Lindi. Mafuriko yaliyotokea nchini kati ya Oktoba 2023 hadi Mei mwaka huu, yameendelea kusababisha maumivu kwa wakazi wa maeneo yaliyoathirika na janga hilo, hasa katika Kijiji cha Myumbu wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi.
Mei 4 mwaka huu wilaya hiyo ilikumbwa na mafuriko yaliyoambatana na Kimbunga Hidaya, yaliyosomba mashamba, vyombo, nyumba na vyakula vya wakazi hao.
Jumla ya kaya 207 kati ya 776 zilizopo Kijiji cha Myumbu zimeathirika, huku matumaini ya kula mara mbili kwa siku au tatu kwa kaya 80 yakiwa yameyeyuka.
Mjane Darlin Ngalamba (83) anayeishi na wajukuu zake wanne katika nyumba ya udongo kando ya Mto Wenza, mazao yake yote ikiwamo mihogo na migomba katika shamba la ekari tano, yalisombwa na mafuriko.
Darlin anayetegemea kilimo na ufugaji, kuku wake pia walisombwa na mafuriko na kubaki wawili tu, kati ya 30.
“Baada ya hapo ndiyo tunaangalia utaratibu wa kununua kuku wengine,”anasema mjane huyo ambaye kwa sasa hawezi tena kulima na anategemea misaada ya wasamaria wema kutokana na umri wake mkubwa pamoja na kusumbuliwa na maumivu ya miguu.
Akisimulia ilivyotokea, Darlin anasema: “Tuliamka na mvua ilianza kunyesha kidogo kidogo, mvua iliendelea hadi saa tatu asubuhi maji yakaanza kufurika. Wajukuu zangu wakanambia kuna maji.”
Kutokana na umri wake, ilikuwa vigumu kwa Darlin kutembea mwenyewe kuyakimbia maji hadi maeneo yaliyokuwa salama.
Darlin anasema katika hali hiyo, walitokea wasamaria wema waliosaidiana na mjukuu wake mkubwa kumbeba hadi katika eneo lisilokuwa na maji.
Miongoni mwa wajukuu zake, mkubwa ana umri wa miaka 25 anayefanya vibarua ili kupata fedha za kusaidia familia ingawa hazitoshi.
Darlin anasema baada ya kupata msaada wa kubebwa hadi eneo lisilokuwa na maji, ilimchukua wiki moja kuishi nje ya nyumba yake, akisubiri maji yaondoke na baadaye alirejea.
“Kurudi hapa (nyumbani kwake) vitu vyote hamna; mabeseni na sufuria naletewa na watu kama msaada,” anasema Darlin.
Mjane huyo anasema anatamani kupata msaada haraka kutoka serikalini hasa wa chakula kwa kuwa ndicho kitu muhimu katika uhai.
Mbali na Darlin, mkazi mwingine aliyepoteza kila kitu baada ya mafuriko kusomba nyumba, chakula, vyombo na mifugo yake, ni Abdulrahman Kingoma.
Mkazi huyo wa Kijiji cha Myumbu amebaki bila chakula na mavazi huku akitegemea msaada wa majirani.
Kingoma aliyenusurika kwa sababu mafuriko yalitokea mchana, anasema ingekuwa usiku huenda asingekuwa hai.
“Nilikuwa na ghala la kuhifadhi mahindi na mtama na lilikuwa na mtama gunia moja na nusu limeondoka, banda la kuku limeondoka yaani sina chochote,” anasema Kingoma.
Kwa sasa Darlin na Kingoma mategemeo yao ni msaada wa Serikali, lakini ule waliopewa awali kipindi cha mafuriko (Mei mwaka huu) ulitosha kwa mlo mmoja wa siku.
