Utekelezaji mradi wa maji Busega wafika asilimia 75, kukamilika Oktoba 22

Simiyu. Utekelezaji wa mradi wa maji wa Kalemela-Igalukilo wilayani ya Busega Mkoa wa Simiyu umefikia asilimia 75 na unatarajiwa kukamilika na kuanza kutoa huduma Oktoba 22 mwaka huu.

Mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya Sh3.7 bilioni utakapokamilika utapunguza ama kuondoa adha na ukosefu wa maji safi kwa wakazi zaidi ya 13,018 wanaoishi vijiji vya Mwamagigisi, Lunala, Nyangiri na Malangale wilayani humo.

Taarifa ya maendeleo ya mradi huo imetolewa leo Jumapili Agosti 4, 2024 na Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Busega mkoani humo, Daniel Gagala mbele ya kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Godfrey Mnzava.

“Mradi huu utakapokamilika utakuwa na faida za kijamii ambazo ni pamoja na kuimarisha afya za wananchi kwa kupunguza magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo safi,” amesema Gagala.

Gagala amesema mbali na kutatua changamoto hiyo, utapunguza kero ya kutumia muda mwingine na fedha kwa wananchi kufuata huduma hiyo umbali mrefu, jambo linalowakwamisha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.

Akizungumzia mradi huo, kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Godfrey Mnzava, amewataka wananchi kuulinda kwa wivu mkubwa na kuwabaini watu wenye nia ovu ya kutaka kuuhujumu, huku akiwataka kuhifadhi vyanzo vya maji vinavyochangia maji katika mradi huo ili uwe endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Amesema lengo la Rais Samia Suluhu Hassan ni kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati na yenye tija kwa umma ikiwemo ya maji, afya, elimu na miundombinu.

 Kwa upande wake, Mkazi wa Mwamagigusu, Nkindwa Kipeja amesema kiu yake ni kuona umekamilika na ukitoa maji, jambo litakalowaondolea  maumivu ya kutembea umbali mrefu kufuata maji katika visima.

“Tumekuwa tukitembea umbali mrefu kufuata maji ikiwemo kwa kutembea ama kutumia punda lakini sasa naamini ukikamilika basi tutapata huduma tukiwa nyumbani,” amesema Nkindwa.

Naye, Hawa Msethi ameiomba Serikali kuongeza msukumo ili mradi huo ukamilike Oktoba 22, kama ilivyoahidiwa.

“Hofu yangu ni kuwa kumekuwa na ahadi za miradi  mingi kukamilishwa ndani ya muda lakini hazitimizwi kwa wakati.”

Related Posts