Dodoma. Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) amewaondoa hofu Watanzania kuwa atafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu walizojiwekea.
Mwabukusi ameyasema hayo katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Dodoma leo Agosti 3,2024 mara baada ya kula kiapo mbele ya Wakili mwandamizi, Dk Mkunga Mtingele.
“Jambo jingine nililotaka kuzungumza ni wasiwasi, jana kuna mmoja amenipigia akaniambia Mwabukusi you are too confrontational (mkorofi), utakwenda kupigana na Serikali, mahakama na wakati mwingine kupigana na umma,” amesema.
Amesema alimweleza aende akasome kifungu cha nne na kwamba yeye si mpiga vita.
Mwabukusi amesema TLS inaongozwa na sheria, kanuni na taratibu walizojiwekea na kuwa sio jambo la mtu mmoja, hivyo wanafanya kazi na kuamua kama timu.
“Mwabukusi ataacha mambo yake na namna yake kama Mwabukusi, anapofanya kazi za TLS atasimama kama TLS kwa misingi tuliojiwekea na kulinda heshima ya chama,” amesema.
Amesema kipekee mambo watakayoyaangalia timu yake ni yale yanayowatenganisha kama chama na nia yake ni warudi na kuwa pamoja ili watimize majukumu yao ya kisheria kwa ufanisi kama timu moja.
Akizungumza kabla ya kukabidhi nafasi hiyo, Rais mstaafu wa chama hicho Harold Sungusia amesema kitu ambacho anachoondoka nacho katika mwaka mmoja wa uongozi wake ni kuwa mvumilivu na kuiishi miiko ya uongozi.
“Kitu ambacho naondoka nikiwa nimefurahishwa nacho ni kuwepo katika uongozi kulivyonikomaza kwa kuijua miiko ya uongozi. Unaweza ukatukanwa kuanzia asubuhi hadi jioni lakini kwa kuwa ni kiongozi mwenye dhamana ya kuongoza wataalamu utulie usiwe na mihemko,” amesema.
Sungusia amesema hizo ni miongoni mwa tunu anazoondoka nazo TLS akiwa na uwezo wa kuhimili mikikimikiki ya mawakili ambao wana maswali mengi.
Amesema pia amewafahamu mawakili wengi, kujenga uhusiano na kurudisha wafadhili wengi ambao walikuwa wameshaondoka ndani ya TLS.
“Hivi ninavyozungumza kulikuwa na mkataba wa Sh300 milioni tunatakiwa tuusaini. Kwa kifupi nimeondoka nikiwa nafahamu kuna mambo mazuri yanaifuata Tanganyika Law Society (TLS).
Sikuwa nimewafahamu vizuri mawakili lakini waone hivihivi, kwa sababu kila kitu kitahojiwa na mpaka mkubaliane jambo ujue kuwa ni lazima ufanye kazi ya ziada,” amesema.
Kuhusu kilichompa wakati mgumu amesema ni kupata mwafaka wa pamoja wa mambo, kwani hata alipokuwa na nia njema ya kufanya jambo, asingeweza kulifanya mpaka kuwe na mwafaka.
“Hilo kidogo lilikuwa ngumu kwa mtu ambaye ulikuwa unataka kufanya jambo kwa harakaraka na kutoa matunda. Kwa kazi hii ya uongozi inakutaka kuwa mstahimilivu, mvumilivu na kuwasikiliza wenzako ili muweze kwenda kwa pamoja,” amesema.