WANANCHI mzuka umepanda wakati klabu ya Yanga ikihitimisha Kilele cha Wiki ya Mwananchi ikiwa na kauli mbiu ya Nyie Hamuogopi, kinachofanyika leo Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sherehe maalumu ambazo uashiria msimu mpya.
Tamasha hilo huchagizwa na wasanii mbalimbali ambao hujitokeza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki, pia hutumika kucheza mchezo wa kirafiki ambapo safari hii itapambana na Red Arrows kutokea Zambia.
Wazambia hao hivi karibuni walikuwapo nchini kucheza michuano ya Kombe la Kagame 2024 kama waalikwa na wakasepa na taji hilo kwa kuifunga APR ya Rwanda kwa penalti 10-9 katika fainali ya kusisimua.
Mwanaspoti linakuletea orodha na matokeo ya mechi zote tano za nyuma ambazo Yanga imecheza tangu tamasha hilo kubwa na la kuvutia nchini lilipoasisiwa rasmi mwaka 2019 chini ya uongozi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Mshindo Msolla.
YANGA 1-1 KARIOBANG SHARKS (2019)
Hili lilikuwa pambano la kwanza la ‘Wiki ya Mwananchi’ kwa klabu ya Yanga na ilicheza mchezo na Kariobang Sharks ya Kenya.
Katika mchezo huu uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 na Kariobangi ilipata bao la utangulizi dakika ya 49 kupitia kwa Patrick Otieno kisha dakika sita mbele, Patrick Sibomana aliisawazishia Yanga kwa penalti.
YANGA 2-0 AIGLE NOIR (2020)
Yanga ikionekana timu tishio, ilicheza mechi ya pili dhidi ya Aigle Noir kutoka Burundi na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Mabao kwenye mchezo huo yalifungwa na Mghana, Michael Sarpong aliyeifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 59 kwa kichwa kikali kutokana na krosi iliyopigwa na Ditram Nchimbi huku lile la pili likifungwa na winga Tuisila Kisinda ‘TK Master’.
Ushindi huu uliamsha shangwe Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati huo, chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho Mserbia, Zlatko Krmpotic.
Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Aigle Noir, msimu uliofuatia Yanga ikaduwazwa kwa kuchapwa 2-1, dhidi ya Zanaco ya Zambia.
Mshambuliaji Mkongomani, Heritier Makambo alianza kuifungia Yanga bao la utangulizi dakika ya 30 tu ya mchezo baada ya kuwapiga chenga za fedheha mabeki wa Zanaco kutokana na pasi safi ya aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Baada ya bao hilo, Zanaco ilijibu mapigo ambapo winga wa timu hiyo, Ackim Mumba alisawazisha dakika ya 60, kisha kiungo Kelvin Kapumbu kufunga la ushindi dakika ya 76 na kuzima kabisa shangwe za maelfu ya mashabiki wa Yanga waliofurika kwa Mkapa.
Agosti 6, 2022, Yanga ilifanya vibaya tena katika sherehe hizo baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0, dhidi ya Vipers ya Uganda.
Mabao ya Vipers yalifungwa na kiungo, Milton Karisa dakika ya kwanza tu ya mchezo huo, huku lile la pili likifungwa na Anukani Bright dakika ya 64, mbele ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana.
Vipers iliyokuwa mabingwa wa Ligi Kuu Uganda ilikuwa chini ya kocha mkuu raia wa Brazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na baada ya kuipa mafanikio hayo, aliondoka na kujiunga na Simba Januari 3, 2023, ingawa alitimuliwa Novemba 7, 2023.
YANGA 1-0 KAIZER CHIEFS (2023)
Hili ndilo tamasha la mwisho lililofanyika Julai 22, 2023 na bao la Mzambia, Kennedy Musonda lilitosha kuipa timu hiyo ushindi wa pili baada ya ule wa mabao 2-0, dhidi ya Aigle Noir kutoka Burundi, mchezo uliopigwa Agosti 30, 2020.
Tamasha hili lilinogeshwa na mastaa wengi huku aliyeteka hisia za wengi ni aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mahlatsi Makudubela ‘Skudu’ ambaye alisajiliwa na kikosi hicho akitokea Klabu ya Marumo Gallants ya kwao Afrika Kusini.
Yanga iliingia katika mchezo huo ikiwa na kocha mpya Muagentina, Miguel Gamondi aliyetambulishwa Juni 24, 2023 kuchukua nafasi ya Nasreddine Nabi aliyejiunga na FAR Rabat ya Morocco japo kwa sasa amejiunga na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Nabi aliachana na kikosi hicho Juni 14, 2023, baada ya kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo na kuipeleka Yanga kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.
YANGA ?-? RED ARROWS (2024)
Safari hii Yanga imeialika Klabu ya Red Arrows ya Zambia katika tamasha hilo huku ikikumbukwa miamba hiyo ndio mabingwa wa Ligi Kuu Zambia (ZPL), baada ya kushinda michezo 21, kati ya 34, sare minane na kupoteza mitano na kukusanya pointi 71.
Timu hiyo ni mabingwa wa Kombe la ABSA 2024 huko Zambia, huku ikichukua pia ubingwa wa michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa kuifunga APR ya Rwanda kwa penalti 10-9, baada ya sare ya bao 1-1, ndani ya dakika 120.
Shauku ya mashabiki wa Yanga ni kuendelea kuona mastaa wapya waliosajiliwa na kikosi hicho msimu huu wakifanya vizuri ambao ni Prince Dube, Duke Abuya, Clatous Chota Chama, Jean Baleke, Chadrack Boka, Khomeiny Abubakar na Aziz Andambwile.
Timu zote zinakutana zikiwa ni mabingwa wa nchi zinapotoka ambapo Yanga imechukua Ligi Kuu Bara msimu uliopita ikiwa ni mara ya tatu mfululizo na Kombe la Shirikisho la FA, hivyo unapoita mchezo huu wa kibingwa baina yao utakuwa uko sahihi.