Prince Dube awakuna Wananchi mapemaa

WAKATI zimesalia saa chache kabla ya kikosi cha Yanga kutambulishwa kwa mashabiki katika sherehje za kuhitimisha Kilele cha Wiki ya Mwananchi, mashabiki wa klabu hiyo mapema tu wameanza kumtja straika mpya wa timu hiyo, Prince Dube wakidai ndiye usajili uliowakuna zaidi.

Mashabiki hao wamesema Dube ndioye aliyebeba kwa sasa matumaini yao katika eneo la mbele na hasa wakati huu wanaenda kuvaana na Simba katika Ngao ya Jamii siku ya Agosti 8 kabla ya kuanza kazi kwenye michuano ya kimataifa  ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho.

Nyota huyo amejiunga na Yanga msimu huu baada ya kuachana na matajiri wa Azam FC, huku mashabiki wa kikosi hicho wakipongeza viongozi kwa kukamilisha usajili huo wakisema wamelamba dume.

Mmoja wa shabiki wa timu hiyo aliyehudhuria kilele cha ‘Wiki ya Mwananchi’ kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, aliyejitambulisha kwa jina la Nurath Athuman amesema, usajili wa Dube ni silaha tosha ya kuwapa ubingwa msimu ujao.

“Msimu huu tumefanya usajili mzuri sana ila kwangu wa Dube umenipa jeuri ya kutamba mtaani, naamini msimu ujao tunabeba tena mataji yote ya ndani,” amesema Nurath.

Kwa upande wa shabiki mwingine aliyejitambulisha kwa jina la John JR amesema, hakuna asiyejua uwezo wa Dube hivyo mashabiki wa timu pinzani wajipange kwa maumivu mengine.

Shabiki mwingine, Ally Hamis amesema, licha ya Dube kuonyesha uwezo mkubwa hadi sasa ila wachezaji wote waliosajiliwa ni wazuri na wanawapa matumaini makubwa msimu ujao.

Tangu nyota huyo asajiliwe na kikosi hicho, tayari amefunga mabao mawili akianza katika michuano ya Mpumalanga Premier International Cup 2024, wakati alipoifungia Yanga iliposhinda 1-0, dhidi ya TS Galaxy ya Afrika Kusini.

Bao lingine Dube alifunga wakati timu hiyo iliposhinda mabao 4-0, dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika mchezo wa kirafiki ambao uliipa Yanga ubingwa wa michuano ya Kombe la Toyota Cup 2024.

Mashabiki hao wametoa kauli hiyo wakati wa kilele cha tamasha la ‘Wiki ya Mwananchi’, linalofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni msimu wa sita kufanyika tangu lilipoasisiwa mwaka 2019, na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Mshindo Msolla.

Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA msimu uliopita, imenasa saini ya nyota wapya saba ambao mbali na Dube ila wengine ni Clatous Chama aliyetokea Simba, Jean Baleke (Al-Ittihad SCS Tripoli), Aziz Andambwile (Fountain Gate), Chadrack Boka (FC Lupopo), Khomeiny Abubakar, Duke Abuya (Singida Black Stars).

Dube amesajiliwa baada ya kuitumikia Azam kwa misimu minne mfululizo akiifungia zaidi ya mabao 30 katika michuano yote tangu alipojiunga nayo mwaka 2020 akitokea Highlander ya Zimbabwe, huku akiwa na kismati cha kuitungua Simba mara kadhaa alipokutana nao katika michuano tofauti.

Related Posts