Bidhaa feki mipakani pasua kichwa, za sola nazo zaanza kuzagaa

Mbeya. Wakati matumizi ya sola yakionekana kuanza kushika kasi kwa wakulima, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imevielekeza vyombo vya usalama mipakani kuhakikisha inadhibiti uingizwaji holela wa bidhaa hizo zisizo na ubora.

Pia, imezitaka kampuni zinazohusika na uuzaji wa sola na pampu za umwagiliaji kufanya biashara hiyo kwa kuzingatia kipato cha mkulima na mwananchi mwingine, ili kuleta matokeo chanya kama Serikali ilivyolenga.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Agosti 4, 2024 katika maonyesho ya wakulima Nanenane jijini hapa, Ofisa Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari) Uyole, Agustino Ndelwa amesema kutokana na kuanza kushamiri kwa matumizi ya teknolojia hiyo, lazima vyombo vya usalama kuwa makini na uingizwaji wa mitambo hiyo.

Amesema inapotokea fursa yoyote, baadhi ya watu kwa maslahi yao binafsi huingiza bidhaa zisizo na ubora wala kiwango na kuathiri matarajio ya Serikali na kwamba ili kufikia malengo ya Serikali, kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kuongeza umakini.

Amesema Tari imefanya utafiti na kujiridhisha usahihi wa matumizi ya sola kwa wakulima, hivyo kinachohitajika ni kuona mkulima anazalisha kwa tija na haitapendeza kuona gharama zinakuwa kubwa kuliko uwezo wa mwananchi.

“Serikali ilishapitisha matumizi ya teknolojia hii katika kilimo na sisi taasisi ya utafiti tulishajiridhisha ubora wake, japokuwa kwa baadhi ya watu au kundi wasio na nia njema hutumia fursa kama hii kuingiza bidhaa feki, hivyo vyombo vya usalama viwe makini.

“Kuhusu gharama tunajua huenda upatikanaji wa teknolojia hizi hutumia gharama kubwa, lakini lazima kampuni zinazohusika zizingatie uwezo wa kipato cha mkulima na mwananchi” amesema Ndelwa.

Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuona mkulima anafaidika na kilimo chake, lakini kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwamo matumizi ya nishati safi na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Meneja wa kampuni ya Sola ya MySol Mkoa wa Mbeya, Ayoub Mwinuka amesema wanaungana na Serikali kupinga uingizwaji wa bidhaa feki ambazo mbali na kuharibu ustawi wa kilimo, hata biashara huyumba.

Amesema watu wanaojihusisha na uingizaji mitambo isiyo na ubora hufanya kampuni zilizoaminiwa kukosa uaminifu na kwamba suala la gharama hutegemeana na makubaliano ya mkulima.

“Kwanza mteja anapochukua mzigo anakuwa ameiamini kampuni, hivyo sisi MySol tunaungana na Serikali, wale wanaoingiza bidhaa feki wakamatwe ili kutulinda hata sisi tulioaminiwa,” amesema.

Related Posts