Madarasa vinara wanafunzi kuacha masomo yatajwa

Dar es Salaam. Wanafunzi 306,113 waliacha shule mwaka 2023 huku darasa la nne, kidato cha kwanza na pili wakiongoza, Ripoti ya Best 2024 inaeleza.

Hiyo ni baada ya madarasa hayo kutoa asilimia 55.6 ya wanafunzi wote walioacha shule, huku wadau wa elimu wakitaja umaskini, kutoandaliwa vyema kumudu masomo ya sekondari, ufuatiliaji duni wa wazazi kuwa sababu za mdondoko huo.

Ripoti hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), inaonyesha idadi ya walioacha shule kuanzia darasa la kwanza hadi la saba ni pungufu kwa asilimia 18.19, huku wale wa sekondari wakiongezeka kwa asilimia 10.01.

Uchambuzi unaonyesha, mwaka 2022 walioacha shule ya msingi walikuwa 193,605 ambao walipungua hadi kufikia 158,372 mwaka 2023 na wale wa sekondari wakiongezeka kutoka 134,295 hadi kufikia 147,741, mtawaliwa.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, kati ya walioacha shule ya msingi mwaka jana, asilimia 33.62 ni wale wa darasa la nne na upande wa sekondari, asilimia 79.2 wote walitoka kidato cha kwanza na pili.

Hiyo ikiwa na maana kuwa, darasa la nne waliokacha masomo mwaka 2023 walikuwa 53,260 huku kidato cha kwanza na pili wakiwa 117,018.

Akizungumza na Mwananchi, Mwalimu Richard Mabala amesema anguko la wanafunzi wakati mwingine huchangiwa na mazingira yaliyopo na baadhi ya wanafunzi kushindwa kujua umuhimu wa shule kwa kuona hawapati wanachokitaka.

Uwepo wa vitendo vya ukatili kati ya wanafunzi kwa wanafunzi na walimu kwa wanafunzi, pia ni sababu nyingine inayoweza kufanya wanafunzi kuacha shule.

“Pia, wakati mwingine hali za kiuchumi za familia ni tatizo, mtoto anaona bora aende kufanya shughuli za kiuchumi kwa ajili ya kuhudumia familia,” amesema Mabala.

Katika upande wa kijinsia, ameshauri kuwapo kwa ulinzi kwa wanafunzi hasa wasichana wanapokwenda na kurudi kutoka shuleni kwa kuwa baadhi hukaa mbali na wanakosoma.

“Hali ya daladala si nzuri na rafiki kwa baadhi ya wanafunzi wakati ambao wengine wanatembea umbali mrefu kwenda shuleni peke yao, muda ambao si rafiki ila wanataka kuwahi,” amesema Mabala.

Maoni yake yaliungwa mkono na Mtafiti wa Elimu, Muhanyi Nkoronko anayeeleza ushiriki wa wazazi katika elimu za watoto wao kwa sasa ni kikwazo.

Wazazi wengi wanachoangalia ni mtoto kwenda na kurudi kutoka shule, lakini si kujua amejifunza nini, ameelewa nini na siku yake imekwendaje.

“Hali hii inafanya wanafunzi kushindwa kuona umuhimu wa shule kwa sababu wazazi hawaonekani kujali maendeleo ya watoto wao shuleni,” amesema Nkoronko.

Amesema mdondoko wa wanafunzi kwa upande wa shule za sekondari wakati mwingine huchochewa na kutoandaliwa vyema kwa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba, ili wamudu masomo ya sekondari.

Mbali na mazingira watakayokwenda kukutana nayo, lugha ya kujifunzia kwa baadhi ya wanafunzi huwa ni changamoto inawayofanya kukimbia masomo.

“Katika hili ni vyema kufanya maboresho, ikiwamo ya kisera ili mwanafunzi anapoingia kidato cha kwanza aweze kumudu masomo,” amesema Nkoronko.

Kuhusu maandalizi ya kidato cha kwanza, Oktoba mwaka jana, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu wa Tamisemi, Dk Charles Msonde aliiambia Mwananchi kutokana na kutambua changamoto ya wanafunzi kushindwa kumudu lugha, Serikali ilizindua mkakati wa kuboresha elimu mwaka 2022.

Pamoja na mambo mengine, ulilenga kuwaandaa wanafunzi ili waweze kumudu lugha ya kujifunzia.

Mkakati huo uliozinduliwa, ulitenga muda wa kuanzia Januari hadi Mei kuwa maalumu kwa wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza kujifunza Kiingereza, ili wamudu stadi za kuandika, kusikiliza, kusoma na kuwasiliana.

“Tathimini tuliyoifanya ndani ya miezi mitatu, watoto wa kidato cha kwanza wameonyesha umahiri wa lugha na sasa wanakaribiana na wale wa kidato cha pili,” alisema Dk Msonde alipozungumza na Mwananchi.

Akiendelea kuzungumza na Mwananchi, Nkoronko amesema ugumu wa maisha ndani ya fimilia ni sababu nyingine zinazofanya wanafunzi kuacha shule.

Pamoja na Serikali kutoa elimu bila malipo ya ada, amesema bado wazazi wanalazimika kutumia fedha nyingi katika kuhudumia wanafunzi ili wahudhurie masomo.

Jambo hilo husababisha utoro wa rejareja na wanafunzi hutumia muda wa masomo kufanya shughuli za kujiingizia kipato.

“Pia, matokeo baada ya mtu kumaliza masomo, mwanafunzi anapoona hakuna ajira, waliomaliza wapo mitaani wanaona hakuna ulazima wa kuendelea na shule,” amesema.

Akieleza namna suala hili linaweza kutokomezwa, Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Oscar Mkude amesema ni wakati sasa kuangalia namna ya kuzisaidia kaya maskini ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kuendelea na masomo, badala ya kuingia katika shughuli za kiuchumi kwa ajili ya kuisaidia familia.

Amesema tayari Serikali imekuwa ikifanya hivyo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), lakini ni vyema ikawaita wadau mbalimbali kusaidia katika jitihada hizo.

“Katika hili, Serikali inaweza kuangalia wadau wa maendeleo kupitia yale mashirika yasiyokuwa ya Serikali wanayoweza kufanya masuala ya kijamii, wakawahamasiha kufanya vizuri, ni kweli kila mtu huwa anakuja na malengo yake, lakini ikiomba usaidizi ni vyema zaidi,” amesema Mkude.

Pia, sekta binafsi zilizo na mifuko mbalimbali zinaweza kutumia ziada yao kuchangia mfuko kama Tasaf kuwaongezea hela, jambo litakalochochea kaya nyingi zaidi kufikiwa kwa sababu wao tayari wana mifumo mizuri ya kuwafikia walengwa.

 “Wakati haya yakifanyika, pia watu wahamasishe watoto hawa kwenda shuleni, ada imekuwa si changamoto kidogo baada ya kuondolewa, kuna gharama kidogo ambazo mzazi anazitumia hivi sasa lakini kuna kitu kimepungua,” amesema.

Katika hilo pia, amesisitiza kuwa umefika wakati wa wazazi kuzaa watoto wanaoweza kuwahudumia, kuwapa ujuzi na elimu bora na si kuzaa bila kuwa na mipango na uwezo wa kuwahudumia.

Wakati hili likielezwa, Julai 14 mwaka huu Mkurugenzi Mtendaji waTasaf, Shedrack Mziray aliwaambia wanahabari kuwa upo mpango wa kukwamua kaya maskini unaokwenda hadi mwaka 2025.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts