Chanongo hatihati kuivaa Mbuni | Mwanaspoti

Arusha: Kiungo mshambuliaji wa Pamba Jiji FC, Haruna Chanongo huenda akakosa mchezo wa mwisho wa Ligi ya Championship dhidi ya Mbuni FC kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya nyama za paja.

Umuhimu wa nyota huyo unatokana na kuwa ndiye kinara wa ufungaji kwenye kikosi hicho cha TP Lindanda kinachonolewa na kocha Mbwana Makata akiwa amehusika kwenye magoli 15 akifunga 12 na kutoa pasi za mwisho zilizozaa mabao mengine matatu.

Mchango wake umewezesha Pamba kuwa timu ya pili Championship kwa kufunga mabao mengi ikifunga 50 huku ikizidiwa Biashara United pekee ambayo imefunga mabao 56.

Daktari wa timu hiyo, Dishon Chacha ameiambia Mwanaspoti kwamba nyota huyo alitonesha majeraha aliyokuwa nayo ya nyama za paja kwenye mchezo uliopita dhidi ya TMA Stars ambayo Pamba Jiji ilishinda mabao 2-1.

“Alikuwa na majeraha ya kwenye paja kwa sababu ya kufanya mazoezi kwa muda mrefu, nyama zikapanuka na kuchanika na si kwamba aliumia katika mchezo huo bali alitonesha majeraha iliyopelekea kushindwa kuendelea na mchezo,” amesema Dk. Chacha.

Amesema Chanongo ambaye amewahi kucheza katika klabu kadhaa ikiwemo Simba SC na Mtibwa Sugar zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, alilazimika kucheza mechi dhidi ya TMA kutokana na hali halisi ya mchezo uliokuwepo na umuhimu wake.

“Kucheza itategemea na uamuzi wa waalimu kwani majeraha yake ni ya muda mrefu,” ameongeza.

Mbali na nyota huyo wachezaji wengine wawili Ismael Mtamba na Saleh Seif ambao nao waliumia katika mchezo dhidi ya TMA Stars kwa sasa wanaendelea vyema ambapo uwezekano wao wa kucheza mchezo ujao ni mkubwa.

Akizingumzia hali ya kikosi kwa ujumla meneja wa timu hiyo, Japhary Juma amesema kikosi kinaendelea na maandalizi kujiandaa na mchezo dhidi ya Mbuni FC wa Jumapili hii Aprili 28 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha ambao kwao ni muhimu kushinda au kutoa sare ili kupanda daraja kwenda Ligi Kuu Bara.

Pamba inashika nafasi ya pili kwa alama 64, alama tatu nyuma ya kinara Ken Gold FC yenye 67 ambayo tayari imepanda daraja hivyo TP Lindanda inahitaji angalau sare katika mchezo wa mwisho ili kupanda daraja moja kwa moja na kukata kiu ya mashabiki wa soka Mwanza ambao wamesubiri kwa zaidi ya miaka 20.

Kama Pamba itapoteza hlafu Mbeya Kwanza inayoshika nafasi ya tatu kwa alama 62 ikashinda basi Mbeya Kwanza itafikisha alama 65 na kupanda, lakini kama itatoa sare itafikisha 65 ambapo itapanda kutokana na tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Utofauti wa timu hizo kwenye magoli ya kufunga na kufungwa iko hivi, Pamba imefunga mabao 51 na kufungwa 17 huku Mbeya Kwanza FC ikifunga 49 na kufungwa 28.

Related Posts