Ufadhili wa kilimo-viwanda ulivyobadili maisha ya Ruhigo

Kigoma. Kijana Ruhigo Mayala, ameleta mapinduzi ya kilimo katika kijiji chake cha Itebula, wilayani Uvinza Mkoa wa Kigoma.

Safari yake iliyojaa uvumilivu, uthubutu, ubunifu na faida ya elimu inaonesha matunda ya programu ya Serengeti Breweries Limited (SBL) ya udhamini wa kilimo-viwanda ya kuwawezesha wanafunzi katika masomo ya kilimo.

“Baada ya kumaliza masomo yangu ngazi ya cheti, nilishindwa kuendelea kutokana na changamoto za kifedha. Udhamini wa Serengeti Breweries ulinifungulia ukurasa mpya katika maisha yangu. Nilipata matumaini mapya ya kufuatilia ndoto zangu ya kuendelea na masomo ya kilimo,” anasema Ruhigo.

Katika Chuo cha Mafunzo ya Kilimo cha Igabiro (ITIA), Ruhigo si tu alipata maarifa ya kitaaluma, bali pia stadi za vitendo na ushauri wa kitalaamu.

Baada ya kumaliza masomo yake ya diploma katika kilimo, anasema alirudi kijijini kwao Itebula akiwa na lengo la kutumia mbinu za kisasa katika kilimo na kuhamasisha jamii yake kufuata mfano wake.

Awali, Ruhigo anasema aliamua kulima ekari moja ya mpunga akitumia mbinu za kisasa alizozipata chuoni.

Mavuno yalimshangaza hata mwenyewe: “Nilivuna karibu gunia 20 za mpunga kutoka kwenye ekari moja. Hata majirani zangu hawakuamini mpaka wakawa na shauku kujua nilifanyaje.”

Anasema mafanikio hayo ya kwanza yalibadili mwelekeo wa maisha yake, kwa kuwa yalimpa mtaji wa kukuza shughuli zake za kilimo na kuwekeza zaidi kwenye ardhi yake.

Anasema aliongeza eneo la kulima, akahifadhi mavuno yake na kuuza kwa bei nzuri mpaka akaanza kununua mazao kutoka kwa wakulima wengine.

Kijana huyo anasema ujasiriamali uliboresha si tu hali yake kifedha, bali pia alikuwa mfano wa kuigwa kwa wengine kijijini kwake.

Akiwa na malengo ya kuleta mabadiliko makubwa zaidi, Ruhigo anasema ameamua kujiendeleza kielimu, kwa kuwa sasa anasomea Shahada ya Usimamizi wa Ushirika na Uhasibu katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

Anasema maono yake ni kuleta mapinduzi na mabadiliko chanya katika kilimo kwenye jamii yake.

“Nataka kuboresha kilimo kijijini kwangu kwa kuanzisha miradi ya umwagiliaji katika Kata ya Nguruka, ili kuongeza mavuno ya wakulima na wanufaike zaidi na juhudi zao,” anasema Ruhigo.

Anatarajia kujenga kisima kitakachotumia nguvu za jua, ili kutoa huduma ya uhakika ya maji kwa umwagiliaji, kuruhusu kilimo cha mazao mbalimbali kama mahindi, mtama, ngano na nafaka.

“Umwagiliaji utasaidia wakulima kulima muda wote kutokana na uhakika wa maji bila kujali msimu. Tunataka kutumia teknolojia katika kilimo ili kuwawezesha wakulima wetu,” anasema Ruhigo.

Ruhigo pia ana mpango wa kuwaunganisha wakulima katika kata yake na Serengeti Breweries, ili wawe na uhakika na soko la mazao yao.

“Wakulima wanaweza kupata uhakika wa soko la mazao yao kutoka kwa SBL, kitu ambacho kitawafanya waongeze uzalishaji na hivyo kuboresha maisha yao,” anaeleza.

Zaidi ya hayo, Ruhigo ana mpango wa kuwaunganisha wakulima kwa kuwahamasisha kuunda kikundi cha ushirika, kwa kuwa anaamini wataweza kujadili masuala yao kwa pamoja na kudai haki zao kwa sauti moja kama kikundi.

Ushirika huo unaweza kuwa jukwaa la wakulima kubadilishana maarifa, kushughulikia changamoto kwa pamoja, na kujadiliana upatikanaji wa bei na soko bora kwa mazao yao.

Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na programu hiyo, Mkazi wa Kijiji cha Itebula, Saimon Mbaje anasema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inapaswa kuongeza utoaji wa programu kama hizo za kilimo ambazo kwa sasa ni mkombozi kwa vijana.

“Mimi nina mtoto kamaliza Chuo Kikuu Dodoma (Udom) yupo tu nyumbani, naona sijui kozi aliyosoma haina mpango kama huu. Ona huyu mwenzao kasoma, lakini elimu yake imemsaidia ndiyo kama unavyomuona hapa, si tegemezi tena, ila sasa yeye anategemewa zaidi na familia yake,” anasema Mbaje.

Naye Angela Nyambo, mkazi wa Kigoma anasema vijana wasing’ang’anie kuajiriwa, bali wafanye kama Ruhigo.

“Alipomaliza shule pamoja na kwamba alifaulu, lakini umaskini ukamfanya asiendelee na shule, lakini hakukata tamaa, saa hizi huyo tunamuona anavyofurahia maisha kwenye kilimo, vijana tuangalie na kilimo kinaweza kututajirisha,” anasema Nyambo.

Kuanzia mwaka 2020, SBL ilianzisha programu ya udhamini wa Kilimo-Viwanda kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wenye vipaji kutoka jamii za wakulima nchini.

Udhamini huo unajumuisha kugharamia ada ya masomo na kutoa mafunzo na uongozi kutoka kwa wafanyakazi wa SBL na wakulima wazoefu. Hadi mwisho wa 2023, jumla ya wanafunzi 300 walikuwa chini ya udhamini wa kilimo-viwanda. Kwa mwaka huu, wanafunzi 40 ndio wamepata ufadhili wa SBL.

Chuo cha Mafunzo ya Kilimo cha Igabiro (ITIA) ni moja ya taasisi nne nchini ambazo SBL imeungana nazo kutoa fursa za mafunzo kwa wapokeaji wa udhamini wake.

Vyuo vingine ni Chuo cha Kilimo Maria Goreti, Kaole Wazazi College of Agriculture, na Kilacha Agricultural College.

Related Posts