Rais Samia aagiza sukari ya viwandani kuzalishwa nchini

Dar es Salaam. Kutokana na Tanzania kuagiza zaidi ya tani 250,000 ya sukari ya viwandani ambayo imetajwa kama upotevu wa fedha za kigeni, Rais wa Samia Suluhu Hassan ameagiza kiasi hicho cha sukari kizalishwe hapa nchini.

Katika kulitekeleza hilo Rais Samia amewaagiza mawaziri wa viwanda, na kilimo kuweka sera nzuri ili viwanda vilivyopo nchini vizalishe sukari hiyo.

“Nina hakika tukivipa kazi viwanda vyetu vya sukari, sukari hii ya viwandani itazalishwa hapa na tutaokoa fedha za kigeni zinazotumiwa kuagiza nje.”

Kauli hiyo ameitoa leo Agosti 4, 2024 wakati akiweka jiwe la msingi ujenzi wa kiwanda cha sukari Kilombero mkoani Morogoro ikiwa ni siku ya tatu katika mwendelezo wa ziara yake rasmi ya kikazi mkoani humo aliyoianza Agosti 2 hadi Agosti 6, 2024.

Rais amesema uzalishaji wa sukari ya jumla ya viwandani na inayotumika majumbani utaokoa pesa za kigeni zinazotumika kuagiza kununulia sukari nje ya nchi.

Amesema kutanuka kwa viwanda vya vinavyozalisha bidhaa hiyo kunatoa uhakika katika nchi.

Katika kuunga mkono hilo, amebanisha kwamba Serikali inasamehe kodi ya zaidi ya Sh246 bilioni kwa viwanda vitano vya sukari hapa nchini, ili viendelee kuzalisha bidhaa hiyo muhimu.

Akielezea umuhimu wa upanuzi wa viwanda unaoendelea hivi sasa ikiwemo vya Mtibwa, Kagera, K4, pamoja na wawekezaji wa Lake Agro na Kasulu, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema wanatarajia ifikapo mwaka 2025/26 Tanzania itajitegemea kwa sukari yake ya ndani.

Bashe amesema kwa sasa mahitaji ya sukari nchini ni tani 650,000 na mwaka huu zitazalishwa tani 520,000 hadi 550,000 na ifikapo mwaka huo Tanzania itazalisha sukari ya ziada.

“Faida ya upanuzi wa kiwanda hiki utaongeza tani 271,000, kuongeza idadi ya wakulima kutoka 9,500 hadi 16,000 na mapato ya wakulima yataongezeka kutoka Sh65 bilioni hadi Sh165 bilioni.

Aidha, Bashe amesema wameyapokea maelekezo ya Rais kuandaa sera itakayosimamia sukari za viwandani ili kuwapa fursa wenye viwanda kuanza uzalishaji na uagizaji.

Hiyo ni kwa sababu sasa hivi uagizaji wa sukari za viwandani unafanyika kwa jumla na unampa fursa kila mtu kuleta kitu ambacho kinaathiri sukari inayotumika katika matumizi ya ndani.

Akizungumza kuhusu upanuzi wa kiwanda hicho kilichopo Morogoro, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amesema ofisi ya msajili inamiliki asilimia 25 ya uwekezaji wa kiwanda hicho.

“Kiwanda hicho kikikamilika Juni mwakani kitakuwa kinazalisha asilimia 50 ya sukari yote inayozalishwa hapa nchini. Ila kwa sasa kinazalisha tani 127,000 hadi tani 272,000,” amesema.

Ameongeza kwamba upanuzi huo umetokana na sera nzuri za Serikali ambapo kuna ajira 4,500 za moja kwa moja na 25,000 zisizo za moja kwa moja. 

 “Kwa saa moja kiwanda hicho kinatumia tani 420 za miwa hivyo miwa itachakatwa mapema na lile suala la athari za mvua za El Nino, litabaki historia.”

Mchechu amebainisha ujenzi utakapokamilika kutakuwa na mtaji wa zaidi ya Sh1 trilioni ambapo kwa sehemu ya Serikali itakuwa ni Sh250 bilioni.  Amesema hadi sasa  zimeshatumika jumla ya Sh470 bilioni ikiwa ni sawa na asilimia 83 ya ujenzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Kilombero Sugar, Guy Williams amesema uwekezaji huo ni miongoni mwa uwekezaji wa pesa nyingi wa kiwanda cha sukari Afrika Mashariki.

Amesema faida ya mradi huo ni kuhifadhi sukari ya ziada na kuiweka kwa miezi 12 ambayo itauzwa hata katika nchi za jirani.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Kampuni ya Sukari Kilombero, Balozi Ami Mpungwe amesema kiwanda hicho kitakuwa cha kisasa, kiteknolojia ambapo kitaiweka Tanzania katika mstari wa mbele kwenye maendeleo ya teknolojia ya kisasa ya viwanda barani Afrika.

Amesema kiwanda kitakamilika Juni 2025 na kitazalisha nusu ya mahitaji yote ya sukari nchini.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema mradi huo unaendeleza hadhi ya mkoa huo kama mzalishaji mkuu wa sukari nchini. 

Related Posts