Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeanza uchunguzi wa kubaini watu wasiojulikana wanaodaiwa kumteka Shadrack Chaula (24), mkazi wa Kijiji cha Ntokela wilayani Rungwe.
Chaula anadaiwa kutekwa na watu hao ikiwa ni takribani siku 20 zimepita tangu alipotoka Gereza la Ruanda Mkoa lililoko mkoani Mbeya, alipokuwa amehukumiwa kifungo cha miaka miwili au kulipa faini ya Sh5 milioni.
Baada ya kifungo hicho kilichotolewa Julai 4, 2024, wadau mbalimbali waliendesha michango mitandaoni na kufanikiwa kupata kiasi hicho cha fedha na Julai 8, 2024 ililipwa na kuachiwa.
Juzi Ijumaa, katika mitandao ya kijamii kumekuwa na taarifa zinazoeleza kutekwa na watu wasiojulikana wakiwa na gari nyeusi kisha kuondoka naye na jitihada za kumtafuta zimekuwa zikiendelea.
Jana Jumamosi, Agosti 3, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya (RPC), Benjamin Kuzaga amesema kimsingi wanafuatilia uwepo wa tukio hilo.
“Tayari tumeanza uchunguzi ili kubaini ni kweli alitekwa kama mitandao ya kijamii ilivyoripoti maana wapo waliomchangia kutoka gerezani,” amesema.
Mmoja wa viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Kijiji cha Ntokela ya Ndato, aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema wanashindwa kuelewa matukio hayo yako vipi dhidi ya familia ya huyo kijana.
“Alikuwa magereza alipotoka kama viongozi hatukujua na tulisikia tu kaenda Dar es Salaam, leo lingine limeibuka kama katekwa kweli wazazi wake walishindwa kutoa taarifa ili tufuatilie,” amesema kiongozi huyo.
Amesema jambo hilo lina mkanganyiko, kama kuna jambo nyuma ya pazia watafuatilia kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kama ni masuala ya kisiasa yanatumika kupitia kwake itaeleweka maana ni kipindi cha kuelekea uchaguzi,” amesema.
Julai 4, 2024, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya alimhukumu kifungo hicho baada ya mshtakiwa huyo, kukiri kosa la kuchoma picha ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Baada ya kukiri kosa hilo, Hakimu Shehagilo alimtia hatiani Shadrack kwa kosa la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa TikTok, jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya makosa ya mtandao kifungu cha 16.
Awali, alisomewa shitaka hilo na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Rosemary Mgenije, aliyekuwa akisaidiana na Wakili Veronica Mtafya.
Alisema Juni 22, 2024, eneo Ntokela lililopo Kata ya Ndato, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, mshtakiwa alitenda kosa hilo kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii @jet.fightershop akiwa ameshika picha inayomwonyesha Rais Samia, akisema:
“Kwa kuwa umeshindwa kutetea Taifa lako lisiathirike na ushoga, hii video inakuhusu wewe na si mtu mwingine wakati ukijua taarifa hizo ni uongo na upotoshaji kwa jamii,” amedai Wakili Veronika.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, upande wa mashtaka ulieleza kuwa, ingawa hauna kumbukumbu ya makosa ya nyuma, uliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa, ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kumdhalilisha Rais wa nchi.