Mwananchi Day 2024… Nyie hamuogopi!

NDIYO kaulimbiu iliyoko mtaani leo katika siku ambayo Yanga wana pati lao la Mwananchi Day kwenye Uwanja wa Mkapa. Wanatamba kikosi chao ni bandika bandua hasa kutokana na mastaa wazoefu waliowaongeza kutoka katika baadhi ya washindani wao ikiwemo Simba na Azam.

Shoo ya leo inafanyika saa 24 tu, tangu Simba nao wafanye pati lao la Simba Day kwenye uwanja huo huo.

Yanga inatambulisha kikosi kipya, jezi mpya na msimu mpya kwa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa Kombe la Kagame 2024, Red Arrows ya Zambia kujiweka sawa kwa msimu mpya kwa klabu hiyo iliyotimiza miaka 89 tangu iliposisiwa mwaka 1935.

Kwa umri wa kibinadamu unaweza kusema Yanga ni kikongwe kwa sasa, kwani miaka 89 si mchezo.

Kama hujui, Yanga ilizaliwa Februari 11, 1935, lakini wikiendi hii itakuwa ikihitimisha Kilele cha Wiki ya Mwananchi inayoambatana na utambulisho wa kikosi kipya sambamba na kutambulisha uzi mpya wa msimu pamoja na burudani nyingine.

Hata hivyo, historia inaonyesha chimbuko la timu hiyo ilianza kati ya mwaka 1926-29 ikiwa na lengo la kisiasa la kuwaunganisha Waafrika katika kudai Uhuru wa Tanganyika.

Inaelezwa Yanga iliundwa na wananchi wanyonge, wengi wakiwa manamba wa mashambani, wachuuzi na Waafrika waliokuwa wakitengwa mbele ya watu weupe (Wazungu na Waarabu).

Wanaoifahamu zaidi klabu hii wanasema ilianza kwa jina la Jangwani Boys kisha kuja kuitwa Navigation kabla ya kubadili jina miaka ya 1930 na kujiita Taliana FC.

Hata hivyo, mwanzoni mwa 1930, Yanga ilibadilishwa jina na kuwa New Young na kisha kuasisiwa rasmi mwaka 1935 na miezi michache baadaye timu iligawanyika kwa baadhi ya wachezaji kujiengua na kwenda kuasisi klabu ya Sundeland (Simba) iliyozaliwa 1936.

Upo mkanganyiko juu ya tarehe rasmi ya kuasisiwa kwake, baadhi wakisema ni Juni na wengine wakidai ni Februari 11, hata hivyo, Yanga ni moja ya klabu kongwe nchini na barani Afrika.

Licha ya kuwa moja ya klabu kongwe nchini, Yanga ambayo ilianza kulitumia jina hilo mwaka 1971 baada ya agizo la aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume aliyezitaka timu zote kuwa na majina ya kiafrika, ina rekodi tamu.

Yanga ndiyo klabu ya kwanza nchini kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa na kuandika historia ya kufika robo fainali ikifanya hivyo mara mbili mfululizo, yaani 1969 na 1970.

Kitu cha ajabu ni Yanga ilifika hatua hiyo na kucheza na Asante Kotoko ya Ghana na moja ya mechi yao iliamuliwa kwa kurushwa kwa sarafu baada ya kushindwa kupata mbabe katika mechi zote mbili za awali.

Achana na rekodi hiyo, Yanga pia ndiyo klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikifanya hivyo mwaka 1998, msimu mmoja tu tangu Klabu Bingwa Afrika ibadilishwe mfumo wake mwaka 1997.

Pia Yanga inashikilia rekodi ya kuwa klabu pekee hadi sasa ya Tanzania kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika tangu michuano hiyo ilipobadilishwa mfumo mwaka 2004, baada ya awali kuwa klabu pekee iliyowahi kufika makundi ya michuano hiyo mara mbili mwaka 2016 na 2018 kabla ya Namungo na Simba kufuata baadae.

Mbali na rekodi hiyo, Yanga pia ilikuwa klabu ya kwanza Tanzania Bara kucheza robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika mwaka 1995, mwaka mmoja tu baada ya Malindi kufika hatua hiyo 1994.

Ni kweli Simba ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), ikitwaa taji mara sita, lakini Wekundu hao kwa Yanga wamekaa.

Ndiyo, licha ya Simba kushikilia rekodi ya kubeba taji hilo mara nyingi, lakini hawajawahi kutwaa nje ya Tanzania, tofauti na Yanga ambao inashikilia rekodi hadi sasa kwa kufanya hivyo.

Vijana wa Jangwani waliandikia historia kwa kutwaa taji la michuano hiyo mwaka 1993 Kampala, Uganda, tena ikienda Kampala kinyonge kulinganisha na watani wao waliokwenda kwa ndege wakiwa ndio watetezi na kurudi mikono mitupu.

Kama kuna watu waliodhani Yanga ilibahatisha mwaka huo, basi walikosea kwani ilirejea tena rekodi hiyo mwaka 1999 walipokwenda kutwaa tena ubingwa huko huko Uganda kwa mara nyingine.

Rekodi zinaonyesha hadi sasa Yanga imetwaa taji hilo mara tano ikiwa nyuma ya taji moja dhidi ya watani wao, huku Azam FC ikifuatia kwa kulibeba mara mbili, mwaka 2015 na 2018 ambazo zote ilitwaa pia ikiwa nyumbani kama ilivyo kwa Simba.

Licha ya kubeba mataji matano ya Afrika Mashariki na Kati, lakini Yanga bado ni Baba Lao katika Ligi Kuu ya Bara kwani tangu ilipoasisiwa mwaka 1965 imetwaa ubingwa mara 30.

