 206 alizocheza kwenye Serie A, huku huduma yake ikiwa na uhakika wa kufunga mabao 25+ kwa msimu. Sokoni bei yake inasema ni Euro 110 milioni.
2. Kylian Mbappe – Euro 180 milioni
Kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, Kylian Mbappe alikamilisha uhamisho wake wa kwenda kujiunga na Real Madrid akitokea Paris Saint-Germain kwa uhamisho wa bure kabisa. Lakini, bei yake sokoni inatajwa kuwa ni Euro 180 milioni, kwamba ukilipa kiwango hicho cha pesa, hujapigwa, ndiyo bei yake. Mashabiki wa soka kwa sasa wanasubiri kuona ni kitu gani Mbappe atafanya baada ya kutua Los Blancos.
1. Erling Haaland – Euro 180 milioni
Kwenye ishu ya bei zao sokoni, hakuna kinachowatofautisha Erling Haaland na Mbappe kwa sasa, kutokana na kuelezwa wote thamani yao ni Euro 180 milioni. Wakati Haaland akitamba kwenye soka la ngazi ya klabu, akibeba mataji makubwa, ikiwamo Ligi ya Mabingwa Ulaya na Klabu Bingwa Dunia, Mbappe amekuwa moto kwenye soka la kimataifa, akibeba Kombe la Dunia. Haaland anahudumu Man City na bei yake ni hiyo.