Huku Fei Toto, kule Chama Kombe la Muungano

KUTOKANA na ubora wa viungo waliopo Azam FC na Simba, huenda mechi ya fainali ya Kombe la Muungano ikaamuliwa na wachezaji wa nafasi hizo, wakati timu hizo zitakapokutana Jumamosi hii kuanzia saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Azam FC inashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo iliyokuwa imesimama kwa takribani miaka 20, tofauti na Simba iliyochukua mataji matano (1993, 1994, 1995, 2001 na 2002), Yanga ikiwa kinara kwa kuchukua mara sita (1983, 1987, 1991, 1996, 1997 na 2000), japokuwa mwaka huu timu ya Wananchi haijashiriki.

Michuano ya mwaka huu imezishirikisha timu nne zilizoanzia hatua ya nusu fainali, KVZ 0-2 Simba, KMKM 2-5 Azam FC ambapo kwa matokeo hayo, yanazifanya Simba na Azam kucheza fainali hiyo.

Ugumu wa mchezo huo, unatokana na matokeo ya timu hizo kwenye mechi za Ligi Kuu za hivi karibuni 2022/23 Azam 1-0 Simba (Oktoba 27), Simba 1-1 Azam (Feb 21), na 2023/24 Simba 1-1 Azam (Feb 9), na mzunguko wa pili wa ligi zitakutana Mei 9.

KWA NINI KUAMULIWA NA VIUNGO
Azam FC anayeongoza kwa mabao 14 ya Ligi Kuu Bara ni kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’, wakati kwa Simba waliogongana kwa mabao saba ni Said Ntibazonkiza ‘Saido’ na Clatous Chama, hivyo wana nafasi kubwa ya kuzibeba timu zao kwenye fainali ya Muungano.

WALICHOSEMA MAKOCHA
Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola amesema: “Mchezo utakuwa mgumu, Azam ina wachezaji wazuri na wenye ushindani, lakini tunawaamini wachezaji wetu watafanya kazi nzuri.”

Beki na nahodha wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alisema: “Tupo tayari kupambana kuhakikisha tunalichukua taji, tunajua mashabiki wetu wanajitoa katika nyakati ngumu na raha na wengi walikuwepo kuanzia mechi ya kwanza na tunatarajia kuwaona fainali, tutapambana kwa ajili yao.”

Kwa upande wa kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo amesema haitakuwa fainali nyepesi, lakini anakiamini kikosi chake kitafanya vizuri. “Simba ina kocha mzoefu, najua atakuja na mbinu kali katika mchezo huo, ila tupo tayari kupambana.”

Kiungo wa timu hiyo ya Chamazi, Fei Toto amesema: “Haitakuwa fainali nyepesi, Simba ina wachezaji wazoefu, jambo ninaloamini mashabiki watafurahia kuona burudani nzuri.”

Kwa upande wa mashabiki, Visiwani Zanzibar Azam inaonekana kupata sapoti kubwa, ingawa mashabiki wa Simba wapo ambao wanasafiri kuifuata timu yao popote inapokuwa.

UCHAMBUZI
Mtalamu wa data ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga, Said Maulidi ‘SMG’ alisema: “Kutokana na rekodi zao za mechi za Ligi Kuu, mchezo huo hautakuwa mwepesi, dakika 90 zitaipa furaha timu ambayo itacheza kwa umakini zaidi.”

Related Posts