Wao ndio vinara wakifuatiwa na watani wao waliobeba mara 22 hadi sasa, pia ndio wababe wa kwanza katika mechi ya watani walipoifumua Simba bao 1-0 Juni 7, 1965.

Katika mchezo huo bao pekee la Yanga liliwekwa kimiani na Mawazo Shomvi kabla ya pambano kuvunjika dakika ya 80 na kugoma kurudiana na watani wao waliokuja kupewa ubingwa mwaka huo wa kwanza kwa kuasisiwa kwa Ligi ya Bara.

Pia kama hujui ni Yanga haohao iliyokuwa ya kwanza kutoa kipigo kikali katika mechi ya watani kwa kuifunga Simba mabao 5-0 katika mchezo uliopigwa Juni 1, 1968.

Mabao ya Yanga yaliwekwa kimiani na Maulid Dilunga na Saleh Zimbwe waliyefunga mawili kila mmoja na Kitwana Manara ‘Popat’.

Hata hivyo, ni Yanga hao hao waliokuja kuandikia historia ya aibu kwa kufumuliwa mabao 6-0 na watani wao Julai 19, 1977 na kwa miaka zaidi ya 40 wanahaha kufuta aibu hiyo bila mafanikio.

Aidha Yanga ndio klabu ya kwanza nchini kunyakua ubingwa wa nchi mara tano mfululizo ikifanya hivyo miaka ya 1968-72, japo Simba nayo ilikuja kufanya hivyo baadaye kati ya 1976-80 na kurudia tena kubeba kwa misimu minne ya hivi karibuni kabla ya Yanga kuamka na kutwaa mara tatu mfululizo sasa.

Pia ni Yanga tena waliandika rekodi ambayo hadi leo haijawahi kufikiwa na timu yoyote katika Ligi Kuu ikiwamo Simba kwa kutwaa mataji mara tatu mfululizo katika vipindi vinne tofauti.

Ilitwaa mara tatu mfululizo kwa mara ya kwanza mwaka 1991-93 kisha ikarudia tena 1996-98, kisha 2007-2010 na kurudia tena 2022-2024.

Kwa sasa Simba inatambia uwanja wake wa mazoezi uliopo Bunju, huku Azam ikitangulia mapema kuwa na uwanja wa kisasa, lakini unaambiwa Yanga ndio baba lao tangu zamani.

Yanga ndiyo iliyokuwa klabu ya kwanza kumiliki uwanja wake mwenyewe, walipoujenga Uwanja wa Kaunda, uliokuwa mitaa ya Jangwani na Twiga yalipo makao yao makuu.

Uwanja huo uliifanya Yanga kufunika kwa klabu za Tanzania kwani walikuwa wakitambulisha vikosi vyao kuanzia vya watoto, vijana hadi timu yao kubwa kwenye uwanjani huo.

Pia waliutumia kwa mechi zao mbalimbali za kirafiki kabla ya mafuriko ya mara kwa mara kuwatibulia na kuufanya uwanja huo ufe, japo hivi karibuni walitaka kuufufua upya na kushindikana.

Hata hivyo, kama hujui, mbali na uwanja, Yanga pia ndiyo klabu iliyokuwa na jengo linaloweza kuwahifadhi wachezaji na viongozi wake kwenye makao yao makuu, mbali na kuwa klabu ya kwanza nchini kuanzisha utaratibu wa kuwalipa wachezaji fedha zao benki.

Mbali na kubeba mataji mengi ya Ligi Kuu, Yanga pia inashikilia rekodi kadhaa za kubeba mataji mengine mbalimbali ikiwamo ya michuano ya Ligi Kuu ya Muungano (iliyorejeshwa mwaka huu iliyoshirikisha timu za Bara na Zanzibar).

Imetwaa michuano ya Kombe la FA/ASFC mara nane (1967, 1974, 1999, 2001, 2015-16, 2021-2022, 2022-2023 na 2023-2024), Kombe la Nyerere, Kombe la Tusker, Kombe la CCM, Kombe la Hedex mbali na kubeba pia Ngao ya Jamii mara saba ikiwa nyuma ya Simba iliyotwaa mara 10 ikiwa ndio vinara.

Licha ya mafanikio makubwa kisoka nchini, lakini Yanga inaweza kuwa klabu iliyowahi kukumbwa na migogoro iliyoacha historia nchini, mbali na ule mgawanyiko uliokuja kuizaa Simba 1936.

Yanga ilikaribia kufutika kama sio hekima zilizotumika kutuliza mambo wakati wa mgogoro wa kihistoria uliotokea mwaka 1976 na kusababisha kuzaliwa kwa Pan Africans na kuibuka kwa utani wa Kandambili na Raizon.

Aidha Yanga miaka ya katikati ya 1990 ilikumbana na kisanga kingine kilicholazimisha hadi serikali kuingilia kati ya Yanga Asili na Yanga Kampuni iliyosababisha kutimuliwa kwa timu nzima.

Mzozo huo uliibuka kutokana na pande mbili za Wafadhili waliokongozwa na kina Abbas Gulamali, Mohammed Viran na wenzake dhidi ya uongozi wa George Mpondela ‘Fidel Castro’ na wenzake kiasi Waziri wa Mambo ya Ndani enzi hizo, Augustine Mrema kuingilia kati.

Kifupi ni kwamba katika miaka 85 ya uhai wa Yanga klabu hiyo imepita kwenye vipindi tofauti vyenye ladha ya utamu wa asali na uchungu wa shubiri.

Hata hivyo, mwisho wa yote ni Yanga bado inaendelea kupambana ikibaki kuwa klabu ya kipekee na ya kihistoria nchini ikiendeleza falsafa yao ya Daima Mbele Nyuma Mwiko. Kwa rekodi hizo nyie hamuogopi?

Related Posts