Vinyongo, visasi vinavyogharimu maisha ya wenza

Mwanza. Hivi karibuni matukio ya wanandoa kujichukulia hatua mkononi ikiwemo kuua wenza wao yameshamiri huku, sababu kubwa ikitajwa ni visasi na vinyongo.

Hili linatokana na kutokuwepo nafasi ya kuzungumza kutafuta namna bora yakutatua tatizo pale wanapotofautiana.

Kufuatia hali hiyo baadhi ya wadau wakiwemo viongozi wa dini wamezungumza na jarida la Familia na kushauri namna bora ya wanandoa kukabiliana na changamoto zao ili kuepukana na mauaji dhidi ya wenza.

Mchungaji wa kanisa la wadventista wasabato katika jimbo la Nyanza kusini, Emmanuel Mpina anasema kwenye ndoa kumekuwepo na changamoto kubwa ya vinyongo vinavyosababisha chuki na hata uhusiano mbovu kwa wanandoa.

Anasema vijana wengi wanakutana ndani ya muda mfupi kabla ya kujuana vizuri wanaingia kwenye ndoa hivyo kukosa ufahamu wa namna ya kuchukuliana kwenye ndoa nakupelekea mawasiliano kuwa siyomazuri kati yao jambo linalopelekea mambo mengi.

“Ndoa ni taasisi na ndoa ni jambo pana lenye kina kirefu sababu muasisi wake ni Mungu, sasa watu wengi wanaingia kwenye mahusiano bila kuwa na elimu sahihi kuhusiana na elimu ya ndoa.

Wengi wanakutana ndani ya muda mfupi wanaanza mahusiano lakini mwisho wake sababu jambo hilo limebeba mambo mengi wanajikuta kwamba kwasababu ya kukosa ufahamu namna ya kuchukuliana na hali ya ndoa yenyewe basi kinachotokea kwanza mawasiliano yanakuwa siyo mazuri kati yao,”anasema.

Mchungaji huyo anabainisha kuwa jambo la aina hiyo likitokea husababisha madhara mengine zaidi ikiwemo mmoja wapo kuanzisha uhusiano nje ya ndoa kama sehemu ya kupata faraja.

“Badala ya kutatua tatizo hilo anatengeneza sasa uadui mkubwa zaidi na ndiyo haya tunavyoshuhudia wengi wanajikuta wanaanza kulipizana kisasi wananza kugombana na mwisho wa siku kwa sababu ya wivu wa mapenzi anaamua kumfanyia mwingine kitendo kibaya kwa sababu ya hasira,”

Kwa mujibu wa mchungaji huyo ndoa inaanzia katika familia kwa maana ya malezi au wazazi wanapaswa kuwa walimu wa kwanza kuwafundisha watoto wao hasa wanapofikia umri wa kuingia kwenye uhusiano kwa kuwapa elimu sahihi kuhusu ndoa.

Hayo yameelezwa pia na Imamu wa msikiti mkuu wa Baraza la waislamu (Bakwata) Mkoa wa Mwanza, Ustadhi Khalifu Issa ambaye anaeleza kinyongo huwa kinamsukuma mtu kufanya matukio mabada dhidi ya mwenza wake.

“Mtu akiwa na kinyongo ni hasira ndizo zinamjaa kwahiyo hizo, akiwa katika hali hiyo anaweza kufanya jambo linaloweza kumdhuru mwingine ndiyo tunasikia mauaji dhidi ya wenza.

“Kiuhalisia mapenzi hutokana na moyo kukubali kitu na mtu anapokubali kitu basi huwa tayari kufanya chochote kile kwaajili ya kupata kile alichokikubali. kwahiyo mtu anapompenda mtu anakuwa tayari kufanya chochote kitu kwaajili ya kumlinda” anasema na kuongeza

“Inapotokea sasa ikitokea yule mtu anayempenda akifanya jambo ambalo yeye halitaki au halipendi lazima kiuhalisia na kibinadamu kuna kitu kitakachotokea ambacho ni chuki au kinyongo”.

Anasema ili kuepusha haya wanandoa wanapaswa kufahamu majukumu yao katika ndoa akidai kila mtu ana nafasi yake, ana wajibu wake na kazi yake maalum iliyomfanya akawa pale.

“Kipi kifanyike kunusuru hayo yote? Ni wanandoa kupata elimu, kuelimishwa na kutengenezwa ni namna gani kuingia katika ndoa na kipi katika ndoa kinachostahili na kipi katika ndoa hakistahiki au unapomkosea mtu unatakiwa kufanya mambo haya kuliko kumpiga mwenzako, kumjeruhi au kumuua kabisa”.

Askofu wa Kanisa la IEAGT Shinyanga mjini Kambi ya Waebrania, David Mabushi anasema wanandoan hawana budi kuepuka visasi hasa pale mmoja kwenye ndoa anapokosea ili kuondoa migogoro huku akitaja changamoto ya malezi na imani za ushirikina kuchangia migogoro kwenye ndoa.

