Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limeanza uchunguzi wa tukio la kikatili lililodaiwa kufanywa na wanaume watano dhidi ya msichana (jina halijafahamika), mkazi wa Yombo Dovya, Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam.
Msichana huyo anadaiwa kubakwa na kuingiliwa kinyume na maumbile na vijana hao wanaodai kupitia video hiyo kuwa, wametumwa na afande wakimtuhumu (msichana) kutembea na mume wa mtu.
Kipande cha video kinachosambaa mitandaoni kinaonyesha jinsi vijana hao walivyotekeleza tukio hilo ambalo tayari Polisi na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalumu, Dk Dorothy Gwajima wamelilaani.
Leo Jumapili, Agosti 4, 2024, Meya wa zamani wa Ubungo, Dar es Salaam, Boniface Jacob katika ukurasa wake wa X ameelezea tukio hilo na kuwaomba viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan na Inspekta Jenerali wa Polisi nchini (IGP), Camilus Wambura kuchukua hatua.
Mbali ya hao, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Taxameombwakuingilia kati suala hilo.
“Kwa kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania ni mama, Waziri wa Ulinzi ni mama, Waziri wa Wanawake ni mama tunatarajia kuona wakichukizwa zaidi juu ya udhalilishaji na ukatili juu ya mtoto wa kike, wao wakiwa kama wazazi na viongozi wenye dhamana ya kulinda raia wa Tanzania,” ameandika Jacob.
“Askari hao waliomrekodi wakiwa wanambaka na kumlawiti wamesambaza video zake mitandaoni kwa maagizo ya kiongozi wao ambaye amewatuma kumpatia huyo binti adhabu,” amedai.
Akitoa maoni katika andiko hilo la Jacob, Waziri Gwajima ameandika: “Salaam. Ahsante sana kuniTag. Nimesoma na kuwasilisha kwenye mamlaka yenye dhamana ya kuchunguza na kukamata ambayo ni Wizara ya Mambo ya Ndani. Watatoa taarifa kwa nafasi yao.”
“Aidha, kwa namna yoyote ile, taarifa hii inasikitisha na jambo kama hili halifai, ni la kulaaniwa na haliwezi kufumbiwa macho. Iwapo manusura au aliye karibu naye atasoma hizi taarifa wasiogope, watoe taarifa ili manusura apate msaada haraka, ikiwamo huduma za afya, kisaikolojia na usalama.”
Waziri Gwajima amemalizia kwa kusema: “Ahsante, tuendelee kushirikiana kulinda jamii yetu. Sisi ni jamii moja, uovu hapana.”
Dakika chache baadaye, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime akatoa taarifa kwa umma kuzungumzia tukio hilo, akisema wameanza kulifanyia kazi na kulaaniwa, kwa kuwa halikubaliki na ni kinyume cha sheria, maadili ya Mtanzania na hali za binadamu.
“Jeshi limetoa wito kwa wananchi wote waache kuendelea kusambaza video hiyo, kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria lakini pia ni kitendo cha kuendelea kudhalilisha utu wa binadamu mwenzetu,” amesema Misime na kuongeza:
“Tunatoa wito kwa mwenye taarifa ya kuhakikisha mkono wa sheria unawafikia kwa haraka waliofanya ukatili huu asisite kutusaidia kwa kutupa taarifa au kumpatia kiongozi yoyote yule wanayemwamini kwamba taarifa ikimfikia watu hao watapatikana haraka iwezekanavyo.”
Baada ya Polisi kutoa taarifa hiyo, Waziri Gwajima akarejea kwenye ukurasa wa Jacob na kuiweka na kuandika: “Kwa rejea ya taarifa ya @tanpol. Ndugu wanajamii, tuendelee kutoa ushirikiano sasa na daima. Ahsante sana, ahsanteni sana.”