VITA ya mashindano ya Olimpiki kusaka medali ya dhahabu ya mchezo wa kikapu jijini Paris, Ufaransa inaendelea kuwa moto upande wa makundi, ambapo wababe wawili walioupiga mwingi ni kutoka ukanda unaochezwa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) ikiwa ni pamoja na Canada.
Canada ilifanikiwa kushinda mechi zote tatu juzi Ijumaa ilipoifunga Hispania 88-85 ikisonga hatua ya robo fainali ambapo imeikwepa Marekani iliyocheza mchezo wa mwisho jana Jumamosi dhidi ya Puerto Rico.
Canada inashiriki mchezo huo wa kikapu tangu mara ya mwisho ishiriki mwaka 2000 na ni miongoni mwa timu tishio kwenye Olimpiki mwaka huu kutokana na ubora wa wachezaji ilionao ikiwa 10 kati ya 12 wakicheza NBA.
Wachezaji 10 ni Shai Gilgeous Alexander, Jamal Murray, Dillon Brooks, Andrew Nembhard, Kelly Olynyk, Dwight Powell, Trey Lyles, Luguentz Dort, Rowan Alexander “RJ” Barrett na Nickeil Alexander Walker.
Wakati Canada ikiwa na wachezaji 10 wanaocheza NBA, ni Marekani yenye wachezaji wote 12 wanaokipiga kwenye ligi hiyo na ndani yake yakiwemo majina makubwa yanayoongoza kwa kila kitu NBA.
Mabingwa hao mara tano wa Olimpiki wana mtaji wa mastaa wote wanaokiwasha NBA ambao ni LeBron James, Steph Curry, Kevin Durant, Jayson Tatum, Bam Adebayo, Joel Embiid, Derrick White, Jrue Holiday, Anthony Edwards, Anthony Davis, Devin Booker na Tyrese Haliburton.
Timu zote zinazopewa nafasi kubwa ya kuibuka bingwa upande wa kikapu zinaongozwa na mastaa wanaokiwasha NBA ambao pia wana balaa kwenye ligi na wamelihamishia kwenye michuano hiyo inayofanyika kila baada ya miaka minne.
LeBron James ndiye mchezaji kinara wa Marekani akipewa nguvu na wakali Kevin Durant anayeongoza kwa pointi nyingi zaidi kwenye michuano hiyo na pia yupo Steph Curry ambaye amecheza Olimpiki ya kwanza akisaka medali ya dhahabu kutokana na ukweli kwamba hatarajii kuwepo Olimpiki ya 2028 nchini Marekani.
Giannis Antetokoumpo kwa upande mwingine anaongoza matumaini ya Ugiriki kusaka taji la kwanza Olimpiki akiwa ndiye mchezaji pekee anayecheza NBA kutoka nchini kwao.
Dennis Schroeder kazi yake matata kwenye kikosi cha Ujerumani inamfanya awekewe matumaini ya kuibeba Ujerumani kama alivyofanya mwaka jana kwenye michuano ya mabara.
Schroeder kama LeBron na Giannis, walipata heshima ya kubeba bendera za mataifa yao siku ya ufunguzi wa mashindano hayo wakiwa manahodha jambo linalofanya wawe na kazi kubwa ya kupigania nembo za mataifa yao kuibuka bingwa.
Canada ilishafuzu robo fainali itakayoanza Jumanne ambapo kuongoza kundi kulimaanisha kuwapisha wababe Marekani kwenye mtoano ili kuisaka hatua ya nusu fainali na pengine fainali yenyewe ambayo inasubiriwa kutokea baada ya mechi za nusu fainali na hasa ikiwa Marekani na Canada inayoongozwa na Shai Gilgeous-Alexander (SGA) pamoja na Jamal Murray.
Nikola Jokic ambaye ni mchezaji bora mara tatu (MVP) wa NBA, ikiwemo tuzo ya mwaka huu anaiongoza Serbia ambayo haina nafasi kubwa kushinda kulingana na kukosa wasaidizi bora ukiachana na Nikola Jovic.
Swali linabaki ni timu ipi itabeba medali ya dhahabu kwenye Olimpiki mwaka juu?
01 – CURRY, Schroeder, Giannis wamecheza Olimpiki ya kwanza
04 LEBRON ameshiriki Olimpiki yake ya nne
13 PG13 anabaki mchezaji pekee wa draft ya 2010 anayecheza NBA
14 GORDON Hayward amestaafu NBA baada ya miaka 14 (kacheza Utah Jazz, Boston Celtics, Charlotte Hornets na Oklahoma City Thunder.