Mwanafunzi wa udaktari KCMC ashinda gari droo ya Simbanking

Moshi. Mwanafunzi wa udaktari katika Chuo Kikuu cha Tiba cha KCMC, Hussein Hamisi Hamadi ameibuka mshindi wa gari aina ya Nissan Dualis, kupitia droo ya pili ya shindano la Simbanking ya Benki ya CRDB.

Hussein amekabidhiwa gari hilo ambalo ni la pili kutolewa mwaka huu katika viunga vya Chuo Kikuu cha Tiba KCMC mwishoni mwa wiki mbele ya wanafunzi wenzake, walimu na wafanyakazi wa chuo hicho.

“Najisikia furaha sana kushinda gari hili,” amesema Hussein baada ya kukabidhiwa kadi ya gari, ufunguo pamoja na nyaraka za bima kubwa.

Ushindi wa mwanafunzi huyo wa fani ya fiziotherapia ulitangazwa na Meneja wa Huduma za Benki ya CRDB kwa Simu ya Mkononi, Emmanuel Moshi katika droo ya pili ya mshindi wa gari iliyofanyika mwezi uliopita.

“Ilikuwa ni bahati yake kwa kweli kwani kabla yake, walipigiwa simu wateja wawili. Mmoja hakupatikana kabisa ila mwingine simu yake iliita lakini hakuipokea. Utaratibu unatutaka kumpigia mteja mara tatu na kama hatopatikana au hatopokea basi droo inarudiwa, ndivyo kwa Hussein,” Moshi ameelezea jinsi mchakato huo ulivyokuwa.

Hussein amekabidhiwa gari hilo na Meneja Biashara wa Kanda ya Kaskazini wa Benki ya CRDB, David Peter aliyesema matumizi ya huduma za Simbanking yanazidi kuongezeka na benki inaendelea kuwahamasisha wateja wake kuzitumia, ili kuingia kwenye uchumi wa kidijitali ambao ndio uelekeo wa dunia kwa sasa.

Mshauri wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha KCMC, Anza Lema amesema ushindi wa Hussein umeleta furaha kwa wanafunzi, walimu pamoja na wafanyakazi wa chuo hicho ambao nao wamehamasika zaidi kutumia huduma za Simbanking.

“Wengi hatukuwa tunaamini kuwa unaweza kushinda lakini Hussein ametuthibitishia kuwa ni suala linalowezekana, hamasa imeongezeka miongoni mwetu.”

“Kampeni hii ni ya mwaka mzima. Kila mwezi huwa tunawatangaza washindi wawili wa bodaboda na mmoja wa bajaji. Mshindi wa gari tunampata kila baada ya miezi mitatu. Aprili tulimpata mshindi wetu wa kwanza wa Nissan Dualis na Julai tumempata Hussein. Nawakaribisha wateja wetu wote na Watanzania kwa ujumla kuendelea kutumia huduma za Simbanking ili nao wawe sehemu ya ushindi huu,” amesema Peter.

Tangu zawadi zilipoanza kutolewa, Peter amesema tayari pikipiki nane, bajaji tatu na magari mawili yameshatolewa. Ukiacha vyombo hivi vya usafiri, Peter amesema zawadi nyingine zinazotolewa ni kompyuta mpakato kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, fedha taslimu, pointi za tembo zinazoweza kubadilishwa kuwa fedha taslimu, simu za mkononi, chupa za maji na nyinginezo.

“Lengo la kampeni hii ni kumpunguzia mteja gharama ili afanye kila muamala anaotaka akiwa mahali alipo kupitia huduma zetu za Simbanking. Huduma hii imedumu sokoni kwa zaidi ya miaka 15 sasa, ni njia rahisi ya kupata huduma,” amesema Peter.

Huduma za Simbaking zinatolewa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu ambayo ni salama na ya uhakika, inayowawezesha wateja kupata huduma kupitia simu za mkononi. Kwa sasa, wateja wanaweza kupata zaidi ya asilimia 95 ya huduma kidijitali wakiwa mahali popote.

Ili kushinda moja ya zawadi zinazotolewa na Benki ya CRDB, amesema mteja anatakiwa kufanya miamala mingi kupitia Simbanking kama vile kulipia bili za umeme na maji, kukata tiketi ya usafiri wa ndege, kulipa ada na michango ya shule, kulipia bidhaa zinazouzwa mtandaoni au kununua muda wa maongezi na huduma nyingine nyingi zinazopatikana ndani ya Programu ya Simbanking.

“Sifa zilizowapa ushindi wateja hawa watatu zinawezekana kwa mteja mwingine yeyote wa Benki ya CRDB hivyo niwahimize wateja wetu wote kutoka mahali popote walipo kuendelea kutumia huduma za Simbanking, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kushinda zawadi kemkem tulizonazo,” amesema Peter.

Related Posts