Tanzania sasa mtazamaji mbio za magari Afrika

KWA mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili, Tanzania imeshindwa kuandaa raundi ya nne ya mbio za magari ya ubingwa wa Afrika  na ukata umetajwa kuwa ndiyo sababu kuu.

Kwa mujibu wa kalenda ya Chama cha Mbio za Magari cha Dunia (FIA), Tanzania ilikuwa iandae raundi ya nne Agosti 23-25 mwaka huu, lakini mashindano hayo yamefutwa kwa mujibu wa maafisa wa chama kinachosimamia mchezo huu.

Taarifa ya Shirikisho la Mbio za Magari Tanzania imethibitisha na kusema kuwa ilibidi kuyafuta mashindano ya mwaka huu licha  ya jitihada kubwa ya kusaka udhamini kutoka mashirika, taasisi na makampuni binafsi.

Baada ya Tanzania kushindwa kuandaa raundi ya nne ya mbio za magari ya Afrika, raundi ya nne  itafanyika nchini Burundi katikati ya Septemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya FIA, raundi ya nne itajulikana kama Rallye International Du Burundi na itafanyika kuanzia Septemba 20 hadi 22 mwaka huu.

“Tumehuzunisahwa sana, lakini hatuna cha kufanya kwani jitihada zetu zote za kunusuru mchezo zimegonga mwamba,” alisema Randeep Birdi dereva anayeongoza mbio za ubingwa wa taifa nchini Tanzania.

Kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, Tanzania imekuwa ni moja ya mataifa nane ya Afrika yanayopewa heshima ya kuandaa mashindanio ya mbio za magari ya ubingwa wa Afrika.

Mataifa mengine yanayofanya vizuri katika uandaaji wa mchezo wa mbio za magari  kwa ngazi ya Afrika ni Kenya, Uganda, Zambia, Rwanda, Afrika ya Kusini, Zimbabwe na Ivory Coast.

Tanzania ililipata mafanikio makubwa katika miaka ya 2005 hadi 2015,  kipindi ambacho  madereva wa Kitanzania waliweza kung’ara  na kutoa ushindani mkubwa kwa madereva bingwa wa mbio za magari  barani Afrika.

Madereva waliofanya vizuri katika kipindi hicho ni pamoja na Omary Bakhresa, Ahmed Huwel, Navraj Hans, Kirit Pandya, Pano Calavrias ambao mara nyingi walikuwa pia wakitoka nje ya Tanzania katika azma yao ya kuwania ubingwa wa Afrika.

Wakati mchezo ukiwa katika ubora wake, madereva wa Tanzania  walishiriki mashindano ya mbio za magari nchini Afrika ya Kusini, Kenya, Uganda na Rwanda,lakini miaka ya karibuni wengi wameshindwa kutoka.

Related Posts