Mtanzania uso kwa uso na Mzambia usiku wa vitasa

MJI wa Kyela utasimama kwa muda kupisha usiku wa ngumi pale mabondia 18 wakiwamo Joseph Mwaigwisya (Tanzania) na Mbachi Kaonga raia wa Zambia watakapozichapa Agosti 8 katika ukumbi wa Unenamwa uliopo mjini humo.

Mabondia hao kila mmoja anajivunia rekodi zake za ndani na nje na kufanya shauku kuwa kubwa kwa wapenzi wa ndondi na Mwaigwisya amecheza mapambano 12, ameshinda nane ikiwamo KO mbili na kupoteza mawili, huku Kaonga akicheza matano na kushinda yote ikiwamo KO nne.

Mwandaaji wa pambano hilo, ambaye ni promota wa ngumi za kulipwa, Edgar Mwansasu alisema ameamua kupeleka pambano hilo mjini Kyela ikiwa ni sehemu sahihi kuamsha mchezo huo kwa vijana.

Amesema kwa kipindi kirefu ngumi zimeonekana kuwa kimya mkoani Mbeya, hivyo kupitia pambano hilo linalohusisha mabondia wenye rekodi zao kimataifa itakuwa sehemu ya kuamsha upya mchezo huo.

“Ngumi ni ajira na inainua kipato kwa vijana, mchezo huu umekuwa kimya sasa na kutokana na pambano hili litaenda kuamsha upya ari na morali katika mchezo huo,” alisema Mwansasu.

Mwansasu aliongeza mbali na wababe hao, kutatanguliwa na mapambano mengine tisa kwa kuwashirikisha mabondia wa ndani ya nchi ikilenga kuwapa nafasi kuonyesha uwezo wao.

“Niwaombe wananchi na wapenzi wa ngumi kujitokeza kwa wingi, kwani viingilio vipo poa, lakini lengo la mapambano haya ni kuwainua vijana kiuchumi kupitia mchezo huu,” alisema promota huyo.

Related Posts