Mhadhiri Udom ataka Muungano ufundishwe shuleni

Dodoma. Ili kuuenzi vema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Serikali ya Tanzania imeshauriwa kuweka somo hilo, litakalofundishwa shuleni kuanzia ngazi za chini katika  pande zote mbili za Tanzania Bara na Zanzibar kwa faida ya vizazi vijavyo.

Ushauri uliotolewa na jana Alhamisi Aprili 25, 2024 na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) katika Shule Kuu ya Sheria, Dk Mohamed Khartoum wakati wa mahojiano na Mwananchi Digital.

Dk Khartoum ambaye familia yake ni wanufaika wa matunda ya Muungano amesema kutimiza miaka 60 si kidogo hivyo juhudi zaidi zinahitajika ili Muungano uendelee kudumu kwa kurithisha kizazi kupitia elimu.

Amesema idadi kubwa ya Watanzania waliopo sasa wamezaliwa baada ya Muungano, hivyo bila juhudi za makusudi za kuweka somo la Muungano kitatokea kizazi kisichothamini urithi huo.

“Sasa hivi  elimu kuhusu Muungano inatolewa wakati wa maadhimisho tu na baada ya hapo kila kitu kinaishia lakini kama somo maalumu likiwepo na kufundishwa kila Mtanzania aliyeko Bara na Zanzibar atajua umuhimu wake kuulinda kwa hali na mali.

“Kwa sasa linafundishwa shuleni kama mtalaa kwa ajili ya kujibu katika mtihani kuwa Muungano ulifanyika Aprili 26, 1964 ili watu kupata alama nzuri za ufaulu lakini baada ya hapo hakuna anayejua zaidi kuhusu umuhimu na kwa nini nchi hizi mbili ziliungana,” amesema Dk Khartoum.

Amedai kwa sasa suala la Muungano limeachwa mikononi mwa wanasiasa wanaolisemea ili kupata alama wakati wa kuzungumza, ingawa kuna wakati mwingine wanapotosha.

“Kwa mfano juzi kuna mbunge ametaka kuingia Zanzibar iwe ni kwa hati ya kusafiria  kauli iliyoleta taharuki kwa watu wengi lakini ukiangalia hiyo ilikuwa zamani na sasa wameiondoa,  sasa mtu akisikia hivyo ni lazima auchukie Muungano kwa kudhani kuna ubaguzi wakati wa kwenda upande wa pili,” amesema.

Aprili 23 akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa mwaka 2024/25, mbunge wa Konde, Mohamed Said Issa alishauri kurejeshwa kwa utaratibu wa kuingia Zanzibar kwa hati ya kusafiria.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo alimjibu Said kuwa wazo ni kuirudisha nyuma nchi kwa kuwa iliishaondoka tangu utawala wa Ali Hassan Mwinyi na Dk Salmini Amour.

Amesisitiza kama kweli Serikali imedhamiria Muungano uendelee na kudumu ni lazima  kuweka nguvu ya ziada ya kuwaelimisha watoto kuhusu suala hilo ili kujua ukweli si kwa kuusikia tu bali kwa kufundishwa na ikitokea mtu anaposha basi wajue jinsi ya kumjibu.

Mbali na hilo, ameshauri wizara inayoshughulikia masuala ya Muungano kuleta vipindi vya elimu ya Muungano kwa wale waliomaliza shule ili kujua suala hilo kupitia redio na vyombo vingine vya habari.

“Nikiwa mmoja wa wanufaika wa Muungano na familia yangu tumeweza kufanya kazi na kupewa haki sawa bila ubaguzi kama Watanzania wengine wanaofanya kazi kwenye taasisi za umma na binafsi,” amesema.

Amesema familia yake imegawanyika wengine wapo Pemba na wengine wapo bara akiwamo baba yake mzazi aliyehamishia makazi yake mkoani Tanga ambako anaishi huko hadi sasa.

“Lakini pia tumechanganya damu na watu wa Tanzania bara kwa sababu mdogo wangu ameoa mchaga na wanaishi vizuri tu na wote wapo huku bara na mimi dini inaniruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja kwa hiyo muda ukifika nitaweza kuoa huku maana huyu niliye naye nilienda kuoa nyumbani,” amesema Dk Khartoum.

Hata hivyo, Dk Khartoum amesema Muungano una manufaa makubwa ambayo kama akitaka kuyaelezea hataweza kuyamaliza kuanzia ngazi za kijamii, kielimu, kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi.

Amesema waasisi wa Muungano huo, hayati Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume walikuwa na nia nzuri ya kuungana hivyo ni lazima utunzwe kama mboni ya jicho.

Amesema kero za Muungano zilizopo zinazungumzika na hazina madhara makubwa ya kuhatarisha Muungano kwa sababu pamoja na kuwepo lakini mazungumzo ya pande zote mbili yanaendelea.

Hivi karibuni Dk Jafo alisema kero nne ikiwamo ya uletaji wa sukari kutoka Kiwanda cha Mahonda Zanzibar kuja Tanzania Bara ni miongoni mwa mambo ambayo bado hayapatiwa ufumbuzi.

Related Posts