SHIRIKISHO la Soka Ulaya (UEFA) lina sheria na taratibu za kuhakikisha kuna nidhamu ya mapato na matumizi miongoni mwa nchi wanachama wake ikiwa ni pamoja na klabu.
Lengo la utaratibu huu siyo tu kuondoa ‘fedha chafu’ kwenye soka, pia kuhakikisha kuna utamaduni unaofanana katika matumizi ya fedha bila kujali klabu kubwa na ndogo.
Katika utaratibu huu wa Football Financial Fair Play (FFFP) kunatakiwa kuwepo uwiano mzuri kati ya mapato na matumizi ya klabu.
Klabu hazitakiwi kununua kuzidi kiasi, zinatakiwa kudhibiti matumizi au kulazimika kuuza sana ili kuweza kununua sana.
Hapa kwetu klabu hazijawekewa kiasi au namna ya matumizi ya fedha za klabu katika manunuzi ya wachezaji. Hii yawezekana ni matokeo ya historia ambako klabu zilikuwa hazinunui wachezaji wote.
Huko nyuma kulikuwa na wachezaji waliokulia kwenye klabu, waliomaliza mikataba kwingine na walionunuliwa na mashabiki au wanachama.
Kwa jinsi hii hakukuwa na haja ya kuwajibika kwenye matumizi na manunuzi ya wachezaji.
Muda huu tunapokaribia mwisho wa msimu, juhudi kubwa za viongozi wa klabu zinaelekezwa katika kununua wachezaji kuliko kuuza wachezaji.
Sawa, kununua wachezaji ni jambo jema kwa klabu na ni habari njema kwa mashabiki wanaposikia mchezaji mpya kaingia.
Lakini kuna umuhimu wa kuweka uhalali kati ya wachezaji wanaoingia na wanaotoka, pia wanaopandishwa kutoka vikosi vya vijana.
Baada ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kuruhusu klabu kusajili wachezaji hadi 12 wa kigeni, unaweza kuona kuna klabu zina kiu hata ya kununua wachezaji 15 wa kigeni wakati kuna klabu za ligi kuu hazina hata uwezo wa kununua mchezaji mmoja kutoka nje ya nchi.
Migogoro ya klabu zetu na Fifa nayo imeongezeka kwa baadhi ya klabu kushindwa kutumia majukumu yao ya kimikataba au hata ya kiutawala kuhusu usajili wa wachezaji. Matokeo yake, pesa nyingi zimeenda nje kama faini au fidia.
Kuna swali moja nimekuwa nikijiuliza, je kuna klabu ngapi zimeuza wachezaji nje ya nchi? Au tuliweke hivi… Je ni wachezaji wangapi wameuzwa nje ya nchi?
Naamini kabisa majibu ya swali hilo hapo juu litakuonyesha klabu zetu zina hamu ya kununua kuliko ya kuuza wachezaji.
Klabu zina uwezo wa kwenda nje na kununua wachezaji lakini haziweki juhudi kwenye kutafuta soko la wachezaji wake kwa lengo la kupunguza matumizi, kuingiza kipato na kupata wachezaji walio bora zaidi.
Hata tukiachana na suala la kuuza wachezaji nje ya nchi, je ni klabu ngapi zinauziana wachezaji miongoni mwao?
Jibu la swali hili litakushangaza. Idadi kubwa ya wachezaji wanaosajiliwa kutoka klabu moja kwenda nyingine walio wengi ni wale waliomaliza mikataba (Free Agents), wakifuatiwa na wale walio kwenye mikopo (on loan) na mwisho ni wale ambao klabu imeuza mchezaji (sale transfer).
Maswali hayo hapo juu yananipeleka kwenye swali kubwa ni kwa muda gani klabu zinaweza kuendelea kuishi kwa kununua wachezaji huku wakiuza kidogo sana au kutouza kabisa?
Hivi leo ziko klabu nyingi za madaraja yote ambazo ukiuliza msimu wa 2023/24 wameuza wachezaji wangapi, jibu utakalopewa ni sifuri au karibu na hapo.
Katika uzoefu wangu wa uongozi wa klabu zaidi ya miaka 10 iliyopita, sikumbuki kuingia mikataba mingi ya kununua au kuuza wachezaji miongoni mwa klabu za hapa nchini.
Kidogo Mtibwa Sugar FC tulifanya biashara nao biashara wakiuza wachezaji kama Juma Abdul, Bahanuzi na wengine waliotapakaa klabu mbalimbali.
Mtibwa siyo tu ilikuza vipaji, pia ilikuwa na mikataba inayoeleweka kwa wachezaji wake kiasi klabu nyingine ikipiga hodi kutaka kununua mchezaji hawababaiki wanapokaa nayo mezani.