Rabii Mbonde, mjumbe wa Kamati ya Maafa, anasema hali hiyo ya uchache wa chakula imesababisha malalamiko kutoka kwa wananchi, wakihisi viongozi wameficha misaada.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Myumbu, Hamidu Mnola anasema walipokea kilo 100 za unga, maharagwe kilo 400, mablanketi 100, vyandarua 130, ndoo za maji na magodoro sita, ingawa kaya zilizoathirika ni 207.
Elimu na changamoto za mafuriko
Khadija Makalani, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Myumbu, wilayani Kilwa, anakabiliwa na changamoto ya kuhitimu elimu ya msingi kutokana na ukosefu wa Sh10,000 za kununua sare za shule baada ya alizokuwa akivaa kusombwa na mafuriko.
Familia ya mwanafunzi huyo anayeishi na bibi yake Mariam Gumba, ilipoteza mali na kuishi katika hali ngumu.
Khadija alikatisha masomo kwa takriban wiki nne tangu sare zake ziliposombwa na maji, na sketi aliyopata kwa msaada ilichanika haraka.
Hali ya familia ya Khadija
Mariam Gumba, bibi wa Khadija, anaeleza jinsi familia yake ya watu saba ilivyopoteza mali nyingi kutokana na mafuriko.
Anasema hali hiyo iliwalazimu kulala nje kwa siku tano kabla ya kupata hifadhi kwa muda hadi Oktoba 5 mwaka huu.
Hadi sasa, Mariam hajui wapi watakwenda baada ya kumaliza muda huo itakapofika Oktoba kwa kuwa, familia yake inakabiliwa na ugumu wa maisha.
Mariam mwenye watoto tisa ambao hawana uwezo wa kumsaidia, anategemea kilimo ambacho pia kimeathiriwa na mafuriko.
Mazao yao yote, ikiwamo mpunga na mihogo, yamesombwa na maji, hali hiyo iliyobadili ratiba ya mlo wao kutoka mara mbili kwa siku hadi moja.
Hassan Kingoma, jirani aliyewahifadhi Mariam na wajukuu zake, anasema aliwasaidia kuokoa baadhi ya vyombo vyao huku maji yakiwa yamejaa hadi kiunoni.
Hata hivyo, athari za mafuriko zimepoteza matumaini ya wakazi hao kupata mazao kutokana na kilimo, kwa kuwa maeneo mengi yameingiliwa na mchanga na hayafai tena kwa uzalishaji.
Zubery Utondwe, Ofisa Kilimo wa Kijiji cha Myumbu, anapendekeza Serikali itoe msaada wa mbegu za muda mfupi ili kusaidia wakazi kuotesha mazao na kukabiliana na baa la njaa wanalohisi linalokuja.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilwa, Yusuph Mwinyi, anasema wataalamu wa mazingira wamekwenda kutoa ushauri wa aina ya mbegu zinazohitajika.
“Serikali imeanza kuleta mbegu, lakini bado wilaya inahitaji msaada zaidi kutoka kwa wadau,”anasema.
Mwinyi anasema uongozi wa wilaya unaomba msaada zaidi wa mbegu za maboga, mahindi na kunde kutoka kwa wadau mbalimbali.
Katika Wilaya ya Kilwa, mafuriko hayo yameathiri kata 14 na kaya 1,020 zenye wanafamilia 4,080 na kusababisha vifo vya watu watano.
Jumla ya nyumba 525 zimeharibika na nyingine 495 zikihitaji kujengwa upya, huku wananchi wengi wakiwa kwenye kambi tofauti za wilaya.
Hata hivyo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Julai mwaka jana ilitabiri uwepo wa mvua za El-Nino kuanzia Oktoba 2023.
Mvua hizo kwa mujibu wa TMA, zingesababisha athari katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwamo mafuriko na uharibifu wa miundombinu.
Baada ya utabiri huo, Oktoba mwaka jana, mvua hizo zilianza kunyesha na athari katika mikoa mbalimbali zilijitokeza.
Kilwa, Pwani, Morogoro, Mbeya na Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa mingi iliyokumbwa na athari za mvua hizo.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917. Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation