Rais Samia asisitiza kutekeleza 4R katika Muungano

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema katika kutekeleza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa mwaka 1964 Watanzania hawana budi kutekekeleza kwa vitendo falsafa ya 4R.

Tangu ameingia madarakani Machi 19, 2021 Rais Samia amekuwa na falsafa yake ya R nne (4R) anazozitumia katika utawala wake. 4R maana yake ni maridhiano (Reconciliation), mabadiliko (Reforms), ustahimilivu (Resilience) na kujenga upya (Rebuilding).

“Haya ndio yatakayoendelea kujenga amani na utulivu wa kudumu nchini kwetu na kuleta maendeleo endelevu, leo tuna fahari nchi imefika uchumi wa kati ngazi ya chini na kuna dalili za kuimarika ili kufikia uchumi wa ngazi ya juu.

“Hivyo tuendelee kudumisha amani ya nchi yetu ili kujenga uchumi na kuleta ustawi zaidi wa wananchi wetu,” amesema Rais Samia katika maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Sherehe za maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zimefanyika katika Uwanja wa Uhuru wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam.

Ameeleza hayo leo Ijumaa Aprili 26, 2024 katika sherehe hizo ambazo mwaka huu, zina kauli mbiu ya ‘tumeshikamana, tumeimarika kwa maendeleo ya Taifa letu’, zikihudhuriwa na marais wa Zambia, Kenya, Comoro, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kwa nyakati tofauti, Rais Samia amekuwa  akiwasisitizia wasaidizi na watendaji wake wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuzisimamia 4R katika utekelezaji wa majukumu yao, akisema ndiyo mwelekeo wa kujenga Taifa lenye umoja na mshikamano.

Mbali na hilo, Rais Samia amesema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia Muungano uliotokana na matakwa ya wananchi.

Amesema katika kipindi cha miaka 60 Taifa likiwa na watu wenye makabila zaidi ya 120, lakini wote wanaounganishwa na lugha moja ya Kiswahili na wamefanikiwa kuitunza na kudumisha Tanzania kwa amani na utulivu.

“Kupitia Muungano tumejenga umoja na mshikamano wa kitaifa, kuimarisha udugu na kupiga hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na kudumisha mila na desturi zetu, tunayo kila sababu ya kujivunia Muungano wetu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ametoa pole kwa walioathirika na mvua zinazoendelea kunyesha akisema anawaombea faraja huku Serikali ikifanya kila linalowezekana ili kurejesha miundombinu iliyoaharibiwa.

“Niendelea kutoa wito kwa wananchi kuzingatia tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili kuepuka madhara,” amesema.

“Kwa hali ya hewa ya leo haikuwezekana wote kuwa hapa. Lakini nina uhakika wapo katika runinga wanatufuatilia,”amesema Rais Samia.

Mvua hizo za El-Nino zilizoanza kunyesha Oktoba mwaka jana, zimesababisha vifo zaidi ya 160, uharibifu wa makazi, mali, miundombinu na kupandisha gharama za maisha ikiwemo nauli za usafiri.

Rais wa Comoro, Azali Assoumani amesema yeye na ujumbe wake wanajivunia kusherehekea miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Ni furaha kwetu sisi kuona ndoto na dhamira za waasisi waliounganisha mataifa haya mawili imejenga misingi ya kiuchumi na kijamii. Ni heshima kubwa Tanzania ni taifa tuliopakana nalo na nchi ya mfano yenye amani, demokrasia na maendeleo.

“Sifa moja kubwa ninayoweza kuitoa kwa Tanzania ni viongozi waliotangulia kutawala wamekuwa na ubinadamu na ukaribu na Taifa langu la Comoro,” amesema Rais Assoumani.

Mbali na hilo, Rais Assoumani amesema Tanzania imekuwa na vuguvugu la kutafuta uhuru katika mataifa mbalimbali ya Afrika ikiwemo Comoro.

Naye, Rais wa Burundi, Evarist Ndayishimye amesema Muungano wa Tanzania ni Muungano wa Afrika Mashariki, akisema jumuia ya Afrika Mashariki ni watu wenye umoja.

“Sababu iliyotutoa mimi na mke wangu kutoka Burundi ni kuja hapa kwenye sherehe kubwa hii, ndugu zangu Watanzania mnajua tangu enzi za mababu zetu, waha, waangaza walikuwa ndugu.

“Warundi na Watanzania walikuwa wakitembeleana, Warundi walikuwa wanaenda Tanzania kuuza majembe na Waha wa Uvinza walikuja Burundi kuuza chumvi,” amesema Rais Ndayishimiye.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema wakati Taifa linasherehekea miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kuna hatua kubwa zimepigwa katika sekta za kiuchumi na huduma za kijamii.

Mbali na hilo, Dk Mwinyi amesema Tanzania imeendelea kupata sifa kubwa kutokana na Muungano uliodumu na kuwa na amani, umoja na mshikamano.

“Nitumie fursa hii kutoa shukrani kwa viongozi waliopita wa Tanzania na Zanzibar kwa jitihada zao kudumisha malengo ya Muungano na kuzifanyia kazi changamoto.

“Ni jambo la faraja na kutia moyo kuona mambo mengi yaliyoangaliwa kama changamoto za Muungano yameshapatiwa ufumbuzi na machache yaliyobaki yapo katika hatua mbalimbali kupatiwa ufumbuzi,” amesema Dk Mwinyi.

Related Posts