Mtibwa ilikuwa tayari kuongea na kumpa ruhusa mchezaji kuongea masilahi binafsi (personal terms) na kisha biashara inaendelea.
Kwa namna hiyo, naamini mpaka leo Mtibwa itakuwa wanauza wachezaji kila msimu hivyo kupata kifuta jasho kutoka gharama walizotumia kumlea na kumtunza mchezaji.
Kwa leo siwezi kuongelea kinachowakuta Mtibwa kwenye Ligi Kuu pamoja na maono na sera nzuri ya kukuza vipaji na kuuza wachezaji.
Klabu kubwa kama Yanga, Simba na Azam zina uwezo na mvuto wa kuweza kuvutia vipaji na kwenda hatua mbele zaidi ya Mtibwa.
Kwenye michezo ya Shule za Msingi (Umitashumta) na ile ya sekondari (Umiseta) na hata mtaani kuna vipaji vingi wakiamua kuvitafuta.
Klabu hizi na nyingine zikiimarisha vikosi vyao vya vijana wanaweza kuvuna wachezaji wazuri wanaoufahamu utamaduni wa klabu lakini ambao pia wanaweza kupunguza uwiano wa wachezaji wanaonunuliwa na wanaouzwa.
Zaidi kuna ‘mapato ya milele’ ikiwa mchezaji aliyekuzwa klabuni anafanikiwa kuuzwa hata na klabu ya tano tangu aondoke klabuni.
Kama ulikuwa hujui, Mbagala Market (African Lyon?), Simba na TP Mazembe bado zinapata kipato kutokana na jasho la kijana wao Mbwana Samatta kiasi wanatamani auzwe kila siku na asitundike daruga.
Azam FC hivi karibuni imetangaza kuanzisha vituo vya vijana au akademi katika mikoa mbalimbali. Ikiwa jambo hili waliratibu vizuri linaweza kuwaletea faida kubwa kimpira na kifedha.
Siyo lazima wachezaji wote watakaoandikishwa na vituo vya klabu hiyo watafanikiwa kufikia kiwango cha kuchezea timu yao au hata kucheza ligi kuu, hasha, lakini bado wanaweza kuuza wachezaji kwenda klabu nyingine na ligi nyingine ikapatikana fedha ya kuchangia kununua wachezaji na gharama nyingine za klabu.
Huu ni mradi endelevu katika uendeshaji wa michezo. Mchezo unakuwa kwenye kiwango cha kujilisha wenyewe. Kuwa na wachezaji wengi chini ya klabu ni mkakati unaoipa wigo mkubwa klabu ya kupata wachezaji kutoka ndani.
Mfano mzuri ni klabu za Ligi Kuu England (EPL), ambazo hulea na kukuza wachezaji hata 100 na kisha kuwatawanya sehemu mbalimbali kwa mikopo huku wakifuatilia maendeleo yao.
Angalia msimu huu Manchester City ina wachezaji 36 walio nje kwa mkopo huku Arsenal ikiwa na wachezaji 29 walio nje kwa mkopo.
Kwa wanaojua biashara ya michezo, ni hasara kubwa sana klabu inaposajili mchezaji ikamtumia na kisha akaondoka bila kuuzwa.
Hii ina maana uwekezaji wote tangu kumnunua mchezaji mpaka anaondoka unakuwa umekomea hapo. Sioni maendeleo endelevu kwa klabu ambayo imeamua kuishi maisha ya kununua wachezaji bila kuuza. Biashara ya mpira ni kununua na kuuza.
Huko nyuma kulikuwa na tangazo moja lililomnukuu Rais wa awamu ya pili hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi akisema;
“Biashara maana yake ni kuuziana na kununuliana na siyo kuuziana tu au kununuliana tu.”
Kauli hiyo ilitoka katika muktadha wa kuonyesha umuhimu wa ulali wa biashara kimataifa lakini kauli hiyo bado ni muhimu katika sekta ya michezo hasa soka.
Mara nyingi tunasikia katika klabu vya ligi kubwa hasa Ulaya pale kocha anapoleta maombi ya fedha za kununua wachezaji wapya anaulizwa wangapi ameuza ili aweze kupewa fedha.
Wachezaji wananunuliwa kwa kuangalia uwiano wa wachezaji wanaoondoka kwa kuingiza kipato.
Ni wakati sasa kwa kila klabu kujiuliza ni kwa nini kila msimu unakuwa ni wa kununua tu? Ni wakati wa kuweka utaratibu na mikataba mizuri ambayo itawezesha klabu kuuza wachezaji ambao hawahitajiki badala ya kila mara kuwaacha huru huku zikilazimika kuwafidia.
Ni wakati wa klabu kuangalia namna ya kushirikisha mifumo yake ya kutafuta vipaji na mifumo ya kuuza wachezaji.
Mwandishi wa makala haya ni Katibu Mkuu Mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.