Chunya yamlilia Sauli, wafanyakazi wakihofia vibarua vyao

Mbeya. Halmashauri ya Wilaya ya Chunya imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mwekezaji maarufu na mzaliwa wa wilaya hiyo, Solomon Mwalavila ‘Sauli’, aliyefariki dunia kwa ajali ya gari.

Mwalavila, ambaye alikuwa mmiliki wa mabasi ya Sauli yanayosafirisha abiria mikoani, amefariki dunia leo Jumapili, Agosti 4, 2024 baada ya gari lake kugongwa kwa nyuma na lori la mchanga eneo la  Mlandizi, mkoani Pwani.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Tamimu Kambona, amesema kifo cha Mwalavila ni pigo kubwa kutokana na mchango wake katika uwekezaji na maendeleo ya Chunya.

Ameongeza kuwa marehemu alikuwa mzaliwa na mkazi wa Chunya, na mbali na kumiliki mabasi alikuwa pia na migodi ya uchimbaji ambapo aliajiri vijana wengi.

“Mbali na kuwa mfanyabiashara na mwekezaji, alikuwa mtu wa karibu sana na mimi. Hivyo si Halmashauri pekee iliyopata pigo, bali na mimi binafsi nimeumia sana. Alikuwa mtu anayependa ushirikiano,” amesema Kambona.

Kambona amesema kwa sasa wanasubiri utaratibu wa familia kuhusiana na maziko na si wakati muafaka wa kuzungumzia hatma ya wafanyakazi wake kwa kuwa jukumu liko kwa familia.

Baadhi ya wafanyakazi katika migodi ya dhahabu aliyokuwa akimiliki marehemu  Mwalavila wamesema wamepata pigo kubwa.

Keneth Jackson, mmoja wa wafanyakazi hao, amesema Mwalavila alikuwa msimamizi mkuu wa migodi hiyo, hivyo wanasubiri uamuzi wa familia.

Emanuel Bahati, ambaye alianza kufanya kazi na Mwalavila tangu mwaka 2015, amesema marehemu alikuwa kama mzazi na mlezi kwake.

“Nimeumia sana. Marehemu alikuwa msaada mkubwa kwangu kimaisha tangu nilipoanza kufanya naye kazi mwaka 2015,” amesema Bahati kwa huzuni.

Dany Mussa, mmoja wa wananchi waliomfahamu marehemu amesema, “Hakuwa mtu wa kujikweza hapa Chunya. Alimpenda na kumthamini kila mtu,” amesema Mussa.

Related Posts