Dar es Salaam. Baada ya kuibuka vurugu wiki iliyopita katika upangaji wa wafanyabiashara katika soko jipya la Tandale, sasa shughuli hiyo itafanywa na kamati maalum badala ya Mwenyekiti wa soko hilo, Juma Dikwe, kama ilivyokuwa awali.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi Agosti 3,2024, na Ofisa Biashara Mkuu wa Halmashauri ya Kinondoni, Philipo Mwakibete, alipozungumza na Mwananchi kuhusiana na sakata hilo.
Wiki iliyopita shughuli hiyo ilikwama baada ya kuibuka vurugu kati ya wafanyabiashara wa nafaka na wale wa matunda na mbogamboga hadi kuchapana ngumi hali iliyosababisha shughuli hiyo kusitishwa.
Katika sakata hilo, wafanyabiashara wa matunda walikuwa wakilalamikia wenzao wa nafaka kupangwa katika eneo linaloitwa VIP peke yao huku wao wakipangwa eneo la shimoni ambalo walidai sio rafiki kwa mazao wanayoyauza kwa kuwa yanaharibika mapema.
Mwakilishi wa wafanyabiashara hao, Pius Setebe, alimtuhumu mwenyekiti kukiuka makubaliano yao ya kupangana upande wa Mashariki na Magharibi kama walivyokuwa wakikaa awali kabla ya soko kujengwa na hata kwenye vikao vyao mbalimbali kipindi cha ujenzi walishakubaliana hilo.
Setebe amesema watakuwa tayari shughuli hiyo iendelee kama hilo la kupangwa pande mbili litatekelezwa.
Kwa upande wake, Dikwe amesema amefanya upangaji huo kwa kuwa kamwe biashara ya nafaka haiwezi kuchanganywa na za matunda na mbogamboga, lakini pia ni katika kurahisisha uondoaji taka kwa kuwa ndizo zinazozalisha taka kwa wingi kuliko bidhaa nyingine sokoni hapo.
Pia Dikwe amesema wafanyabiashara hao wa matunda wanaligomea hilo, wakati walishaelezwa katika vikao vyao mbalimbali vilivyofanyika kabla na wakati wa ujenzi wa soko hilo.
Akizungumza walichoamua Halmashauri, Mwakibete amesema wataunda kamati itakayokuwa na mwakilishi kutoka vitengo 11 vilivyopo sokoni hapo kusimamia shughuli hiyo.
“Kwa kufanya hivyo tutajenga imani kwa kila mfanyabiashara sokoni hapo kuwa atapangwa anapostahili, badala ya kuacha suala hilo kwa mtu mmoja kwa kuwa sisi tunamthamini hata yule anayeuza nyanya kwa mafungu,” amesema Mwakibete.
Pia amesema katika ugawaji huo, wamezingatia makubaliano yaliyofanyika katika kikao chao wakati soko hilo lilipokuwa katika mpango wa kujengwa, ambapo iliamuliwa kuwa wafanyabiashara wa nafaka na wale wa matunda wakae eneo hilo moja la VIP, huku wale wa miwa wakikaa eneo la shimoni.
Ofisa huyo biashara amesema wasingependa kuona kuna upendeleo katika upangaji huo, kwa kuwa lengo la Halmashauri ya kujenga soko hilo ni kila mfanyabiashara kufanya shughuli zake katika mazingira yaliyo bora.
“Haiwezekani wakati wa soko likiwa bovu mlikaa wote eneo moja, jua, mvua vikawa vya kwenu, leo soko limeboreshwa baadhi wajione wao wana haki ya kukaa eneo moja wenyewe kwa kisingizio kuwa bidhaa zao haziwezi kuchanganyika na za wengine, hilo Halmashauri haitakubali,” amesema.