Kalaba aruhusiwa kutoka hospitalini | Mwanaspoti

NAHODHA wa zamani wa Zambia, Rainford Kalaba ameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kujeruhiwa vibaya katika ajali ya gari mwanzoni mwa mwezi huu.

Kiungo huyo wa zamani wa TP Mazembe, alikuwa akiendeshwa katika gari aina ya Mercedes-Benz iliyogongana uso kwa uso na lori katika tukio la kutatanisha ambalo awali ilihofiwa amepoteza maisha yake.

“Bw.Rainford Kalaba ameruhusiwa kutoka UTH-Adult ambapo alilazwa baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani wiki mbili zilizopita,” alisema Ofisa wa Hospitali ya Mafunzo ya Chuo Kikuu, Nzeba Chanda katika taarifa iliyotolewa.

“Leo (Ijumaa Aprili 26) inaadhimisha siku 14 kamili tangu wakati wa kulazwa kwake. Ataenda kuendelea kuuguzwa katika nyumba ya familia yake.”

Wanasoka mbalimbali wameonyesha kumuunga mkono Kalaba, wakikumbuka mchango wake katika soka la Zambia kama kiungo mahiri na kiongozi.

Siku ya Alhamisi Aprili 25, Rais wa TP Mazembe Moise Katumbi alitoa shukrani za dhati aliposimama kando ya kitanda cha Kalaba.

“Nimekuja kumuona mwanangu Rainford Kalaba. Kwanza kabisa, namshukuru Mungu aliyemuokoa mwanangu. Niko Lusaka kabla ya kuondoka kwenda Misri,” alisema Katumbi akinukuliwa na mtandao wa Sports News Africa.

“Naweza kusema kwamba tayari amepona kwa asilimia 99,” alisema Katumbi, akikiri kupona kwa kimiujiza kwa Kalaba.

Mbali na kutoa shukrani zake, Katumbi alimuelezea mchezaji huyo, “Alikuwa mchezaji wa kuigwa, wachezaji wengine wanaweza kuchukua mfano wake, tulishinda naye mataji mengi. Yeye ni kama mtoto kwangu. Ninamshukuru Mungu, Serikali ya Zambia, na madaktari. Kama si wao pengine tungempoteza Kalaba.”

Kalaba alikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wa kihistoria wa Zambia katika Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012, ambapo walitwaa taji lao la kwanza kwa kuishinda Ivory Coast katika fainali ya kusisimua ambayo iliishia kwa mikwaju ya penalti.

Related Posts