Tumeumbwa watu kila aina, wabaya hata wazuri. Kwa vile ndoa hufungwa na wanadamu, tunaomba tugusie suala nyeti bila kuonekana kama tunabagua au kuwawekea utu ubaya.
Hivyo, siyo uzushi kusema dunia ina watu wazuri na wabaya. Leo tutaongelea tutakachokiita RST, ni maana ya Roho mbaya, Sura mbaya na Tabia mbaya.
Kwanza, tukubaliane. Kuna watu wenye sifa hizi. Tutaanza na kisa cha kijana mmoja wa kiume mtanashati. Kijana huyu alijaliwa elimu na kazi nzuri vilivyompatia kipato mbali na biashara zake.
Pamoja na yote, kutokana na makuzi yake ya kizazi cha zamani, hakuwahi kuwa kwenye uhusiano kutokana na sababu zifuatazo; kwanza malezi yake yalikataza uhuni au uhuria unaoanza kujitokeza kwa kuigiza wazungu ambapo watu wasiooa au kuolewa huanza mambo ya wanandoa.
Pili, alichelea kuzaa kabla ya kuoa, jambo ambalo hakutaka liwe kikwazo katika ndoa yake.
Tatu, hakutaka watoto wenye mama tofauti aka rangi mbili. Nne, alikuwa mwenye aibu na mwenye kujitunza, vitu vilivyomtenga na mambo ya starehe, alitunza fedha ili baadaye awe na familia yenye maisha mazuri.
Mfano, alijenga nyumba na kununua gari kwa ajili ya shughuli zake za kikazi na kibiashara kabla ya kuoa. Aliogopa kuwakwaza wazazi wake kwa kujiingiza kwenye mambo ambayo, kimila lazima yapate ridhaa yao. Hivyo, alingoja kupata mwenza atakapoamua kuoa.
Pamoja na kijana yule kutotaka kuoa kabla ya kukamilisha malengo yake na kuheshimu taratibu, hakukosa akina dada waliompenda ama kwa sababu ya mwonekano, elimu au fedha alizonazo. Mwenyewe aliendelea kujijenga ili awe tayari kuanzisha familia yake. Siku ya kutafuta mchumba, alipata taabu sana. Kwanza, alikuwa mwenye aibu na ambaye hakuwa na uzoefu wa kuwa na mawasiliano na akina dada, hasa akichelea wangemuingiza majaribuni.
Kadiri siku zilivyokwenda, wadada wengi walimuona mdenguaji au mwenye tatizo. Hivyo, waliacha kumsumbua na kukosa imani naye. Hapa ndipo tatizo lilipoanza.
Akiwa yuko tayari kutafuta mchumba, alijikuta hajui pa kuanzia, licha ya umri kwenda, alikuwa si mwenye sura nzuri na wala hawakuendana na yule kijana si kwa tabia wala sura. Hivyo, tutamuita jimama.
Kutokana na muda kwenda, jimama lilipogundua kuwa yule kijana mtanashati hakuwa na mke wala rafiki wa kike, lilianza kumzoeazoea kiasi cha kuanzisha urafiki wa kawaida. Jimama lilikuwa limeshafanya kila aina ya ufuska, utoaji mimba, uhuni wa kila aina, kuchumbiwa hata kuvunjika uchumba kutokana na tabia mbaya.
Yule kijana kwa kukosa uzoefu akajikuta anashawishiwa na jimama na wakaingia kweye uhusiano. Haukupita muda, akamtegeshea mimba. Kabla ya hata kujua la kufanya, jimama lilihamia nyumbani kwake kwa kisingizio cha mimba yake. Yule mwanamke akafanikiwa kupata mume mwenye muonekano wa kupendeza na fedha. Ni kama ilikuwa ndoa ya mwewe na njiwa. Alimtambulisha kwa wazazi wake, walistuka na kuhofia kulikuwa kuna namna, lakini wasiingilie kwa kuogopa kumvunja moyo mtoto wao au kuingilia chaguo lake. Kijana akamuoa yule mwanamke, maisha yalianza. Alianza kwa kuwa pole kabla ya ndoa, ghafla, akaanza vituko kwa vile alikuwa ameshaolewa na kumzalia mtoto. Mungu hamfichi mnafiki. Akajisahau akaanza kumchuna yule bwana, kwa vile alijua alivyolazimisha ndoa, alihofia huenda jamaa angeamka usingizini na kumpiga teke.
Hivyo, zile tabia zake asili, yaani RST zilianza. Alianza uhusiano na marafiki zake wa zamani.
Baada ya mume kustuka na kuanza kuwa mkali, jimama alikosa kujiamini akaanza kusaka madawa ya mapenzi kwa waganga wa kienyeji, lisijue hakuna dawa ya mapenzi bali tabia njema, uaminifu na mapenzi ya kweli.
Kufupisha kisa kizima, jimama aliishia kuachika. Hivyo, mnaopanga kuoa hata kuolewa, mjiepushe na RST iwe mke au mume. Tabia njema ni silaha, tuliaswa.
Kwa waoaji wasio na uzoefu, washirikisheni wazazi wenu yasiwakumbe yaliyomkuta kijana huyu asiye na hatia. Msikurupukie mahusiano bila kujiridhisha kuwa mnaingia kwa kuzingatia uchaguzi wenu.
RST ni sawa kilema. Haitibiki. Iepuke. Ni vizuri wanandoa wakaendana kulhali japo wakati mwingine mapenzi hayachagui. Muhimu, tusilazimishe ndoa. Haitadumu. Tusitafute dawa ya mapenzi. Hakuna. Tusiingizane mkenge katika ndoa. Tuwaingizao watakengeuka na kulipiza kisasi.