Jeshi la Polisi nchini limeeleza kuwa limeanza kufanya upelelezi wa tukio linalosambaa kwenye mitandao ya kijamii likimuonyesha binti mmoja anayedaiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam aliyedhalilishwa na kufanyiwa ukatili ambao haukubaliki kwa kuwa ni kinyume cha sheria, maadili ya Mtanzania na ‘Haki za Binadamu’.
Taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa leo, Jumapili Agosti 04.2024 imetoa wito kwa jamii na yeyote mwenye taarifa kuhusiana na tukio hilo kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo na vyombo vingine stahiki ili kwa pamoja ifanikiwe mkono wa sheria kuwafikia watuhumiwa kwa haraka na hatua stahiki zichukuliwe.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David A. Misime ambaye ni Msemaji wa Jeshi hilo imetoa wito kwa wananchi pia kuacha kuendelea kusambaza video kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria, lakini pia ni kuendelea utu wa binadamu ambaye ni mtendwa.
Jeshi la Polisi limetoa namba 0699 99 88 99 kwa yeyote mwenye taarifa zaidi kuhusiana na tukio hilo la ‘kinyama’.
Mapema leo, Jumapili Agosti 04.2024 zimesambaa picha mjongeo (video) zikionesha vijana kadhaa wanaodaiwa kumbaka na kumlawiti binti huyo ambaye anadaiwa kuwa ni mkazi wa jijini Dar es Salaam, kisha baada ya watuhumiwa ambao hawajatambulika hadi sasa kurekodi tukio hilo la ‘kinyama’ na kulisambaza kwenye mitandao ya kijamii