Hao Prisons mikwara mingi | Mwanaspoti

WAKATI Tanzania Prisons ikihitimisha kambi yake Dar es Salaam na kurejesha nyota wake wawili, benchi la ufundi na uongozi umetambia kikosi chake wakiahidi msimu ujao kucheza kimataifa.

Wajelajela hao waliweka kambi yao Dar es Salaam kwa takribani mwezi mmoja na leo Jumatatu watakuwa nyumbani jijini Mbeya kwa maandalizi ya mwisho ya Ligi Kuu inayotarajia kuanza Agosti 16.

Pamoja na kutumia takribani siku 28 jijini Dar es Salaam kwa kambi ya muda, imewarejesha nyota wake wawili, Ezekia Mwashilindi na Vedastus Mwihambi kwa ajili ya msimu ujao.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbwana Makata alisema kambi hiyo haikuwa ya kutembea Dar, bali ilikuwa mahususi kujiweka fiti na kwa maandalizi waliyofanya matarajio yao ni makubwa ligi ikianza.

Alisema anajivunia uwezo na utimamu walioonyesha mastaa wake na wamekuwa na muda mzuri kujaribu mastaa kwa mechi tofauti za kirafiki na kwa sasa wapo tayari kwa Ligi Kuu.

“Tumekuwa na muda mzuri wa maandalizi, vijana wameonekana kuwa fiti na tunarejea Magereza Mbeya kwa mipango ya mwisho kusubiri ratiba kila mchezaji ana hamu ya kutoa mchango wake kikosini,” alisema Makata.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Chacha Waisaka alitamba kwa kikosi walichonacho wanaamini msimu ujao lazima wawakilishe nchi kimataifa kutokana na upana na ubora wa wachezaji.

“Kambi ya Dar es Salaam imekuwa na mafanikio makubwa, benchi la ufundi limekuwa na program nzuri ambazo tunaona uhalisia wa Prisons kucheza kimataifa mwakani, mashabiki watupe ushirikiano zaidi,” alisema Waisaka.

Related Posts