“Mauaji mengi yanatokana wakati mwingine na wivu au kisasi..kunapotokea wivu mtu anaamua kulipa kisasi sasa hiyo inachochea badala ya kurekebisa, jambo lingine ni kukosa uelewa kwahiyo wanandoa wengi wanakuwa si waelewa ndomana hata kunapotokea kutoelewana hawajui wafanye nini ,”alisema

Askofu Mabushi anasema ni muhimu kwa wanandoa kushugulikia migogoro mapema ikiwemo kuwaona viongozi wa kidini, kimila hata kiserikali mapema pindi matatizo yanapotokea kabla moto haujawaka na kuunguza ndoa zao.

Sudi Jamiri ambaye yupo kwenye ndoa miaka 22 sasa, anasema visasi na vinyongo vitokanavyo na wivu wa mapenzi ndio chanzo kikubwa cha mauaji ya wanandoa akitaka kabla ya wenza kuingia kwenye ndoa viongozi wa dini wawape elimu maalumu ya kuwawezesha kuchukuliana madhaifu na kuzungumza ili kuondoa vinyongo.

“Wanandoa wajue wana nafasi ya kuongea, kutafuta namna bora ya kutatua matatizo yao pale mwenza anapojihisi amekwazika au ameumia…kuna namna anaweza kufuata kwaajili ya kutoa dukuduku lake na kutibu maumivu yake ikiwemo kuwashirikisha wazazi, washenga kwaajili ya kutafuta namna bora ya kutatua kuliko kukaa nalo.”anasema Jamir

Macelina Edward anasema vinyongo ana visasi vinatokana uaminifu ndani ya ndoa kupotea akishauri wanandoa kusamehana baada ya kutofautiana na kama wataona makosa hayasameheki basi waachane kuliko kufikia hatua ya kuuana.

“Wanaume wengi wanaua wake zao kwa sababu wanakaa na vitu rohoni, wanakosa ushauri mara nyingi inatokea hivyo. Watu wakiwa na hofu na Mungu, wakitafuta namna bora ya kutatua matatizo yao mauaji hayatoweza kutokea,”anasema Macelina.

Wakati viongozi wa dini wakieleza hayo mwanasaikolojia Jacilita Ndaki anasema iwepo elimu ya mahusiano katika ngazi mbalimbali itakayomfundisha mtu namna ya kutawala hisia zake.

Anashauri pia watu kuwa utamaduni wa jamii kukutana na wataalumu wa saikolojia kupata elimu ya nini anaweza kufanya ikiwa atakabiliana na jambo gumu.

“Jambo lingine watu wafundishwe kuanzia utoto mpaka kukua haki za msingi za binadamu ikiwemo haki ya kuishi kwa sababu huyu anavyoamua kuyatoa maisha yake na mwenzake maana yake haoni yule ana haki ya kuishi na haki ya kuishi inakuwa imekiukwa,”anasema Jacilita.

Baadhi ya matukio ya mauaji yaliyothibitishwa na Makamanda wa Polisi wa mikoa yalipotokea na kuripotiwa na gazeti hili ni pamoja na lile lililotokea Juni 17, 2024 ambapo mchimbaji wa madini Msasa – Nyarugusu mkoani Geita, Ndaki Shabani (35) alidaiwa kumuua mke wake, Pili James (37) kwa kumpiga na kitu kizito kichwani.

Baada ya kufanya tukio hilo Shabani alitoroka na kujificha lakini kwa ushirikiano wa wananchi na jeshi la polisi walibaini alipo na kumkuta amekunywa vitu vinavyodhaniwa ni sumu, walimpeleka hospitali kwaajili ya matibabu.

Tukio lingine lilitokea Aprili 13, 2024 mkazi wa Mwamanyili Halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza, Jackson Kalamji (49) akidaiwa kumuua mkewe, Mariam Bulacha (42) kwa kumchoma visu sehemu mbalimbali mwilini, baada ya kumtilia shaka kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine.

Kabla ya mauaji kutokea, inadaiwa ugomvi ulianza baina ya wa wanandoa hao ambapo Jackson alihisi mkewe anatongozwa na mwanaume ambaye yeye anamtongoza mkewe.

Mauaji mengine ya wenza yaliyotikisa ni ya Ofisa Kilimo wa Kata ya Neruma wilayani Bunda Mkoa wa Mara, Julius Rubambi (38) ambaye alifariki dunia Aprili 2, 2024 kwa madai ya kuchomwa kisu na mke wake kisa wivu wa mapenzi.

Pia lile lililotokea mkoani Kilimanjaro ambapo Beatrice Elias (36), mkazi wa Mtaa wa Katanini Wilaya ya Moshi alidaiwa kumuua mumewe, Ephagro Msele (43) kwa madai ya kumkuta kwa mzazi mwenzake.

Related Posts